Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kutoa mawazo yangu niliyotumwa na wananchi wa Jimbo la Kwela katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu kwa kazi nzuri wanayochapa katika Wizara hii, wataalam wa Wizara hii pamoja na Kamati ya Bunge inayosimamia Wizara yao kazi ni nzuri, niwape pongezi zangu za dhati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya pongezi zangu, naomba niwakumbushe Mheshimiwa Naibu Waziri na Waziri hapo. Mnamo tarehe 12 Februari niliuliza swali kuhusu mgogoro wa Uwanda Game Reserve kule katika Jimbo langu la Kwela. Huu mgogoro umetutesa sana wananchi, hasa wa Kata ya Kapenta, Nankanga, Kilangawani na Kipeta baada ya hili pori kuchukuliwa na askari wa TAWA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwanzo lilikuwa linamilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, mwaka 2013 walipochukua ndio matatizo yalipoanza, maisha ya wananchi yamekuwa ya mateso miaka saba. Naibu Waziri ni shahidi, kila wiki nampigia simu zaidi ya mara mbili nampelekea migogoro, nashukuru ananisaidia, wananchi wangu juzi walinyang’anywa mipunga na askari, wamerudishiwa. Pia wavuvi wale wa Forodha ya Nankanga waliokuwa wamelazimishwa walipe shilingi milioni nane, Waziri ameingilia kati hawakulipa zile shilingi milioni nane. Nawapongeza kwa jitihada hizo ni nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hii ni ad hoc solution, tunatakiwa tuwe na permanent solution. Baada ya askari wa TAWA kuchukua pori lile mipaka ilivurugwa, haieleweki, kwa hiyo, wananchi wamebaki dilemma kwa miaka saba. Wamekuja Mawaziri waliowatangulia wanaahidi na wakawaambia wananchi tumeunda timu ya Mawaziri saba tutawapa majawabu, mimi nimekuwa nikifuatilia hayo majawabu sijayasikia, wananchi wako hawajui kinachoendelea. Kwa bahati mbaya hii Uwanda Game Reserve hata wanyama wenyewe sio wengi, wako tembo wanne na nyati wawili tu na kwa miaka minne iliyopita tumepata watalii wawili tu, for four years watalii wawili. Kwa hiyo, imekuwa ni cost generation centre rather than revenue generation centre. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri, kutokana na mabadiliko ya tabianchi Ziwa Rukwa linakua, limekua mpaka limeingia kwenye hifadhi, wavuvi wakiingia kuvua kwenye hili wanawakamata…
T A A R I F A
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Cecil Mwambe.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nampa Taarifa mzungumzaji kwamba kilichopo kwenye hiyo game reserve anayoitaja, tuna game reserve pia nyingine iko Masasi DC inaitwa Misyenjesi. Wananchi wanatamani waachiwe lile eneo wafanye shughuli zao za kilimo kwa sababu haina manufaa yoyote kwao na hakuna wanyama pale ndani.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Deus Sangu, unapokea Taarifa hiyo?
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naipokea hiyo Taarifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nitoe ushauri kwa Wizara hii, waliniahidi kwamba, tutaenda kutembelea hili pori. Nashukuru, nasubiri hiyo ahadi yao na aliniahidi Waziri kwamba, tukimaliza bajeti hii tunaenda.
Mheshimiwa Naibu Spika, wavuvi wanakamata vifaa vyao. Boti ukilichukua ukalitoa kwenye ziwa ukaweka nchi kavu miaka mitatu, baada ya hapo wakifanya mnada inakuwa ni kuni, inakuwa hasara kwa mvuvi pia inakuwa hasara kwa Serikali, hakuna kitu kiinachozalishwa pale. Kwa hiyo, niwaombe sana ili tuondoe migogoro hii na kufanya ile Uwanda Game Reserve tutoe vibali kwa wavuvi wakavue kwa vibali, kwa sababu kitendo cha kutotoa vibali mmewahalalishia askari waanze kuchukua rushwa. Mvuvi anatoa shilingi milioni moja, hela zinaenda kwa mtu binafsi, Serikali hawapati chochote, si bora watoe vibali ili waingize fedha katika Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwaombe sana Wizara hii. Migogoro hii hata Rukwa Lukwati kule kuna mgogoro wa aina hii, wavuvi wananyanyasika sana. Wavuvi wanakuwa charged mpaka shilingi milioni tatu, hizo fedha wanachukua askari binafsi, Serikali haipati hata senti moja, mateso ni makubwa, wananchi wameumizwa sana. Niwaombe sana watakapokuwa wana-wind up watoe kauli, migogoro ile wataimaliza lini ili la wananchi wa Kata ya Nankanga, Kapenta, Kipeta, Kilangawane, wafurahie kwamba, kuwepo kwa ile Uwanda Game Reserve kuna faida kwa sababu, wanatusaidia katika bio diversity conversation. Wamekuwa wakitusaidia pamoja na kwamba hamna watalii, lakini pia utunzaji wa mazingira, lakini wananyanyasika sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)