Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Asya Mwadini Mohammed

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. ASYA MWADINI MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuweza kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba hii muhimu ya Wizara ya Maliasili na Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nilieleze Bunge lako Tukufu kwamba Utalii ni Sekta muhimu sana katika uchumi wa Tanzania lakini sekta hii inachangia Pato la Taifa asilimia 17. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Taarifa ya Bodi ya Utalii Tanzania, Tanzania inatembelewa na wageni wapato milioni moja kwa mwaka. Pia, Bodi hiyo ya Utalii imesema kwamba hao wageni milioni moja asilimia 60 ni wageni kutoka nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili linanisikitisha sana ukizingatia kwamba tunawategemea sana wageni kutoka nje ya nchi kuliko sisi ambao tupo ndani ya Taifa letu. Kwa hiyo, faida inayopatikana kwa utalii wa ndani, kuna nchi kwa mfano Brazil wao wana wageni wa ndani ya nchi wanaotembelea katika vivutio vyao ni asilimia 68. Wanategemea asilimia 32 tu, wageni kutoka Mataifa mbalimbali kwa ajili ya kwenda Brazil. Hii inaonesha kwamba unapokuwa umejipanga vizuri katika utalii wa ndani huwezi kutegemea sana ule utalii wa nje. Hilo la kwanza. La pili, pato lile unakuwa na uhakika nalo kwa sababu liko ndani ya nchi. Kwa hiyo, haliwezi kutoka nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, naishauri sana Serikali kwanza kabisa masoko yetu yajikite zaidi kufahamisha Watanzania; kwanza kuhusiana na masuala mazima ya utalii. Pili, hata hawa wanafunzi wetu shuleni tungewatengenezea mtaala au vitabu wakaanza kukua na utamaduni wa kufanya utalii ili iweze kusababisha, maana wanavyokuwa wakubwa wanajua utalii ni suala muhimu na linaweza kuwaletea tija wao wenyewe binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tusiwategemee sana wageni kutoka nje ya nchi kuja kututembelea. Kwa mfano, tumeona mwaka jana 2019/2020 kulivyokuwa na janga kubwa la corona. Kwa hiyo, utalii ulitetereka. Tuna watoto wetu na ndugu zetu walikosa kazi wengi sana wakaendelea kukaa nyumbani. Kama tungekuwa tumeimarisha vizuri Sekta ya Utalii hapa kwetu hivyo wale watu wangeendelea kufanya kazi na masuala mengine yangeendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, naomba niende kwenye kipengele kidogo tu, labda niseme, nimeipitia Sera ya Utalii ya Tanzania inanisikitisha sana. Tunavyosema tunahitaji kupiga hatua kwenye utalii lakini sera yetu bado ni ya mwaka 1999. Kwa hiyo, sera hii haikidhi mahitaji ya utalii wa sasa ambao tuko nao. Kwa hiyo, tunahitaji kwanza tuboreshe sera yetu pamoja na sheria za utalii ili tuweze kuinua utalii wetu na pia waweze kuingiza Pato letu la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye utalii wa ndani tusiwategemee sana japo tunapiga kelele Wabunge humu, ofisi mbalimbali, lakini, kwa nini hata hawa Wabunge ukiwauliza humu ndani wangapi wameweza kutembelea vivutio vyetu itakuwa ni mtihani kwa kweli. Wengine wanaweza kukuambia wamefanikiwa tu kwenda kwenye Kamati ndiyo wameweza kuona tembo na chui. Sasa hili halileti tija, maana tunapokaa tunapiga kelele haileti tija, tuoneshe mfano sisi wenyewe viongozi kwanza. Twende kwenye vivutio, tuwape support Wizara ili na hawa watoto wetu tukiwachukua, watoto wakienda kwenye vivutio, unajua watoto wana story, wakirudi shuleni wanahadithia watoto wenzao. Kwa hiyo, watoto nao wanaenda kuhadithia wazazi. Kwa hiyo, tunakuwa na jopo kubwa la mwingilio wa utalii wa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichangie kwenye masuala mazima ya vivutio vya utalii. Mwanzo nilisema kwamba tunategemea sana wageni wapato milioni moja. Average inaonesha kutokana na vivutio ambavyo tunavyo, hawa wageni bado ni kidogo sana. Ni kidogo kwa sababu vivutio vyetu ni vingi, maana yake vivutio vimewakumbatia wageni kwa hiyo, maana yake vinabaki vinahitaji watu. Kwa hiyo, niishauri Serikali kwenye suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, tuweze kuwapa wawekezaji vivutio vingine ambavyo hatuviwezi. Suala la pili, nakumbuka nilichangia kwenye uvuvi, nilizungumza sana issue ya marine park na nikaomba Wizara ya Uvuvi hili suala la marine conservation wawapelekee Idara ya Utalii, kwa sababu ukipitia takwimu inaonekana wageni kuanzia 45,000 kwenda 70,000, wageni hawa wanavyokuja Tanzania wanafanya diving. Wanaenda kuangalia matumbawe na masuala mengine kwenye bahari.