Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Butiama
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JUMANNE A. SAGINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami nikupongeze, umeenea vizuri. Nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa kwanza mchana huu kwenye sekta ya maliasili. Naomba nianze kwa kuungana na waliozungumza asubuhi kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Wataalamu wote wa sekta ya utalii kwa kazi nzuri wanazofanya kuinua na kuendeleza Sekta ya Utalii pamoja na changamoto mbalimbali zikiwepo Covid 19 zilizoikabili Taifa letu mwaka jana 2020 na sehemu ya mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze zaidi na ninaona hili analifanya sana Naibu Waziri la kuhamasisha utalii wa ndani. Tukiweza kwa kweli kuwafanya Watanzania wengi kufanya utalii kwenye hifadhi zetu, tutakuwa tumechangia kwa kiwango kikubwa sana uchumi wa nchi na vile vile tutakuwa tumewafanya wananchi wafaidi rasilimali zao. Haipaswi watu tulio na rasilimali nyingi namna hii tuendelee kuzitazama kupitia runinga, kwenye picha na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo nami niwashajiishe Wabunge wenzangu, kinachofanywa na TANAPA pale nje tukitekeleze. Wanatuomba tukashiriki Ngorongoro. Mimi nipo tayari, nadhani na Wabunge wengi watakuwa tayari kwenda Ngorongoro, kama njia ya kuimarisha utalii wa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawapongeza kwa kuanzisha TFS kama taasisi ya kusimamia eneo la misitu. Yako maeneo ya kuzungumza kwa ajili ya kuboresha, lakini kwa ujumla taasisi hii inatimiza wajibu wake vizuri maeneo yaliyo mengi ukiacha changamoto za hapa na pale, hasa nguvu inapotumika kupita kiasi. Ushauri wangu kwenye maeneo haya hasa TFS na maeneo mengine, kuendelea kutoa elimu. Tusichoke kutoa elimu kwa wananchi wetu na Umma kwa ujumla ili kuimarisha uvunaji wa miti au misitu endelevu na kuendelea kupanda miti mingine ili kuhakikisha kwamba nchi yetu inabaki kuwa salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitegemea sera za mabavu hazitatufikisha mbali sana, utaendelea kutengeneza uhasama kati ya wananchi na Serikali yao. Jambo ambalo kwenye eneo hili linanipa shida kidogo ni pale ambapo mtu ameotesha miti yake mwenyewe, wala TFS hawakuja kumsaidia, akitaka kuvuna mti mmoja au miwili, anawekewa conditions nyingi bila sababu za msingi. Nilidhani hapa tungewatambua watu ambao wamejitokeza kuotesha misitu na wanapotaka kuvuna kwa kweli wasiandamane na masharti. Haya iwakute wale ambao wanakwenda kuvuna bila kuchangia kuotesha miti hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo nataka kuzungumza ni juu ya utalii kwa ujumla kitaifa na ninataka niangalie kanda zetu. Naipongeza nchi yetu kuwa na rasilimali za utalii karibu kila kona ya Tanzania; Kusini mpaka Kaskazini, Magharibi hadi Mashariki, kote kuna vivutio vya ama hifadhi au mapori tengefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani utakubaliana nami kwamba set up ya utalii wa nchi yetu, pamoja na kwamba maliasili zimetawanyika nchi nzima, ziko circuit zaidi towards the North, wakati vivutio vingine viko towards the west, towards the South, na East na kadhalika. Nataka niwaombe wakati ambako Kaskazini wamefanya vizuri sana, nataka niwapongeze kwa kweli, wapo wajasiriamali, wasafirishaji, watu wa kupokea watalii, hoteli nzuri, barabara nzuri na kadhalika; na hata customer care ipo vizuri, ni jambo jema sana. Ila najiuliza, hivi ilitokea kwa dharura tu hawa wakawa wazuri hivyo, kanda nyingine wakawa washamba? