Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Masache Njelu Kasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi ili nami niweze kuchangia kwenye bajeti hii muhimu sana inayogusa wananchi wengi. Kwanza niungane na wenzangu kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri lakini kwa mipango mizuri sana iliyokuwepo kwenye Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tushukuru kwa namna ambavyo tumepata namba za wakandarasi ambao wanaenda kujenga umeme wa REA III na sisi wananchi wa Chunya kwa namna yake kwenye kata zote 20 tunaenda kupata umeme katika kata zote. Umeme huu utaenda kufika kwenye Vijiji cha Lupa Market, Kambi Katoto, Sipa, Lualage, Mwigi, Liheselo, Bitimanyanga, Mazimbo, Kalangali, Magunga pamoja na Shoga. Sasa hapa Chunya tutaenda kuwa tumewaka vizuri. Tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri ambayo anaenda kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na mambo mazuri anayofanya Waziri bado kwa Wilaya ya Chunya tuna changamoto ya umeme mdogo ambao unafika ndani ya wilaya yetu. Kwa kuwa tunaenda kupeleke umeme mwingi kwenye vijiji vyetu changamoto hii Wizara iweze kuichukua na kuitatua kwa haraka zaidi.

Mheshimiwa Spika, kwenye Wilaya ya Chunya kama tunavyofahamu uchumi wetu mkubwa tunategemea uchimbaji kwa hiyo tuna viwanda vingi vidogovidogo ambavyo vinachenjua dhahabu maarufu kama co-elution. Viwanda hii vinazidi kujengwa kila siku umeme ambao wanautumia ni umeme mkubwa, sasa inafikia hatua watu wengine wanashindwa kutumia umeme huo inabidi wawashe majenereta ili kuweza kukidhi mahitaji ya umeme ambayo yanahitajika. Naomba tuone namna ambayo ni nzuri zaidi kuweza kuongeza umeme wa msongo mkubwa uweze kufika kwenye Wilaya yetu ya Chunya ili mahitaji haya yaweze kuwafikia wananchi wetu vizuri.

Mheshimiwa Spika, pia umeme huu ambao unatoka kwenye kituo cha Mbeya unafika Chunya lakini pia unaenda wilaya jirani ya Songwe ambapo kule kuna mgodi mkubwa sana wa Shanta. Mgodi huu na wenyewe bado wanatumia umeme ambao unapita Wilaya ya Chunya, kwa hiyo, inafikia hatua umeme huu haukidhi mahitaji ya wananchi wa Wilaya ya Chunya. Kwa hiyo, naomba kama ikiwapendeza na bajeti ikiwepo tuweze kujenga power station plant pale kwenye Mji wa Makongorosi ili sasa umeme huu uweze kugawiwa vizuri kwenye Miji ya Chunya, Mkwajuni, Lupa mpaka Kambi Katoto ili sasa kuweza kukidhi mahitaji vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na vijiji hivi kupata umeme lakini pia tatizo kubwa tunalo kwenye REA awamu II, vijiji kadhaa viliweza kupata umeme lakini umeme ambao uliweza kufika ilikuwa takribani kilometa moja au moja na nusu, kwa hiyo, wananchi hawa walikuwa wanaonjeshwa tu ule umeme. Unakuta kwenye kijiji kuna nyumba 20 mpaka 25 ndizo zilizopata umeme, wananchi wengi wameomba na wamelipia lakini mpaka sasa hivi bado hawajaweza kupata umeme. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ni msikivu sana naomba tuone namna bora xaidi kushughulikia suala hili. Pamoja na mambo mazuri yanayoendelea tuweke bajeti ya kutosha ili vile vijiji ambavyo vilikuwa havijaweza kufikiwa kwa maana kuongeza kwenye mitaa umeme huo ziweze kufikiwa vizuri.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kuna vijiji ambavyo vilikuwa kwenye mradi wa TANESCO havikuwa kwenye mradi wa REA kama Igundu, Sangambi, Godima pamoja Itumbi. Mradi huu ulianza zaidi ya miaka mitatu na nusu iliyopita toka 2018/2019 nguzo zimefika kwenye vijiji hivi lakini mpaka leo umeme haujaweza kuwaka. Kwa hiyo, tuiombe Wizara kuona namna ambavyo tunaweza tukapata vifaa kwa maana ya transformer pamoja na mita ili sasa wananchi wale waweze kupata umeme.

Mheshimiwa Spika, vijiji nilivyovitaja hapa ni vikubwa lakini umeme haujaweza kuwaka na kuna baadhi ya vitongoji vimepata lakini vijiji havijapata. Kwa hiyo, malalamiko ya wananchi yamekuwa makubwa na wanaanza kuona kama Serikali hii haiwajali. Kwa hiyo, niombe sana wakati Mheshimiwa Waziri ana wind-up aone namna iliyokuwa bora zaidi na hivi vijiji pia viingizwe kwenye mpango ikiwezekana kwenye hii REA III ili na wao waweze kunufaika na umeme huu na baadaye waweze kuona matunda mazuri zaidi ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan.

Mheshmiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)