Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mtera
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kunipa muda huu mfupi ili nichangie katika hii Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza, wametoa pongezi zao nyingi sana kwa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na mimi bila kupoteza muda nawapongeza sana kwa kazi nzuri wanayofanya na kwa kweli mimi nawakaribisha Jimboni kwangu ili tuweze kutembelea vivutio vipya vya utalii. Kama Waziri hatakuwa na nafasi basi naweza kwenda na Naibu Waziri na kwa sababu kule barabara ni mbovu, wakati mwingine tunaweza tukalala huko huko kutokana na ubovu wa barabara. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Wizara zitachukua ushauri japo nusu tu wa Waheshimiwa Wabunge, zitakuja na kitu kizuri sana. Wabunge wameshauri kwa ufasaha na kwa ufundi mkubwa sana. Wasiwasi wangu tusije kuwa tunatwanga maji kwenye kinu, wanayachukua hapa lakini hawaendi kuyafanyia kazi. Hebu tujifunze kufanyia kazi ushauri wa Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kwenye vivutio vipya, tuna tatizo la kugundua na kuvivumbua vivutio vipya vya utalii. Hapa Dodoma Mjini, katikati ya Tanzania wameweka pale Jiwe na wameweka alama pale, hakuna shughuli zozote za utalii zinaendelea pale. Pale tungeweza kujenga hoteli, tungeweza kupika vyakula vya makabila yote ya Tanzania. Mtu akitembea hapa anaenda anatalii katikati ya nchi ya Tanzania, lakini hatuvumbui! Ukisikia jina la Dodoma kuna mahali tembo alizama hapa karibu na St. John, ndiyo Mgogo akasema tembo idodomela, ndiyo ikaanza Dodoma, Mzungu akashindwa kutamka. Hakuna shughuli zozote zinafanyika pale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nenda katika Jimbo la Kibakwe, hapo Pwaga, kuna ndege ambao dunia nzima hawapo wako kwa Mheshimiwa Simbachawene, tena Mheshimiwa Simbachawene ni rafiki mkubwa wa Waziri lakini hajawahi kumkaribisha akaangalie. Kwa hiyo, ningeshauri tuendelee kuvumbua vivutio vipya vya utalii. Tunajenga uwanja mkubwa wa ndege hapa Msalato. Hivi mtalii atashuka Msalato, aende Iringa kilometa 274 halafu ndiyo aende kuzitafuta tena kilometa 160 na kitu wakati tuna barabara kati hapa ambayo ni njia fupi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa barabara hii ukitoka hapa unaenda Mpunguzi, ukitoka Mpunguzi unaenda Mwitikila, ukitoka Mwitikila unaenda Nagulo, ukitoka Nagulo unaenda Uzi, ukitoka Uzi unaenda Manda, unavuka mto Kizigo tayari umeshaingia Ruaha National Park kwa kilometa 125 tu. Badala ya kutembea kilometa 300, ukikatiza hii njia ya kati unafika kwenye maeneo ya utalii kwa urahisi Zaidi, tuimarishe. Kwa hiyo, sio lazima watalii wazunguke mbali, kilometa nyingi wanaenda kutafuta wanyama wakati ukikatiza hapa katikati unafika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuna vivutio vingi sana. Ukija kwenye jimbo langu mimi kuna mapango yako hapo Kata ya Ilolo. Ukitembea hapo unaenda unakuta mapango mazuri, watu huwa wanaenda pale wakati mwingine wanaomba na mvua inanyesha hapo hapo, hata kama jua ni kali. Kuna jiwe moja kubwa sana liko Mloda pale, nawakaribisha Wizara waende wakaangalie, kuna vivutio vingi, vingi vingi, vinaweza kutusaidia nchi hii kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kitu kimoja nataka nishauri hapa. Suala sio kwamba wanyamapori wameongezeka kuvamia mashamba yetu, hapana. Sisi tunachoshauri kingine ni uharaka wa kuwafukuza. Mnyama anaingia, anashinda humo analala mpaka siku tatu. Hivi, tunasema eti oh! Hakuna silaha, hakuna watu, hawawahi mbona Bunge linawahi hapa Tanzania? Bunge halijawahi kuchelewa, saa tatu kamili limeanza. Mbona Bunge halichelewi? Kwa hiyo, Taasisi kubwa kama hii lazima tuipongeze, hakuna siku Bunge limechelewa hata dakika moja. Bunge ni saa tatu kamili kila siku na saa tatu kamili Bunge liko hewani. Mbona sisi tunawahi? Taasisi zingine za Serikali zinashindwa wapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, tumewafundisha vijana ulinzi shirikishi. Hivi kwa nini wale vijana tuliowafundisha ulinzi shirikishi kwenye kila kijiji kama pale Handali wapo vijana wazuri sana. Manda kuna vijana wazuri sana. Ukienda Chiluhuru kuna vijana wazuri sana wamefundishwa na nyie. Kwa nini wale vijana wasipewe silaha ili wawafukuze wanyama wakifika? Wanawaaminije kuingia mpaka hadi kwenye hifadhi wawafukuze majangili lakini hawawaamini kwenye kulinda mali zao? Kila Kijiji kingeweza kununua silaha, sio kusema kwamba wanaua wanyama, wazitumie kufukuza wanyama kwa sababu wamewaelimisha wao na Askari walio nao ni wachache.
Mheshimiwa Naibu Spika, vijana wale ambao tumeshawafundisha, tuwafundishe vile vile kujilinda kwa sababu kujilinda ni haki ya mtu. Mbona jambazi akiingia ndani mtu anamuua jamani na wala hashtakiwi na mtu yeyote? Sasa tembo anaingiaje kwenye shamba la mtu anakula, anamaliza, anakula anamaliza tunakuja hapa tunajadili habari ya kifuta machozi, kifuta jasho, wakati tungesema vijiji vyote vinavyopakana na wanyamapori na ambavyo vimesajiliwa, kila kijiji kimiliki silaha kwa ajili ya kufukuza wanyama hatari wanapoingia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)