Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Saashisha Elinikyo Mafuwe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Hai

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Wizara hii. Kabla sijaendelea, naomba nitoe pole nyingi sana kwa wananchi wa Jimbo la Hai, kwa kuondokewa na mama yetu mpendwa ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Kilimanjaro, lakini ni mke wa Waziri Mstaafu baba yetu Msilo Swai.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pole hizo, niungane na wenzangu kupongeza sana uongozi wa Wizara hii. Bahati nzuri nilikwishasema mimi sio mwepesi sana wa kupongeza, ila napongeza kwa sababu. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, kwa namna ambavyo anasimamia Wizara hii na taasisi zake. Pia nimpongeze kwa sababu, yeye anafikika na anasikia akiambiwa, ni Mawaziri wenye sifa za pekee pamoja na huyu. Hata hivyo, nimpongeze Naibu Waziri kwa namna ambavyo na yeye pia ni mtu anayefikika, mama mwema kabisa huyu, nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze pia watendaji wa taasisi wakiongozwa na Katibu Mkuu. Isipokuwa wale wa TAWA wao sitawapongeza kwa sababu, nina jambo nao. Vile vile nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri tulienda naye kwenye ziara kwenye Jimbo la Hai na tulitembelea eneo lile la Makoa kwenye Chama cha Ushirika. Nimshukuru sana kwa kusimamisha mkataba ule uliokuwa mbovu na leo sitaki kuzungumza jambo lile kwa sababu najua Waziri anaendelea na uchunguzi. Nimpongeze kwa hatua za awali kusimamisha mkataba ule ambao ulikuwa hauna maslahi kwa wananchi wa Jimbo la Hai. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe pamoja na pongezi hizo sasa nishauri. Tumekuwa tukipokea mapato makubwa sana kwenye Serikali kuu kwenye vyanzo vinavyotokana na maeneo ya utalii. Hata hivyo, imekuwa bahati mbaya, wananchi wanaozunguka maeneo haya, hawanufaiki moja kwa moja pamoja na kwamba, tunapokea fedha kutoka Serikali Kuu. Hili linaongeza kutokuwa na upendo na maeneo yale. Ili wananchi hao wanaozunguka maeneo haya wawe na upendo na watunze vyanzo vyetu, lazima tuone namna ya kuwa-motivate na kuwafanya wawe na upendo na vivutio hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, tuna Mlima Kilimanjaro pale, utashangaa sana wale wanaoenda kusaidia watalii wanaowapandisha mlima wanatoka nje ya maeneo yale. Lakini vile Vijiji vya Foo na vingine vinavyozunguka Mlima Kilimanjaro, wale vijana hawapati kazi hizi. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri, mimi niko kwenye mchakato naandaa database ya vijana wanaozunguka vijiji vya Mlima Kilimanjaro, ambao wana sifa za kupandisha watalii kwenye Mlima huu waweze kupata ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nitakabidhi database hiyo ya vijana wa Hai, wako tayari, wana afya njema na wana sifa za kupanda Mlima Kilimanjaro. Wizara iwatumie na ipeleke maelekezo maalum kwa makampuni yanayopanda Mlima Kilimanjaro, ili waweze kuwatumia vijana hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kushauri, tuna mageti kadhaa yanapanda Mlima Kilimanjaro, lakini ukiyaangalia najua tumepita kwenye kipindi cha mpito ambacho ugonjwa ya Corona umesababisha idadi ya watalii ishuke. Hata hivyo, najua mungu ni mwema atatusaidia na watalii wanaongezeka. Kwa sababu hiyo naomba sasa tuwe na geti lingine jipya ambalo litaanzia pale barabara ya kutoka Kwa Sadala, litapita pale Ng’uni, litapia Mula kwenye Kata ya Masama Mashariki na Masama Kati. Lengo ni nini, ni kupanua wigo wa utalii kuelekea Mlima Kilimanjaro.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukifungua barabara hii kuna vivutio vingi vya tofauti na barabara ile ya Machame na barabara nyingine zilizoko kwenye wilaya nyingine. Kwa hiyo naomba sana hili pia walitazame. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo napenda kushauri, Waheshimiwa Wabunge wengi hapa wamesema. Utaratibu wa kutoa vibali kusafirisha nje ya nchi lazima tubadilishe mfumo huu, tumeshatoa vibali vingi ndege wetu, wanyama wetu wanapelekwa nje ya nchi. Swali la kujiuliza hapa, hawa wanyama wanakwenda huko nje ya nchi tuna-control vipi kuzaliana kwao. Nataka niwaambie kuna siku hapa tutakosa watalii kwa sababu wanyama hao wakienda kule wanazaliana wanaongezeka na bahati nzuri wenzetu hawa wanateknolojia ya kutushinda sisi. Watakwenda kutunza hawa wanyama watatengeza zoo kubwa kubwa, mwisho wa siku huku nchini tutakosa watalii wakuja kututembelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali ya kawaida, wewe mwenyewe huko hapa ukiona kwamba leo tutakushangaa eti unatoka hapa Tanzania kwenda kushangaa au kutembelea Zoo ya Simba nje ya nchi. Ndivyo itakavyokuwa simba watakuwa wengi, vyura watakuwa wengi, ndege watakuwa wengi na mamba watakuwa wengi kule kwao, huku hawatakuja. Kwa hiyo niombe sasa imetosha, vibali tulivyowapa vimetosha. Hili ni sambamba pia na wanyama wanaokuja kuletwa huku kwetu, iwe ni kuja kutunzwa au vinginevyo. Najua kwenye hili kuna shughuli inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi vibali vya kuruhusu wanyama kutoka nje ya nchi kuja huku kwetu tutazame. Tusije tukaletewa wanyama wa kuja kuharibu wanyama wetu. Tunafahamu hapa Tanzania sisi ndio tunaongoza kwa idadi kubwa ya simba lakini tunaletewa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa niunge mkono hoja. Nashukuru sana sasa, lakini nimalizie kwa kuomba Wizara hii ishirikiane na wizara nyingine…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.