Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Spika, nakushuru kwa kunipa nafasi. Kabla sijasahau kwanza nianze kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya.

Mheshimiwa Spika, nami niendelee kusisitiza kwamba Giza Cable Industry huyu mkandarasi ambaye amepewa kazi katika Wilaya nne za Tarime, Serengeti, Butiama pamoja na Rorya, mkandarasi huyu kama alivyosema Mheshimiwa Sagini hapatikani kwenye simu. Sisi kama wakazi wa Mkoa wa Mara kwenye hizi wilaya nne tunapata wasiwasi kwa sababu kama wakandarasi wengine wamekwishaanza kufanya survey lakini yeye mpaka sasa hapatikani. Leo asubuhi nilikuwa naogea na Injini wa Wilaya yangu Rorya anasema hajaona mkandarasi yeyote maeneno yale. Kwa hiyo, kama Bwana Giza ananisikia popote alipo basi ni vema tukafanya mawasiliano ili angalau atuondoe kwenye adha hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo, naomba nishauri mambo mawili ambayo yako ndani ya jimbo langu. La kwanza ni kushukuru kwa kazi kubwa iliyofanyika katika Jimbo langu la Rorya, ndani ya vijiji 87 vijiji 73 vyote tayari vina umeme wa REA. Ni imani yangu kwa Vijiji 14 vilivyobaki vya Kanyamsana, Kabache, Nyamusi, Masike, Nyabikondo, Burere, Wamaya, Nyabihwe, Nyihara, Bugendi, Busanga, Ulio, Tai pamoja na Lalanya navyo vitapata umeme. Ni imani yangu utekelezaji wa REA awamu hii vijiji vyote vitakuwa vimepata umeme.

Mheshimiwa Spika, ni imani yangu Mheshimiwa Waziri atatusaidia pia kutatua kero kwenye maeneo ambayo tayari ndani ya vijiji 73 hivi ambavyo umeme umefika ili angalau maeneo mengine waweze kupata umeme. Kwa sababu hiyo Mheshimiwa Waziri nishauari maeneo mawili, ni kweli umeme umefika kwenye vijiji 73, lakini kwenye kijiji kuna kaya au wakazi wako 20 kwenye center ya Kijiji, unaweza ukaona kwamba kama wako watu 20 ni nyumba tano tu ndizo zinazopata umeme lakini nyumba 15 hazina umeme. Sasa kwa status ya Rorya jinsi ilivyo katika hizo 15 bado unakuta watu 10 tayari wamelipia umeme zaidi ya mwaka mmoja lakini hawajaunganishiwa umeme. Kwa hiyo, unaweza ukaona kwamba wananchi wengi pamoja na kwamba tunawaambiwa ndani ya kijiji chenu wana umeme hawaoni tija ya umeme ule.

Mheshimiwa Spika, atakuambia tu Mheshimiwa Mbunge ninachoona ni nguzo mimi nimelipia nina miaka miwili au mwaka mmoja sijapata huo umeme. Zile kaya tano zilizosalia wanashindwa kulipia kwa sababu wanaona wenzao mpaka sasa hawajatatuliwa tatizo lolote la umeme. Nikuombe Mheshimiwa Waziri kipindi unakimbizana na namna ya kutatua changamoto ya vijiji vilivyosalia nchi nzima tupeleke fedha TANESCO ili wakimbizane kumalizi hivi vijiji vilivyosalia ili hawa watu 15 waliosalia na waweze kupata umeme katikati ya kijiji kwenye maeneo ya centre. Kwa kufanya hivyo utakuwa umetatua tatizo zima la eneo lile.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili nizungumzie kuhusu kukatikakatika kwa umeme. Mimi kwangu ni changamoto kubwa sana, naweza nikawa naongoza kwenye Mkoa wa Mara kwa Jimbo la Rorya kukatika umeme. Changamoto kubwa ni ukubwa wa kilometa za mraba ambazo TANESCO Halmashauri ya Wilaya ya Rorya wanazohudumia. Watu hawa wanahudumia zaidi ya kilometa 344, kutokea Nyamongo mpaka ndani ya jimbo zima ni zaidi ya kilometa 344.

Mheshimiwa Spika, lakini ukifuatilia historia ya umeme ule nguzo zina zaidi ya miaka 40 kwa hiyo zimechoka na kuchakaa. Pamoja na kwamba utakuja kutoa majumuisho na kutoa mwelekeo wa nchi nzima ni kwa nini umeme unakatikatika lakini solution kubwa ni kupeleka fedha za kuboresha miundombinu kwenye maeneo haya. Hizi nguzo za umeme zina miaka 40 sasa kwenye maeneo ambayo kuna chemchem zinaoza halafu zinadondoka ndiyo maana mpaka leo ninavyozungumza kuna maeneo ndani ya jimbo langu watu wana siku tatu hawana umeme. Hivi ninavyozungumza kuna Kijiji cha Chabakenye toka jana mchana hakuna umeme wowote lakini ukifuatilia unakuta miundombinu hii imechakaa.

Mheshimiwa Spika, kwa namna yoyote hata kama Mheshimiwa Waziri atafanya marekebisho ya watendaji mimi niseme kwamba inawezekana hawana wakawa hawana kosa. Kikubwa ambacho anaweza kufanya ni kupeleka fedha ya miundombinu hasa fedha maintenance kwenye maeneo haya ambayo umeme unakatika mara kwa mara. Pamoja na kwamba atakuja na suluhisho lingine lakini aamini nachosema umeme huu kwa maeneo haya nguzo zina muda mrefu sana toka zimeoteshwa. Akitatua hilo pamoja na mengine atakayokuja nao naamini kwenye halmashauri hizi ambazo ziko pembezoni atakuwa amewaokoa kwa kiwango kikubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)