Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bunda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nakupongeza kwa kukalia hicho kiti. Nilikuwa natafutatafuta hapa historia kwamba kuna mtu aliwahi kuwa mdogo zaidi wa kukalia hapo, nikajua ni wewe tu peke yako ambaye ni mdogo zaidi uliyewahi kukalia kiti hicho hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo ambayo wanasema nafasi inapata mtu au mtu kupata nafasi. Nadhani Wabunge wamejua kwamba, sasa hiyo nafasi imepata mtu. Kwa hiyo, ataishughulikia vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Maliasili na Utalii, sasa mimi huwa naangalia, yaani ukimwangalia Waziri wake aah, super, yuko vizuri sana yaani jamani. Ukimwangalia Naibu wake yuko vizuri sana, Katibu wake ndiyo usiseme, Mheshimiwa Kijazi. Wakae sasa ili tusiwabughudhi; maana inaonekana kama miaka yote tunawabughudhi. Ili tusiwabughudhi, waamue Wizara ya Ardhi na Wizara ya Maliasili, wako pamoja kwenye Kamati moja, wajiulize ni wapi ambapo sasa kuna shida ya Watanzania kwenye ardhi hii, waende watatue hayo matatizo ya Watanzania. Kwa sababu hatuwezi kuwa humu miaka nenda rudi, mwishoni Wabunge tutachokwa sasa. Nenda rudi, tunapigia akili kwamba Watanzania wananyanyaswa kwenye maeneo mengi. Watafute maeneo ambayo yapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Ardhi Na. 4 inaruhusu, kwa sababu ardhi yote ni ya Rais. Kwa hiyo, waangalie. Mimi huwa najiuliza, hivi ni kwa sababu hatukuandika land reserve, tumeandika game reserve? Ukisema land reserve, ni ardhi yote ya Watanzania; general land, the village land, yote hiyo na ya game reserve ni ya Rais. Kwa hiyo, tuangalie, ni wapi tunakosea jamani? Wapi tunakosea kila siku Wabunge tuko humu tunapiga kelele? Tuamue tulete migogoro yote. Marehemu Rais Magufuli aliunde Kamati, imeenda huko imefanya kazi, walete hiyo ripoti basi tuone wamebakiza wapi ili tumalize? Kwa nini tunapiga kelele kila siku humu ndani haiishi? Hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naipongeza Serikali kwa maana ya kuweka hali nzuri ya mambo ya mapori yalivyokaa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ila naomba Mheshimiwa Rais aingilie kati migogoro yote ambayo wananchi wanakerwa nayo na pia tumwombe Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu na wote, wale ng’ombe wote waliochukuliwa kwenda porini wakashinda kesi, warudishwe.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Getere ahasante.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Jamani warudishwe ng’ombe wa wananchi.