Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi ya kufunga dimba, nami nichangie katika Wizara yetu ya Maliasili na Utalii.

Kama kawaida, kwa dhati ya moyo kwa kweli napenda kushukuru na kumpongeza shemeji yetu Wana- Kilombero, Waziri wetu Dkt. Ndumbaro kwa maana mama yetu anatoka kule na Naibu Waziri, Mheshimiwa Mary kwa sababu hawa walikuja Jimboni kwetu mapema sana na wakatusaidia kufanya jambo kubwa kabisa kuliko mambo mengine makubwa ya utalii na kulinda rasilimali ambayo haijawahi kufanyika maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mara ya kwanza watu waliona askari wakifukuzwa hadharani baada ya kupatikana ushahidi wa kutosha kwamba askari wale walikuwa wanatuhujumu na kunyanyasa wananchi. Kwa hiyo, tunamshukuru sana kwenye jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nashukuru kwa suala la soko. Alijibu hapa juzi Mheshimiwa Waziri kwamba yale maelekezo yake ya kutujengea Soko la Samaki zuri pale kwenye Daraja la Magufuli, yapo kwenye bajeti hii. Nami nawaomba Waheshimiwa Wabunge jamani tuchangie tuboreshe mwisho wa siku tupitishe bajeti hii ili Wana- Kilombero wapate Soko hili la Samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nataka nikuambie, kuna kijana mmoja hapa wa Kilombero, anasoma Chuo Kikuu hapa, ni engineer amechora soko zuri sana kama ishara ya Panton lililowahi kuzama zamani na wananchi na likaua watu. Ametengeneza soko simple la aina ile ambalo litakuwa na eneo la kupigia picha ili kuvutia watu wanaotaka kupiga picha kuonekana kwa daraja lile, lakini kuonekana kwa viboko na kuonekana kwa mamba ambao wanaenda kuota jua katika Mto Kilombero. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri na hata Katibu Mkuu wetu, nimeambiwa analifanyia kazi suala lile la ombi letu la kupata eneo la mita 50 katika Tarafa ya Mang’ula Corner. Nimemwomba sana Mheshimiwa Waziri na namwomba tena Katibu Mkuu wa Wizara mfikirie, kwa sababu Mkandarasi yuko site, ameanza kutandika lami. Sasa katikati pale kuna eneo linaitwa Mang’ula Corner, barabara imejikunja sana. Kunyoosha ile barabara Mkandarasi ameshindwa kwa sababu eneo ni la kwenu, anaambiwa zile mita 50 zilizoingia ni za Udzungwa kwa hiyo hawezi kunyoosha barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri anisaidie, nitafurahi sana akirudi hapa akituambia kwamba tumepatiwa eneo lile na Mkandarasi; na Waziri wa Ujenzi ametuambia wazi kwamba akipata jibu lako anaweza kumwambia Mkandarasi akachonga ile barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, sisi tulipata nafasi, mimi na baadhi ya Wabunge kabla hatujawa Wabunge, Mheshimiwa Dkt. Kiruswa na kaka yangu Mwana-FA tulipanda Mlima Kilimanjaro mwaka 2019; na tulipofika pale juu tulifikisha picha ya Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kama ishara ya kumuenzi kwa mazuri ambayo alifanya katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kushuka katika Mlima Kilimanjaro tuliandika mawazo na maoni yetu. Maana wageni wengi wanaotoka na tunaokutana nao kule juu; ni safari moja nzuri lakini ni hatari sana na safari ngumu. Wanafika pale juu, wanapopiga picha kwenye ule ubao pale kileleni, tulishauri kuwe na picha ya Baba wa Taifa upande wa kushoto na upande wa kulia wa kile kibao kuwe na picha ya Rais ambaye yuko madarakani. Naomba Wizara wajaribu kulifanyia kazi suala hili. Kufika pale juu, kileleni siyo mchezo. Sasa mtu akifika pale, anakutana tu na maandishi kwamba “Hongera umefika juu ya kilele cha juu zaidi Afrika.” Sasa kungekuwa na zile picha; ya Baba wa Taifa na Rais ambaye yuko madarakani, ingekuwa jambo zuri sana kwa utambulisho wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepanga pia na baadhi ya Wabunge na tutamwomba Mheshimiwa Waziri atusaidie kwamba mwaka huu Mungu akipenda tutapanda tena Mlima Kilimanjaro, tutapandisha picha ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuionyesha Afrika na kuiambia dunia kwamba Tanzania ina thamini akina mama, inapenda wanawake na kwamba wanawake wanaweza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wale Wabunge ambao wameagana na nyonga zao, wako tayari kupanda Mlima Kilimanjaro, wanione, tuliongeze lile group ili tupande pale juu tufikishe picha ya Mheshimiwa Mama Samia pale juu kileleni.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Asenga, mimi mwenyewe nilishapanda huo mlima, wala huna haja ya kuagana na nyonga Waheshimiwa Wabunge. Mjiandae tu, hata ambaye nyonga yake hawajaagana, anao uwezo wa kupanda mlima.