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake najiuliza, iweze kwa mfano umbali wa kufika Serengeti kutokea Mwanza haizidi kilometa 140, lakini kwa nini tumlazimishe mtu anayetaka kutembelea Serengeti ashuke KIA aanze kutembea kilometa zote hizo, kwenye risks zote za barabarani, mpaka aje kuifikia Serengeti, apite Ngorongoro, apite Manyara, is too much! Wakati bahati nzuri wenzetu wa Uchukuzi wamefanya kazi kubwa kuimarisha uwanja wa ndege wa Mwanza, sasa unaitwa Uwanja wa Kimataifa, sasa tunatamani kuona watalii wa Kimataifa wanaolenga kwenda Serengeti washuke Mwanza. Wakifika kule, watapata fursa ya kutembelea hiyo west circuit yote; wataona Rubondo, Saanane, Ibanda Kyerwa, Ibanda Rumanyika, Burigi Chato, Gombe, Fukwe za Ziwa Victoria and so forth and so forth. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili nawaomba Wizara, mje na mpango na mkakati madhubuti wa kufanya ukanda wa Magharibi nao pia uwe busy kwenye maeneo ya Kitalii kama ilivyo ukanda wa Kaskazini. Kinachoshangaza, unapita pale Serengeti Ndabaka Gate wala huoni pilikapilika za watalii wakiingia, lakini ukienda upande mwingine kwa kweli shughuli zipo nyingi za kutosha. Kwa hiyo, ni ushauri wangu kwamba hilo tuliangalie kama kweli tunataka kuimarisha maeneo yote ya nchi yetu yanufaike na hizi rasilimali tulizonazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni kuzungumzia ushirikiano wa Wizara zinazogusa utalii kwa njia moja au nyingine. Nilikuwa naziangalia hapa karibu Wizara nyingi tu, karibu zote, labda nusu; Wizara ya Maliasili yenyewe, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Wizara ya Nishati, Wizara ya Mawasiliano, mention Wizara zote; Wizara inayoratibu watu wa dini, kuna makongamano ya Kitaifa na ya Kimataifa ya Dini, tukiweza hawa wote kuwahamasisha wakaja kwenye dini zao, lakini wakaenda kwenye utalii, tutakuwa tumechangia kupata rasilimali nyingi za fedha za kigeni. Tuna taasisi nyingine hata za ndani, Scouts wanaweza wakahamishiwa wakaenda huko kufanya mikutano yao, lakini wakaenda kwenye utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumaliza ya Kitaifa naomba niguse Butiama. Hapa nina jambo moja, naomba Mheshimiwa Waziri anisikilize. Pale Butiama kuna hifadhi inaitwa Hifadhi ya Taifa ya Msitu wa Kyanyari, lakini kwa kweli ukiangalia vile vilima vya Kyanyari hakuna msitu, ni mlima tu umenyanyuka wenyewe hivi labda na majani mafupi, hakuna mti hata mmoja, lakini mmeita hifadhi na ika-cost watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wamekuwa pale tangu mwaka 1974, mmeenda kuweka beacons mwaka 2013 na mkaondoa kaya 220 kwenye hekta zao walizokuwa wanazimiliki na kufanya shughuli za kiuchumi 1,500. Sisi tunasema, lingefanyika sawa, lakini liwe shirikishi. Wananchi hawakushirikishwa, vijana wanakuja TFS kutoka Musoma, wakabandika ile, wakaondoka. Linalowakera wananchi wa pale, wakati mnasema hii ni hifadhi, ameibuka huko mwekezaji wa madini, amepewa vibali vya kuwa na vitalu kumi kwenye eneo lile lile. Sasa tunajiuliza hapa, kama unawaondoa hawa kwa ajili ya hifidhi, iweje leo ukaribishe mwingine aendelee na shughuli za uchimbaji na utafutaji wa madini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho naomba niseme moja hili la utalii Butiama. Butiama ni kwa Baba wa Taifa. Watu wanakwenda pale mara nyingi, lakini naona wanaishia kufanya ibada kwenye kaburi la Baba wa Taifa na kuondoka au kupita kwenye ile makumbusho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Butiama ni eneo ambalo lina vitu ambavyo wangeweza kujifunza vya kitamaduni. Mfano, tuna makabila yasiyopungua 10; kuna Wairegi, Wakenye, Wakirobha, Wakabwa, Wazanaki, Waluo, Wajita, Waruri, Wakwaya, Wasimbiti, Wasukuma na kadhalika. Haya makabila, ni faida, kuna tamaduni pale. Vyakula vyao ni tofauti; kwa hiyo, nilidhani mje mtusaidie...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Haya, ahsante.
MHE. JUMANNE A. SAGINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)