Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Madaba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na Waheshimiwa Wabunge kukushukuru kwa kupata fursa ya kuzungumza, lakini kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wa Wizara hii kwa kazi kubwa na kwa ubunifu ambao wanao ili kuendeleza sekta ya uhifadhi na utalii nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee namshukuru Mheshimiwa Waziri baada ya kumweleza changamoto za wananchi wangu wa Jimbo la Madaba alikwenda mwenyewe, kwenda kuwasilikiza na kuanza mchakato wa kumaliza changamoto zao. Namshukuru sana Waziri na naomba aendelee na moyo huu huu. Nimemwona anakwenda Tunduru, nimeona anakwenda sehemu mbalimbali ndani ya nchi yetu kwenda kuwasikiliza Watanzania na kuona namna gani tunamaliza changamoto zao na naamini approach aliyonayo itatufikisha salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii ina changamoto kubwa sana, tumeipa mzigo mkubwa sana. Nchi hii inawategemea wakulima, inawategemea wafugaji, inawategemea watalii na inawategemea wahifadhi. Sekta hizi zote zinategemeana na Watanzania wanaongezeka kwa idadi. Changamoto ya Mheshimiwa Waziri ni namna gani tunaweza ku-accommodate tuka-strike balance miongoni mwa wafugaji, wakulima na hifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu Mheshimiwa Waziri azingatie ushauri uliotolewa na baadhi ya Wabunge hapa wa kurejea upya michoro ya nchi hii ili kuweka bayana maeneo ya mifugo, maeneo ya kilimo na maeneo ya hifadhi ili kuhakikisha kwamba kila kitu kinapewa kipaumbele na Watanzania wanaishi kwa utulivu na amani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri pia aendelee kuangalia mgogoro wa wananchi wa Madaba kwa eneo la Slow ambalo tayari ameanza kulifanyia kazi. Wananchi hawa pamoja na kazi nzuri aliyoifanya Waziri, bado hawaamini kwamba lile eneo ni mali ya maliasili, wanaamini kwamba wameporwa. Naomba jukumu la maliasili siyo kushambulia wale wananchi, jukumu la maliasili ni kukaa nao chini na kuelekezana kwenye michoro, ni wapi inaonyesha kwamba ni mali ya maliasili na wapi ni mali ya vijiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya maeneo kama alivyosema Mheshimiwa Ng’wasi, yanatumia michoro ya zamani sana na tayari haya maeneo yameshatangazwa kuwa vijiji, Kijiji cha Nderenyuma kimetangazwa kwenye ziara ya mwisho ya Mheshimiwa Rais Marehemu Dkt. John Pombe Magufuli ameitanganza Nderenyuma kuwa Kijiji. Mbangamawe ni Kijiji cha muda mrefu, maeneo haya yote sasa maliasili wanasema kwamba ni kivuko cha wanyama kwa hiyo wananchi wasilime mazao ya chakula kama mahindi. Ni ushauri mzuri, lakini ukiwa participatory utatusaidia kumaliza mgogoro huu. (Makofi)
T A A R I F A
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Neema Mgaya.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa taarifa kaka yangu Mheshimiwa Joseph Mhagama kwamba tatizo hili la migogoro hii kati ya mipaka ya mapori ya akiba na hifadhi na vijiji vingi ndani ya Tanzania imekuwa tatizo kubwa sana na Wabunge wengi wanalalamikia tatizo hili. Ifikie mahali sasa Mheshimiwa Waziri waweze kutatua migogoro hii, wakae waende kwa pamoja na Waziri wa Ardhi ili mkienda kumaliza tatizo mnamaliza moja kwa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano kule Wanging’ombe, alikuja Naibu Waziri wa Ardhi mwaka 2018, lakini mpaka leo lile tatizo halijamalizika, hebu wakae kwa pamoja na Wizara ya Ardhi muweze kumaliza matatizo haya…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Neema ahsante kwa mchango wako. (Kicheko)
Mheshimiwa Joseph Mhagama.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, napokea kwanza taarifa ya dada yangu Neema Mgaya kwa sababu ya muda…
NAIBU SPIKA: Naambiwa na kengele ilikuwa imeshagonga hapa mbele.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Waziri basi tuendelee kushirikiana na wananchi wa Madaba kumaliza changamoto zao kwa njia ya kushauriana. Ahsante sana. (Makofi)