Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii muhimu, Wizara ya Maliasili na Utalii. Jambo la Kwanza nipende kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi ambayo wanaifanya, lakini pia kwa wasilisho zuri la bajeti yao hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo mawili ya kuchangia; unapotaja utalii kwa kipindi cha sasa huwezi kuiacha Makete nyuma kwa sababu Makete ina hifadhi ya Kitulo, hifadhi ya kipekee hifadhi ambayo ukiambiwa utafute Bara zima la Afrika hata duniani ikiwezekana utaikuta Makete tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu umejikita kwenye mambo mawili; cha kwanza ni kuitangaza Hifadhi ya Kitulo. Kuna Wabunge wamezungumza hapa jana kwamba tumejikita kwenye kuzungumzia vyanzo vilevile vya utalii kwa maana Serengeti, Ngorongoro tunavitaja hivyo, lakini Hifadhi ya Kitulo ambayo kwa muda mrefu na ina upekee tumekuwa tukietelekeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri wauiangalie sana Hifadhi ya Kitulo. Kwanza afahamu jambo moja kwamba kwa upande wa Nyanda za Juu Kusini kwa maana za highlands, Hifadhi ya Kitulo ndio ina mlima kwa maana iko kwenye ukanda wa juu zaidi kuliko hifadhi yoyote, kwa maana kwamba ina mlima ambao unaitwa Mtorwi Mountain ambao una urefu wa mita 2,961 kutoka usawa wa bahari, hamna sehemu nyingine ukiambiwa utafute nyanda za juu kusini iko ndani ya Kitulo, ndani ya Wilaya ya Makete.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana watu wasikimbilie tu kupanda mlima Kilimanjaro, Makete pia tuna hii, waanze kuitangaza, lakini ukiwa kwenye mlima huu unaiona moja kwa moja Malawi, Kyela na Matema. Ni fursa sasa kwa Wizara ya Maliasili kuruhusu hata uwekezaji binafsi kama Serikali imeshindwa tuite uwekezaji binafsi, waweke hata aerial cables, kwa maana zile aerial car cables za kutoka kwenye milima ya Livingstone, ukipita kule Unyangala, ukipita kule Utengule ukipita Kitulo yenyewe, ukielekea kule Busokelo inatakiwa watu wasafiri at least kwa aerial car cables kwenda kufika Matema, Kyela na utalii wetu ukakua, kuliko kuendelea kujikita kubaki kule Serengeti na Ngorongoro na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namsihi Mheshimiwa Waziri, sisi Makete hizi fursa zipo wazitumie wananchi. Sasa kwa nini tunapiga kelele? Ile hifadhi…

T A A R I F A

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kiruswa.

MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba niliwahi kwenda Taifa la Jamaica nikakuta mtindo wa utalii unaotumia hiyo kamba inaitwa aerial cable inaitwa zipline, unatoka mlima mmoja unakwenda mwingine kwa kuambaa angani na watalii waliokuwa wanakuja ku-experience jinsi ya kusafiri kwenye zipline walikuwa wanazidi milioni 12 kwa mwaka kwa nchi ile na uliwaingizia mapato makubwa sana.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Sanga unapokea taarifa hiyo?

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea kwa mikono miwili, lakini naomba ulinde dakika yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kitulo tunaiomba sana waiangalie kwa jicho la pekee, zile aerial cables zinaruhusu kabisa mazingira ya kule na ukipita kule utadhani huko Alaska, kumbe upo Makete jinsi ambako kumepangika. Hiyo ni fursa ya namna nyingine

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie jambo lingine kwa haraka kwa sababu dakika ni chache, ni suala la migogoro ndani ya hifadhi ya TANAPA kwa maana ile ya Kitulo na hii Game Reserve ya Mpanga Kipengele.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kitulo imezungukwa na maeneo mengi ambayo wananchi wanaishi. Kuna Vijiji vya Makwaranga, Misiwa, Nkondo, Lugoda, Kinyika na vingi ambavyo vinazunguka hifadhi hii. Hadi leo hadi GN inatoka tuliyoitunza ile hifadhi ni Wanamakete, lakini kilichojitokeza sasa hivi ni changamoto ya mipaka ile mikubwa kwa kiwango ambacho hakijawahi kutokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyozungumza muda huu kwenye Kijiji cha Lugoba kuna mwananchi wangu amefyekewa mazao na watu wa TANAPA, amefungwa ndani, wanasema ameingia kwenye eneo la hifadhi, lakini Mheshimiwa Waziri ukisoma Sheria ya Uhifadhi inakwambia kabisa; ibara ya 16 kifungu cha 5 inasema hivi: “For the purpose of the subsection (4), sitaisoma, the Minister shall ensure that no land falling under the village land is included in the game controlled areas.”

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo lakini Wizara wamechukua kwenye makaburi ya wananchi wetu. Hii hapa Mheshimiwa Waziri ataisoma. Ukienda kule Makete sehemu kwa mfano ya Mpanga Kipengere eneo la makaburi ya wananchi ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakiishi, limechukuliwa limeingiwa ndani ya hifadhi. Juzi wananchi wawili wamefariki, wanaenda kuzika wamefukuzwa na watu wa game reserve. Pia angalia ukienda hapa maeneo ya Kinyika wananchi wangu shughuli zao kubwa ni za kulima viazi wanafukuzwa na watu wa TANAPA.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, watu wa TANAPA si wastaarabu, kwamba at least wangekuwa na mahusiano mazuri na wananchi; wanafyeka mazao, wanazuiwa watu kwenda kuzika kwenye maeneo ambayo walikuwepo, lakini nikwambie kitu kingine hadi shule wamechukua, wanasema inasoma ndani ya hifadhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, you can be a champion to this country, juzi tumefungua kitabu cha sensa, provision inaonyesha Watanzania tunaenda kuwa milioni 64. Mheshimiwa Waziri anaandaa mazingira yapi ya kukaa na watu milioni 100 Tanzania kwenye hifadhi ambazo wanaendelea kuwa nazo.

Je, tukiendelea na hizi sheria ambazo zinadhibiti wananchi kwa kiwango hiki, Watanzania wakiwa milioni 100 watawapeleka wapi. You need to be a champion to this country kuandaa sheria ambazo zitalinda nchi hii ikiwa na watu millioni 100 au 200.

Mheshismiwa Naibu Spika, kama tumeshindwa kujenga barabara zinazoweza kuishi miaka 20, tutashindwaje kuunda sheria inaweza ikawa na Watanzania milioni 200 mwakani; you can be a champion kwa kuunda sheria ambayo inatuhifadhi Watanzania zaidi ya milioni 200 kama ambayo milioni 64 wanakuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru lakini namwomba Mheshimiwa Waziri…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. FESTO R. SANGA: Dkt. Ndumbaro tunaamini katika hili ataandaa sheria ambayo itawa-acommodate watanzania milioni 200.