Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Devotha Methew Minja

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. DEVOTHA M. MINJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie kwa njia ya maandishi juu ya hoja ya Viwanda na Biashara kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufa kwa viwanda Morogoro; Mwalimu Nyerere alipendekeza Mkoa wa Morogoro kuwa Mkoa wa viwanda tangu miaka mingi iliyopita kwa lengo la kusaidia Jiji la Dar es Salaam kutokana na miundombinu iliyopo ikiwemo umeme, barabara, reli, maji na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda hivi vilitegemewa na wananchi wa Morogoro, vilisaidia kupunguza tatizo la ajira, ambapo hata wananchi wale waliweza kuendesha maisha na kupeleka watoto shule, hali hii ilisababisha population na kupelekea kuwepo kwa vyuo vingi vikuu ambavyo vilitengeneza wanafunzi waliofanya kazi katika viwanda, lakini viwanda hivi leo hii vimekufa baada ya Serikali kuvibinafsisha!
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali kubinafsisha lilikuwa ni kuongeza uzalishaji na kupanua viwanda, lakini hivi sasa viwanda vimebaki kuwa magodauni, vingine vinafuga mbuzi na vingine vimebaki tupu baada ya wawekezaji wasio na nia njema kuuza vyuma vilivyopo ndani ikiwemo kiwanda cha Kanivas cha maturubai na kiwanda cha Asante Moproko kilichokuwa kinatengeneza mafuta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikijitapa kuwa inataka kuingia katika uchumi wa viwanda, lakini tutafikaje bila ku-review upya matatizo yaliyosababisha kufa kwa viwanda hivyo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wito wangu kwa Serikali, ipitie upya mikataba ya ubinafsishaji, ambapo baadhi ya wawekezaji wasio na nia njema walichukua viwanda kwa lengo la kujinufaisha ambapo wengine walichukua viwanda kwa lengo la kupata mikopo katika mabenki, ambapo wengine walichukuwa mikopo na kufungua biashara zingine zikiwemo biashara za mabasi na malori badala ya kuwekeza kwenye viwanda na matokeo yake viwanda vimekufa!
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyakazi zaidi ya 4000; mpaka sasa wengine wameshakufa, walikuwa wanadai fidia baada ya ubinafisishaji kwa lengo la kuwaendesha na kulipa vinua mgongo, lakini wafanya biashara hawa hawakuwalipa Wananchi hao hadi leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kuitaka Serikali kuchukua hatua za haraka ama kupitia upya mikataba, ukaguzi wa viwanda vya Komoa, Kanvas, Asante Moproco, Ceramic Unats, Tanaries, Tanzania Shoe, ambavyo vyote vimekufa na vimegeuzwa kuwa mazalia ya popo na kufugia mbuzi!
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kufungia viwanda vya Plastics nchini; hivi sasa kuna zaidi ya viwanda 20 vya kutengeneza plastics vinavyotengeneza mifuko, ambavyo vingi vimefungiwa kwa sababu vinasababisha uchafuzi wa mazingira, kiwanda kimoja cha mfuko wa plastic kinaajiri watu 200 kwa viwanda, hivi 20 tunawanyima ajira watu 4000! Kwa nini Serikali isije na plan B ya kuwataka wawekezaji hawa wa viwanda vya biashara kama vya mifuko kuagiza material ya kuozesha mifuko badala ya kuja na hoja ya kuongeza micro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imevifungia viwanda hivi kwa kuvitaka vitengeneze mifuko minene yenye unene wa macro 50 kutoka kwenye micro 30 ya hivi sasa. Wawekezaji hao wana mikopo na walifuata utaratibu wote wa kupata vibali na kuwekeza, lakini badala ya kuja na mkakati rahisi kusaidia nchi iendelee kuwa na viwanda sasa inaua viwanda!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi kama Uingereza, Kenya, Ethiopia, viwanda vya Plastics ndiyo vinasaidia kuongeza ajira na kuinua uchumi. Katika hili wamefanikiwa kutokana na ubunifu ambapo ungesaidia kuwezesha mifuko hii badala ya hapa nchini kuja na mkakati wa kufungia viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali ije na plan B ya kusaidia viwanda hivi kwa kuruhusu ku-import material kuwezesha mifuko na hii itasaidia hata bidhaa zingine zinazotumia mifuko kama chumvi, viroba, sanzu na kadhalika. Lakini tukija na mpango wa kuwa na mifuko macro 50 mifuko hii itakuwa ghali na watu wa kawaida hawataweza ku-afford.