Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Maliasili ya Utalii. Kwanza nipende kuwapongeza sana Waziri pamoja na Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii kwa jinsi ambavyo wanafanya kazi zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri na Naibu Waziri wamekuwa ni watu wasikivu sana, unapowafuata kwa kitu chochote kinachohusu Wizara yao kwa kweli wanachukua muda kusikiliza. Katika hotuba ya bajeti ya Maliasili na Utalii wametoa vipaumbele; moja ya kipaumbele ni kuratibu mapitio ya sheria, sera, kanuni na kuandaa miongozo mbalimbali inayosimamia Sekta hii ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa kuna migogoro mingi baina ya hifadhi na wafugaji na kupelekea sehemu zingine wafugaji wanauawa au wananchi wanauawa. Tumesikia katika Wilaya za Kiteto, Longido, Ngorongoro na hata Chemba matukio kama haya yanatokea. Ningeomba Wizara kupitia Wizara ambayo inasimamia wafugaji na inasimamia hifadhi ambayo ni Wizara ya Ardhi. Kwa mtizamo wangu naona kwamba Wizara ya Ardhi ina jukumu kubwa sana la kuhakikisha kwamba maliasili inafuata sheria pamoja na wafugaji na wananchi wengine wanafuata sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, ardhi ipo toka kuumbwa kwa dunia, haiongezeki na haitaongezeka lakini sisi wanadamu tunazaliana kila siku iitwayo leo. Kwa maana hiyo mahitaji ya ardhi yanaendelea kukua kwa kasi kubwa sana kutokana na population yetu Watanzania, lakini unakuta kwamba hifadhi alama ambazo zilizowekwa au mipaka ambayo iliwekwa enzi zile za mwaka 1940 na ngapi kule bado zinatumika mpaka leo wakati kuna ongezeko kubwa sana la wanadamu. Kwa maana hiyo basi, Wizara ipitie katika vipaumbele vyake ipitie kuangalia sheria, kurekebisha mipaka, kuwapa nafasi wananchi waweze kutumia hiyo ardhi, kwa sababu idadi ya wananchi inaongezeka kila leo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa kuna migongano ya matumizi ya ardhi kwa jamii ya wafugaji kati ya wahifadhi, wawekezaji lakini pamoja na wananchi kwa ujumla. Tunaomba Wizara hii ijaribu kushughulikia kuangalia kwamba inatatua vipi matatizo ambayo yanawapata wafugaji. Solution siyo kuwaua tumesikia kuna hili Shirika la TAWA Pamoja na TFS wanafanya kazi zao vizuri, lakini je ni lazima kutumia nguvu, ni lazima kutumia risasi, ni lazima kutumia bunduki.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua sheria zipo, basi tunaomba wafuate sheria. Kama kuna wafugaji, kama kuna wananchi, kama kuna taasisi ambayo imeingia kwenye hifadhi tunaomba sheria zisichukue mkondo wake. Kuna chombo ambacho kinatoa maamuzi kuna mahakama, wasichukue sheria mkononi ya kuwaua. Kuna ambao wanapatikana, kuna ambao wanajulikana wameuawa, kuna ambao hawajulikani, unashangaa watu wamepotea. Naomba sana Wizara ya Maliasili na Utalii ikishirikiana na Wizara ya Ardhi, ikishirikiana na TAMISEMI, ikishirikiana na Wizara ya Mifugo wahakikishe kwamba wanafuata sheria, kanuni na taratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja.