Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Twaha Ally Mpembenwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibiti

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami kuweza kuchangia katika Wizara hii ambayo ni muhimu sana katika mustakabali mzima wa uchumi wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kuchangia, nilikuwa naomba nichukue fursa hii kwanza kabisa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri wake kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wameendelea kuifanya kwa muda mrefu sana katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nichukue fursa hii kukupongeza wewe mwenyewe binafsi, hicho kimekupendeza kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu umegawanyika katika sehemu kubwa mbili; nitachangia Kitaifa halafu nitarudi pale Jimboni kwangu Kibiti ambapo tuna matatizo makubwa sana ya msingi katika sekta hii au katika Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuwa nimepitia vizuri zaidi hotuba ya Mheshimiwa Waziri, haikuweza kutueleza kwa kina zaidi katika baadhi ya maeneo fulani fulani, lakini naomba niguse maeneo mawili tu. Eneo la kwanza nitagusa katika suala zima la utalii wa ndani, halafu eneo la pili, nitagusa katika suala zima la country tourism.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala zima la utalii wa ndani, Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake hakutuambia hasa mikakati ya Serikali au mikakati ya Wizara; nini tunachokwenda kukifanya ili kuweza kuhakikisha utalii wa ndani vile vile nao unakwenda kuchangia katika pato la Taifa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kuna mambo mengi sana yamefanyika, mengi yameelezwa, mojawapo ikiwa ni suala la Simba kuweza kuitangaza Tanzania, “Visit Tanzania.” Swali ambalo tunapaswa tujiulize, tufanye evalution kwamba Visit Tanzania imetusaidia nini katika suala zima la utalii? Kwa sababu tunaweza tukafanya advertisement nyingi sana, lakini at the end of the day, lazima tujue hizi advertisement ambazo tunazifanya tunazi-evaluate vipi? Tunazi-quantify vipi in terms of hawa watalii na fedha ambazo zinakuja kutumiwa na watalii? Hili ni suala la msingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nitegemee tu kwamba wewe pamoja na wataalam wako mkiwa mnakaa katika mikakati ambayo inakuwa inaendelea katika kuweza kuboresha masuala mazima ya internal tourism, hizi activities tunazozifanya lazima tufanya self-evaluation, zimesaidia vipi? Hili ni suala la msingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni suala zima la hunting tourism. Naomba niguse pale ambapo Mheshimiwa Nape alipokuwa amegusa asubuhi kwamba kuanzia mwaka 2013 na kuendelea mapato yale yaliyokuwa yanapatikana katika suala zima la hunting tourism yamekuwa yakipungua kidogo kidogo. Tumeambiwa mwaka 2013 tulikuwa tunapata mpaka dola milioni 27, lakini todate tunazungumzia kwenye Dola milioni nane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu, mfumo wa kugawa vitalu hauna shida, uko vizuri kwangu mimi, kwa sababu Serikali walikuwa wamechukua maamuzi hayo kwa kwa kuzingatia kwamba tunakwenda kutokomeza mambo yale ya ubadhilifu yaliyokuwa yanafanyika kwenye vitalu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha msingi zaidi cha kufanya nafikiri kuna kitu kimoja hapa lazima tukiangalie. Kwenye economics kuna kitu kinaitwa law of demand na law of supply. Kwenye law of demand tunaamini kwamba the higher the demand, the higher the price; na kwenye suala zima la law of supply tunaamini kwamba the highest supply, basi the low the price if other factors zinakuwa zina-remain constant. Tuelewe tu, hapo hapo kwenye economics, kuna kitu kinaitwa product substitutes, yaani kama kuna product fulani ambayo inaendana na product nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wataalam wetu kitu ambacho wamejisahau, tulitoka kwenye Dola 7,000 katika kuuza vitalu hivi, tukaenda kwenye Dola 30,000, sasa hivi tuko kwenye Dola 80,000. Tumeambiwa kwamba tuna vitalu