Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Viwanda na Biashara napenda kuchangia mambo yafuatayo zaidi ya yale niliyochangia;
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda na Biashara itoe elimu ya biashara kwa wananchi kwa kupitia Maafisa Biashara wa Wilaya na Mikoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda na Biashara ijitangaze kwenye internet kwa maana ya kutangaza fursa zilizopo Tanzania ili wawekezaji waweze kuona fursa hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya SIDO vijengwe mpaka Wilayani ili viweze kutoa elimu kwa vijana kwa sababu viwanda vingi viko Mikoani sehemu nyingi Wilayani hakuna viwanda vya SIDO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamiliki wa viwanda waangalie afya za wafanyakazi kwa sababu kuna viwanda vingine vinazalisha sumu kama maji ya sumu na unakuta wafanyakazi hawapewi Boot za kufanyia kazi au vitendea kazi. Nashauri Wizara iwe na Wakaguzi watakaokuwa wanakagua viwanda hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri katika hotuba yake, ukurasa wa 13 anasema kuna viwanda 37 vimefungwa, nashauri Waziri aje na plan kuonesha kwamba atafufua vipi viwanda vilivyobinafsishwa, ambapo tulikuwa na viwanda takribani 474. Pia atueleze mikakati ya hivyo viwanda 37 ikoje. Je, inaweza kuvunjwa kwa sababu katika kubinafsisha kiwanda kuna mkataba umesainiwa, je mikataba ya viwanda hivyo ikoje? Inaweza kuvunjwa bila madhara kwa Serikali kulazimika kulipa fedha nyingi kwa ajili ya kuvunjwa mkataba?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri aje na Plan, atuambie ataanza kujenga viwanda vya aina gani, vya kilimo nikiwa na maana, viwanda vya mbolea au viwanda vya nguo au viwanda vya chuma?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda na Biashara iwasiliane na Halmashauri ili ziwe zinatenga maeneo makubwa ya kujenga masoko na Mikoani ili wananchi waweze kuuza biashara zao. Mara nyingi unakuta Halmashauri inatenga maeneo madogo ya masoko tena mengine hayana hata Parking, matokeo yake wananchi wanapanga bidhaa chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu kama barabara, reli iboreshwe ili wawekezaji waweze kuvutiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme ni wa shida, Mkoa wa Katavi hauna umeme wa Grid wanatumia umeme wa jenereta. Kwa hiyo ili kuwezesha Katavi kuwa Mkoa wa viwanda inatakiwa Mkoa upate umeme wa grid.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji bado ni tatizo nchi nzima, viwanda haviwezi kijengwa bila maji, maana viwanda vingi vinahitaji matumizi ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijengwe viwanda vya kuchakata mazao ya asili kama pamba, mahindi, karanga, alizeti, ngozi, na tumbaku katika maeneo yanayozalisha hayo mazao bila kusahau mbao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji itumie ardhi kama mtaji kwa wananchi.