Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bumbuli
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JANUARY Y. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa fursa hii. Nami nitumie nafasi hii kuipongeza Wizara kwa kazi nzuri inayofanya. Sisi kwetu katika Jimbo la Bumbuli tuna changamoto za vijiji vingi ambavyo havina umeme, lakini nimeongea na viongozi wa REA na Wizara na wametoa ahadi kwamba maeneo yote ambayo hayana umeme yatafikiwa.
Mheshimiwa Spika, hoja yangu ya leo kwenye Wizara hii ni suala la nishati ya kupikia. Nishati ya msingi kuliko zote ni nishati ya kupikia. Kila nyumba kunapikwa na kila siku kunapikwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mahitaji ya nishati hapa nchini unaweza usiwe na umeme wa kupigia pasi au wa kuwasha taa au wa kupooza vinywaji lakini lazima utafute nishati ya kupikia. Kwa hiyo, tunapozungumza suala la nishati kama wawakilishi wa wananchi hatuwezi hata siku moja kuacha kuweka mkazo na msisitizo wa nishati ya kupikia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hapa Tanzania asilimia 92 ya Watanzania wanatumia nishati inaitwa tungomotaka (biomass), yaani kuni na mkaa kupikia. Naomba nirudie; asilimia 92 ya Watanzania wanatumia kuni na mkaa kupikia. Ukichukua matumizi yote ya nishati katika shughuli zote hapa nchini iwe mafuta, gesi, hydro bado nishati ya tungomotaka (biomass) kwa maana ya kuni, mkaa, pumba na kadhalika ni asilimia 80, inashinda hata mafuta yote kwenye magari na mitambo na inashinda hydro zote. Naomba nirudie; ukichukua total primary energy consumption hapa nchini, energy zote tulizoweka kama mitambo na kadhalika bado energy ya tungomotaka ndiyo inaongoza. Ushauri wangu kwa Wizara, nafahamu iko Sera ya Nishati, lakini kutokana na ukubwa na umuhimu wa biomass (tungomotaka) yaani kuni na mkaa, lazima kuwe na sera tofauti ya kutusaidia kama Taifa kuendesha eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, thamani ya mnyororo wa biashara ya mkaa hapa nchini ni kubwa kuliko thamani ya export za mazao yetu yote; ni kubwa kuliko kahawa, chai au korosho. Thamani ya mnyororo wa mkaa, value chain ni karibu dola bilioni moja, siyo biashara ndogo. Revenue ya mkaa Dar es Salaam peke yake mwaka jana ilikuwa ni karibu shilingi bilioni 800; hii ni sekta kubwa mno ambayo kama Serikali na kama Wizara hatuwezi kuipuuza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nafahamu kuna hoja kwamba tunasambaza umeme vijijini ili tunusuru misitu ili umeme utumike kupika. Mji unaoongoza kwa usambazaji wa umeme hapa nchini ni Jiji la Dar es Salaam, asilimia karibu 96 ya Jiji la Dar es Salaam lina umeme. Hata hivyo, mji unaoongoza kwa matumizi ya mkaa hapa nchini ni Dar es Salaam ambapo asilimia 70 ya mkaa wote unaotumika Tanzania unatumika jiji moja. Kwa hiyo, kwa hoja hiyo, itachukua muda mrefu sana kwamba huu umeme tunaousambaza ndiyo utuokoe kutoka kwenye matumizi ya mkaa na kuni. Kwa hiyo, zinahitajika jitihada za makusudi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, inasemekana mkaa ni nishati ya wanyonge. Ni kweli lakini si kweli; humu Wabunge wengi na viongozi na watu wenye uwezo mzuri wa fedha wananunua mkaa, lakini wananunua kwa gunia, wanyonge wananunua kwa kopo. Kwa hiyo, ukipiga hesabu, chakula ambacho nimetumia mimi kwa mkaa wa 70,000, mnyonge anakuwa ametumia kwa 180,000 kwa sababu ananunua kwa kopo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa suala la kuni na mkaa na nishati ya kupikia limekaa maeneo mengi. Biashara ya mkaa inadhibitiwa na TFS (Wakala wa Misitu Tanzania) ambao ipo Wizara ya Maliasili na Utalii; Sera ya Nishati ya Nishati ambayo inahusika na mambo ya nishati ya kupikia iko Wizara ya Nishati; masuala ya hifadhi na mazingira yapo Ofisi ya Makamu wa Rais. Kwa hiyo, naamini kwamba huu mkanganyiko na mtapakao wa udhibiti wa jambo hili muhimu ukifanyiwa kazi vizuri, basi tunaweza kupata manufaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi kama viongozi wa wananchi katika jambo ambalo tunaweza kuwatendea haki Watanzania ni kuhakikisha kwamba tunaondoa umaskini wa nishati, unaitwa energy poverty.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. JANUARY Y. MAKAMBA: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)