karibia 40 vyote hivyo viko katika mazingira kwamba havina watu na vingine 14 viko katika hali mbaya sana. Tafsiri yake ni kwamba, twende kwenye basics za economics kwamba pale ambapo pana demand ya hali ya juu sana. Ni mategemeo yetu kwamba sisi tunaweza kukaviuza vitalu hivi kwa bei ya juu, hakuna shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke tu kwamba, sisi tuna competitors wetu vile vile. Ni vyema zaidi katika sekta hii ya hunting tourism lazima tuweze kufanya kazi ya ziada ili sasa kuweza kufahamu competitors wetu wana-add value vitu gani vinavyoweza kuwavutia wale watu wanaokwenda kuwinda kule? Maana yake ni nini? Ni kwamba vitalu tunavyo, nasi Tanzania we are biological reach, lakini very unfortunately tunashindwa kuutumia huu utajiri tuliokuwanao vile ipasavyo. Namwomba tu Mheshimiwa Waziri akae na wataalam wetu, ili sasa tuweze kujua ni kitu gani ambacho wenzetu wanakifanya ili nasi vile vile tuweze kufanya tuweze kuwavutia watu waje kuwekeza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hilo, nilikuwa naomba vilevile niguse katika sehemu nzima ya mambo ya mapato. Mheshimiwa Waziri ametuambia kwamba kuna fedha tunakusudia kuzikusanya katika mwaka wa fedha huu karibia shilingi bilioni 478.01 katika sekta yetu kule TAWA, Ngorongoro, hizi fedha zote zinakwenda moja kwa moja kule TRA. Ni vyema sasa wangeweza kutuambia mikakati gani ambayo tunakwenda kuifanya ili kuweza kufikia lengo hili? Vinginevyo tunaweza tukawa tunazizungumza hizi namba lakini tafsiri pana ni kwamba, tunaweza tukawa tunashindwa kufikia malengo haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, nilikuwa naomba sasa niende jimboni kwangu. Mheshimiwa Waziri naomba tusikilizane vizuri sana hapa. Wewe ni rafiki yangu, mtani wangu, maana unatokea kule kusini kusini; na mkae mkijua kwamba sisi ndio tuna barabara pale. Mkiwa mnaleta taabu Mheshimiwa Waziri unaweza ukashindwa kuja Dodoma huku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo moja la msingi sana kule. Serikali mwaka 2017/2018 ilifanya zuio kwa makusudi mazima, tena mazuri zaidi ya kuweza kulinda mazingira jinsi ya uvunaji wa mikoko. Mwaka 2019 Serikali ilituma wataalam ili sasa kwenda kufanya tathmini, mikoko ile itaenda kuvunwa vipi na kuweza kulinda mazingira? Mwaka 2020 wataalam wale walikuja katika maeneo husika, maeneo mengi sana ambayo yanazungukwa na maziwa pamoja na mito ili kuja kuwaeleza kwamba tathmini imeshakamilika na kwa namna moja ama nyingine Serikali itatoa tamko ni jinsi gani sasa mikoko ile itawezwa kuvunwa ili tusiweze kuharibu mazingira?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Waziri, kule kwangu mimi kuna maeneo ya delta, nina kata kama tano; kuna Kata ya Kiongoroni, Kata ya Maparoni, Kata ya Mbochi, Nsala, Salale; vile ni visiwa. Hii mikoko ni mali tuliyopewa na Mungu, tunajua lazima tulinde mazingira. Sasa ni jambo la msingi tuweze kujua ni jinsi gani wananchi wale wanakwenda kuokoka katika kuivuna mikoko hii. Kwa hiyo, ni mategemeo yangu Mheshimiwa Waziri, utakapokuja kufanya wind-up hapa, uje kutupa tamko la Serikali, nini tunachoenda kukufanya ili wananchi wale waruhusiwe kuivua mikoko ile? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili na la msingi ni suala zima la wajasiriamali wangu pale Kibiti. Kuna wajasiriamali hawa ambao wanafanya shughuli za randa hizi. Inasikitisha sana, wananchi wale tunawaita wajasiriamali, wanatengeneza vitanda na vitu vingine, lakini cha kusikitisha tu ni kwamba tozo ambazo wanatozwa ni nyingi sana. Kuna urasimu wa hali ya juu kiasi kwamba watu hawa wanashindwa hata kuweza kufanya shughuli hizo.

Kwa hiyo, naomba wa Kihesa wanaenda kulipa TFS, ambayo inawachaji shilingi 55,000/=. Kuna tozo wanaenda kulipa TRA, kuna tozo wanaenda kulipa Halmashauri, kuna tozo wanakwenda kulipa katika vijiji husika. Sasa hawa wajasiriamali tunawasaidia vipi? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Haya, ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Naunga mkono hoja. (Makofi)