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, sawa sawa. Yeyote ambaye yuko tayari, tupande wote Mlima Kilimanjaro na tufikishe picha hiyo ya Mheshimiwa Mama Samia kumuunga mkono kwa mambo mazuri anayofanya katika nchi yetu na hususan mambo yale ambayo yanaongeza sekta ya utalii kwa ujumla na kuondoa zile dhana potofu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimdokeze Mheshimiwa Waziri jambo moja. Nimekuwa nikipata meseji nyingi sana kutoka kwa Kiongozi wa Wavuvi wa Ifakara anaitwa Shaibu Majiji; baadhi ya askari tena wameanza kunyanyasa wavuvi kinyume na maelekezo yako. Ulielekeza wavuvi wale wakienda kuvua, wavue kwa utaratibu kule kwenye maeneo ya hifadhi; wavue kwa nyavu zinazotakiwa, wavue samaki waondoke nao, wasijenge. Walikubali kufanya hivyo na walifurahi ahadi yako ya kujenga soko. Sasa kuna maneno maneno yameanza, kwa hiyo, naomba ulifatilie hilo, uone namna gani hawa askari wetu wazuri wa TAWA ambao wengine uliwapandisha vyeo, wanaoweza kusimamia maelekezo yako vizuri.

Mheshimiwa Waziri, lingine tunaloliomba, sisi ukivuka daraja la Magufuli kuna eneo linaitwa Limaomao, liko karibu zaidi na Mbuga ya Nyerere na zamani Selous, tulikuwa tunaomba Wizara yako ifikirie namna ambavyo mnaweza mkaweka geti pale, kwa sababu ni njia rahisi sana ya game drive ya kuingia Nyerere na kwenda Selous na itakuwa imeongeza mapato yetu. Ni kwamba ukivuka daraja la Magufuli pale kushoto, kuna njia zamani ilikuwa inatumika kwenda Mbuga ya Selous ambayo sasa hivi ni Nyerere. Kama tukipata geti pale, itatusaidia kuchangamsha mji wetu wa Ifakara na Jimbo letu la Kilombero. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri, lingine ni tembo. Ukivuka Daraja la Ruaha, unaanza Jimbo la Kilombero kilometa takribani 35 unapakana na Mbuga ya Udzungwa. Mbuga hii ya Udzungwa ina tembo wengi sana na ni hifadhi yetu, nami naelewa concern yenu ya kulinda hifadhi yetu kwa sababu siyo mali yenu ni mali yetu sisi sote wananchi. Kuanzia hizo kilometa 35, tembo wanavuka kutoka Udzungwa wanaiongia chini upande ambao wananchi wanaishi. Changamoto ni kubwa kweli kweli. Naomba mwapatie askari wale zana ili waweze kufika kwa wakati maeneo ya wananchi kuwafukuza tembo wanavyoingia mara kwa mara.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua kuna issue ya ushoroba na kwamba mmejenga daraja pale kama Serikali la kuhakikisha mnapitisha tembo kwamba wale tembo wanaenda kusalimiana, yaani kuna mashemeji wako Udzungwa, kuna wake sijui wako kule Nyerere, kwa hiyo, wanapita kila mara kwenda kusalimiana huko kama alivyosema Naibu Waziri, mmetengeneza njia maalumu chini ya daraja, mmejenga kwa daraja zuri kwamba wanavuka vizuri; mnawatengenezea fence. Tunaliunga mkono jambo hilo lakini kwa kweli kwa dharura sasa hivi, Askari wetu wale wanatakiwa kupewa magari, kupewa mafuta wafukuze tembo.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nimeenda kwenye msiba, tembo ameua mtu pale; na issue sana siyo fidia ndogo au fidia kubwa; ni mbinu gani tunafanya kuhakikisha tembo hawaui watu? Tembo wanapita kwenye njia yao, wakikua banda la mtu la udongo anaishi humo ndani, wanagonga, wanaenda mbele huko kula mpunga. Tembo wanapenda mpunga kweli Mheshimiwa Waziri. Sasa wasije wakatutia njaa kule tunakoenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, nisiseme mengi, nataka kuwaomba Waheshimwia Wabunge hapa watusaidie tupitishe hii mambo ili tupate lile soko na ile issue ya Mang’ula Corner.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, ahsante sana. (Makofi)