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata ukiangalia kwenye mitandao wageni ambao wanatoka Scandinavia yaani kule kwetu Zanzibar wanavyokuja lazima wakifika waombe kwenda kuangalia coral reef na vitu vingine. Kwa kuwa watu wa utalii ni wataalam zaidi kwenye masuala ya uhifadhi, naishauri Serikali hii Idara ya Marine Park iende moja kwa moja kwenye Wizara ya Utalii na tutaweza kupata pato kubwa zaidi kupitia hii tour moja tu, sikwambii hizo zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende pia zaidi kwenye masuala mazima ya kumshirikisha mwanamke katika utalii wa Tanzania. Tunaona kwamba tunazungumza utalii, nimepitia hotuba na vitu vingine vingi lakini hatuoni mwanamke anatajwa kama ana sehemu kwenye utalii na anafaidika vipi. Namzungumzia zaidi mwanamke ambaye yuko chini grassroot ambaye amepakana na border, hifadhi, yuko kwenye maziwa, yuko chini ya fukwe na yuko katika sehemu pengine nyingi za utalii. Kwa hiyo, mwanamke huyu utaona kwamba yeye yupo amepakana na hifadhi au amepakana na msitu lakini wanaofaidika ni watu labda wanaotokea mkoa mwingine kwa sababu analeta wageni. Yeye yuko pale tu na ule msitu, atafaidika labda kupata hewa safi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niishauri Serikali kwamba; kwanza, tuweze kutengeneza mkakati maalum kuweza kuwasaidia wanawake hawa kupitia miradi mbalimbali midogo midogo ambayo itaweza kuwainua akinamama. Kwa mfano, tuna utalii tunaita culture tourism. Huu utalii, mgeni anaweza akaja mimi mwenyewe binafsi napenda pia kujifunza. Niliwahi kwenda Kagera lakini nilifika nilitumia masaa matatu kuangalia Wanabukoba wanapika chakula chao cha ndizi kwa mtazamo upi. Kwa hiyo, huu ni utalii. Tuwape nafasi akinamama waweze kile kidogo ambacho wako nacho kule majumbani wanafua, wanapika, wanatwanga, lakini mgeni ana-appreciate sana na anajifunza vitu vingi zaidi pale kwa kuona. Kwa hivyo, akinamama watapata pato, lakini vile vile na Serikali nayo itaongeza uchumi. Tusiuache utalii wa utamaduni, ni utalii ambao unaleta pato kubwa ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano ukienda India, Wahindi hawakubali ukifanya utalii usipite katika street zao, usipite kwenye vichochoro vyao ili ujifunze bajia na kachori zinatengenezwa vipi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee zaidi nilizungumza suala zima la masoko na tunahitaji bado masoko yetu yako chini kwenye suala zima la utalii na tunahitaji zaidi Serikali kupitia Idara ya Utalii waweze kutengeneza mechanism ambayo iko strong itakayo-deal na marketing on tourism only ili tuweze kupata pato lakini na kuleta wageni. Narudia tena, tusitegemee zaidi wageni kutoka nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, nishauri labda kwa sababu tunatumia TV, magazeti, vipeperushi lakini kuna mitandao. Sasa hivi, dunia iko kwenye mkono, kuna hawa akina Ayo na wengineo, kwa nini tusingetengeneza vitu kama hivi mtu akiingia tu anapofungua simu yake akiingia kwenye mtandao anakutana na kitu kwamba Visit Tanzania, kuna one, two, three, four ili iweze ku-motivate na nilishazungumza kwamba tutaenda kuwahamasisha watoto wa shule, vyuo vikuu, maana hapa tunakuja Bungeni tunawaleta watoto wa shule, tunawaleta watu kutoka vyuo vikuu, wanahamasika. Kwa hiyo na hiyo itatumika zaidi ili kuweza kukuza utalii wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa nisisahau, ni suala zima la uhifadhi na usimamizi wa mazingira kwa pamoja. Kwenye mazingira hasa masuala ya takataka na mambo mengine tumeukaribisha utalii Tanzania, kwa hiyo, Serikali nayo inapaswa kuanza kufahamu kwamba tayari tunavyoleta wageni nje ya nchi wanakuja na vifungashio vyao tofauti, wanakuja na material yao tofauti ambayo sisi kama utamaduni wetu yalikuwa hayapo.

Kwa hiyo, hatuna budi kwanza pia ku-focus na kwenye masuala mazima ya uhifadhi wa mazingira ili takataka ambazo zipo zinazalishwa kwenye upande wa utalii zisiwe zinachomwa, zisiwe zinapelekwa baharini na zisiwe zinafanyiwa mambo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tujifunze pia masuala mazima ya recycling, tutumie akinamama, tutumie vijana wetu ambao hawana kazi, wajifunze kwenye utengenezaji wa mbolea na masuala mazima mengi kwa ajili ya kukuza uchumi wetu, lakini na kutengeneza step ya kutoka hapa tulipo na twende kwenye hatua ambayo tunataka utalii ukue. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)