Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Jonas Van Zeeland

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na afya, hatimaye na mimi nimeweza kusimama mahali hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kutoa mchango wangu katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii kama kuna watu wanaichonganisha Serikali na wananchi wake basi ni watu wa TFS. Mheshimiwa Waziri kama kuna watu ambao wanaichonganisha Serikali na wananchi ni watu wa TFS. Sisi Mvomero tuna Hifadhi ya Wame Mbiki. Hifadhi hii ilianzishwa miaka ya nyuma, ni hifadhi ambayo imepakana na vijiji vingi; ni hifadhi ambayo imepakana na Kata zaidi ya nne lakini shida iliyopo katika hii hifadhi ni suala la mipaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilishamtafuta Mheshimiwa Waziri nikamweleza habari ya mipaka. Kuna wananchi wanalima, wengine kwa kujua mipaka na wengine kwa kutokujua, lakini mbaya zaidi hawa wenzetu wa TFS wanapowakamata hawa wananchi ambao wapo ndani ya yale maeneo, wanawapiga, wanawatesa na wanawapiga mpaka risasi. Tunaye mwananchi mmoja amepigwa risasi hivi karibuni anaitwa Juma Shabani Bakari; amepigwa risasi zaidi ya mbili kisa amekutwa ndani ya hifadhi. Sasa hata kama ameingia ndani ya hifadhi, sheria zipo, kwa nini hapelekwi kwenye vyombo vya sheria, wanaamua kuchukua sheria mkononi na kumpiga risasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaye mwananchi mwingine anaitwa Said Mwanamvua; huyu alipigwa fimbo, alinyanyaswa na walitaka kumchoma moto. Walikusanya miti wakamuingiza katikati wakataka kuwasha moto ile miti ili aweze kuungua. Sasa hao wananchi wapo Tanzania, kwenye nchi ambayo ipo huru, lakini leo wanataka kuuwawa katika nchi ambayo ni huru. Naomba commitment ya Mheshimiwa Waziri katika jambo hili kwenye suala la mipaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbaya zaidi nilishawasiliana na Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya nikamweleza tatizo ambalo lipo pale. Wananchi ambao wanalima yale maeneo wakati wa kulima wanaruhusiwa, wanalima vizuri, lakini wakati wa kuvuna, sasa hivi wanataka kuvunwa wanakatazwa. Wakikamatwa ndani wananyanyaswa kama nilivyosema, lakini wakati wa kulima wanaruhusiwa walime. Nimezungumza na Mkuu wa Wilaya akaniambia mimi hayanihusu hayo mambo, waache wananchi huko wafuate taratibu ambazo zimepangwa na TFS. TFS kwenye wilaya ipo chini ya Mkuu wa Wilaya, nilishamweleza Mheshimiwa Waziri habari ya TFS na hawa watu wa Wame Mbiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana leo Mheshimiwa Waziri wakati ana-wind up atupe majibu, atueleze lini watakuja kurekebisha mipaka katika vijiji ambavyo vinapakana na Wame Mbiki. Yale maeneo ambayo tayari wananchi wanayatumia kama itaonekana wako ndani ya hifadhi, basi wanaweza wakayapima wakayatoa. Wame Mbiki hii zamani ilikuwa ina jumuiya ambayo inajiendesha yenyewe, ile jumuiya imekufa, sasa hivi wanasimamia watu wa TAWA na watu wa TFS. Hawa wananchi zamani ndio walitoa hayo maeneo yao, sasa hivi kwa sababu wananchi wameongezeka wanayahitaji haya maeneo. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri busara imwongoze aweze kutupatia haya maeneo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la tembo. Wilaya ya Mvomero sisi tumepakana na Hifadhi ya Mikumi, tembo sasa hivi kwenye Tarafa ya Mlali wapo kama mbuzi, yaani wametoka kule kwenye hifadhi nafikiri kule wameisha wote, wapo kwa wananchi, lakini tukiwauliza wanakwambia huu ni ushoroba/njia ya tembo; sasa njia ya tembo, tembo ndo anakaa hapohapo mpaka wanazaliana, kama njia si apite aende kwenye safari zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, tembo wamekaa eneo moja, wanazaliana na sasa hivi wanaingia kwenye nyumba za wananchi. Wakisikia harufu ya mahindi ndani wanafumua paa wanaingiza ule mkonga wao wanakula mahindi ndani. Wananchi hawalali hata ndani kwenye nyumba zao, ni mateso makubwa wanayapata, lakini tukiambiwa ushorobo, kila sehemu tembo anapoonekana ushorobo sasa ushorobo utakuwa nchi nzima. Hapa siku moja tuliambiwa, Chuo Kikuu hapa (UDOM) kwamba tembo wameonekana, tukaambiwa nako ushorobo, sasa mwisho watakuja kuingia hata kwenye Bunge hapa utaambiwa nako ushorobo, barabara hii ya tembo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri lazima wawe na mikakati madhubuti ya kuwarudisha tembo wanapotakiwa kuishi. Kule wekeni hata mipaka itaonyesha wazi kabisa kwamba haya ni maeneo tembo wanapita wananchi msilime lakini ikiwezekana kule kwenye hifadhi wekeni fensi ya kutosha tembo asivuke. Kwa sababu sisi ni maeneo ambayo yanatuathiri sana mfano Kata za Doma, Msongozi, Mangai, Melela na Lubungo wananchi hawalimi.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi ambao wanadai fidia pamoja na fidia yenyewe ni ndogo, wapo 2,050 hawajalipwa fidia. Pia wapo wananchi ambao wameshakufa na tembo wamefika mpaka sasa hivi 26 hawajalipwa fidia na fidia yenyewe ni ndogo, hivi kweli mtu anauawa na tembo analipwa shilingi milioni moja, shamba linavamiwa na tembo analipwa shilingi laki moja. Naomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie katika hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nimalizie kwenye suala la mkaa. TFS watusaidie kwenye suala la mikaa, hivi gunia moja shilingi 12,000 unatakiwa kulipa, wananchi wetu wa vijijini hawana nishati mbadala zaidi ya mkaa na kuni, lakini leo wakikamatwa anatakiwa kulipa 12,000 TFS na 2,000 halmashauri, hivi kule vijijini watatumia nini?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana kengele imegonga.

MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja. (Makofi)