Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuchangia bajeti ya Wizara hii ya Fedha.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha kusimama ndani ya Bunge hili siku ya leo, pia nipongeze Wizara hii Mawaziri Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri Katibu Mkuu na Watendaji wote kwa kazi nzuri naunga mkono hoja hii iliyowasilishwa hapa lakini pia naunga mkono taarifa ya kamati ya bajeti yetu ambayo imewasilishwa hivi punde. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba taarifa iliyotolewa na hata msemaji wa Serikali amezungumza uchumi wetu umeshuka kutoka asilimia 6.9 mpaka asilimia 4.7 na moja ya sababu ambazo zimeelezwa ni changamoto ya ugonjwa huu wa COVID-19, lakini nataka niipongeze kwa dhati Serikali hii ya Awamu ya Sita pamoja na changamoto hiyo na kupitia Wizara hii ya Fedha imekuwa ikiwezesha shughuli mbalimbali zinaendelea ikiwemo miradi ya kimkakati kama ambavyo imeelezwa hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa dhati pia nimpongeze Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kuidhinisha fedha takriban bilioni 172, kwa kila Jimbo milioni 500. Nina imani Mkoa wetu wa Pwani utapata bilioni nne na milioni mia tano pamoja na kwamba Meneja wa TARURA wanawasiliana na Wabunge wa Majimbo lakini niwaombe Wabunge wenzangu wa Viti Maluum nasi tusikae nyuma katika jambo hili tulifuatilie kwa sababu pesa hizi zinaenda kusaidia kurekebisha miundombinu ya vijijini wanakoishi wanawake wengi, wanakojihusisha na shughuli za kilimo na kadhalika. Kwa hiyo, nasi tunayo nafasi tutakaporudi baada ya Bunge hili kufuatilia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nipongeze uwezeshaji katika sekta ya afya kwa Wizara hii ya Fedha takriban bilioni 121 zimekwenda kwa ajili ya madawa, pia takriban bilioni 43 kwa ajili ya kumaliza miundombinu ya hospitali ambapo watumiaji wakubwa ni akina mama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo yote haya yamefanyika kutokana na makusanyo ya mapato, licha ya mawasilisho ya taarifa ya ukusanyaji wa mapato mpaka mwezi Mei na kuonesha kwamba mapato yaliyokusanywa ni asilimia 82, naomba niishauri Serikali kwamba moja ya jambo ambalo pia hata Mheshimiwa Rais Mama Samia ameahidi kwa Watanzania na ndani ya Bunge hili ni kuendeleza mazuri ya Awamu zilizopita na kuanzisha mazuri mapya. Moja ya jambo la kujivunia mazuri hayo ni katika ukusanyaji wa mapato Serikali ya Awamu ya Tano ilikuwa inafanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato. Kwa hiyo hili jambo ni ahadi ambayo Wizara ya Fedha na Mamlaka zinazohusika hususan TRA na mamlaka zingine hazina budi kutekeleza kwa nguvu za zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili ninawashauri pamoja na kwamba ufanisi unaoesha tunakusanya asilimia 12 ya mapato ukizingatia na Pato la Taifa, katika nchi za Afrika Mashariki tunalingana na Uganda, tunazidiwa na Rwanda Pamoja na Kenya lakini bado tuna nafasi kwanza; tuongeze wigo wa kodi mpya, lakini pili; tuongeze wigo wa walipa kodi, tatu; tuendelee kuziba mianya ya ukwepaji kodi. Pamoja na kwamba mazingira ya sasa hivi na kwamba TRA mmeelekezwa nami naunga mkono maelekezo hayo ya kufanya ukusanyaji wa kodi kwa kutumia mbinu za kitaalamu na kwa mujibu wa sheria na matokeo tumeyaona lakini suala zima la kuziba mianya ya upotevu wa kodi iwe kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kubwa tumeona zikianzishwa nafasi za mabalozi mbalimbali kuhamasisha sekta mbalimbali, nashauri Wizara ya Fedha ili kuimarisha sekta mbalimbali inaweza pia nao wakaja na mabalozi wa kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari kwa Watanzania. Sambamba na hilo niwaombe Watanzania tunayo property tax imerudishwa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kila mmoja tuone tuna kila sababu ya kulipa property tax katika mamlaka zetu ili kuwezesha Serikali kufanya kazi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niiombe sekta binafsi wameona namna gani Serikali imewasilisha mipango ya kuboresha mazingira ya sekta binafsi, ikiwemo utekelezaji wa mkakati wa kupitia blue print niiombe sekta binafsi ituongoze katika mapambano ya ulipaji kodi wa hiari na uzuiaji wa ukwepaji wa kodi, wao kwa kuwa ni wafanyabiashara wakubwa, wawekezaji, Serikali kazi yake ni kuandaa miundombinu na kwa kuwa tunaamini kuna methali inasema “kwa kungwi kuliwe na kwa mwali kuliwe” kwa hiyo, nao wana nafasi kubwa kuiwezesha Serikali kukusanya kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo kwa kuwa pia Wizara ya Fedha wamewasilisha maombi ya bajeti ya Ofisi ya Taifa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, niombe yale yote aliyoyashauri kupitia ya bajeti 2019/2020, hususani kwenye mapato na suala nzima la kuwezesha mamlaka za kusikiliza rufaa za kodi, kwa sababu kwa mujibu wa taarifa ya CAG ya 2019/2020, takribani kuna kesi au mapingamizi ya kodi ya trilioni 360 na CAG ameshauri Serikali iwezeshe kibajeti na masuala mengine ili mapingamizi haya yasikilizwe. Naamini yako mapato kupitia mapingamizi haya ambayo Serikali itayapata.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kwa kuwa Serikali imeandaa mazingira mazuri ya Sekta binafsi, kuna suala la malipo ya wazabuni ya muda mrefu, ripoti ya CAG imesema zaidi ya bilioni 81 hazijalipwa.

Mheshimiwa Spika, pia kuna ucheleweshaji wa malipo ya wazabuni ambayo yanaweza kuwa kichocheo katika kuongeza ukwasi wa pesa kwenye uchumi, inasababisha malipo ya ziada ya gharama za kuchelewesha. Serikali katika ripoti ya CAG inaoneshwa inadaiwa zaidi ya bilioni 14 ikiwa ni tozo za ucheleweshaji wa malipo ya wakandarasi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali pamoja na kwamba wanakusanya mapato, lakini yapo matumizi ambayo yanatumika kuongeza ukubwa wa matumizi ya Serikali ambayo yangeweza kuepukwa kama mikakati ya kufanya uhakiki wa madai hayo, kuzingatia kifungu cha 51 cha masharti ya jumla ya mkataba, kwamba mkandarasi anapaswa kulipwa ndani ya siku 28, baada ya certificate yake kupitiwa na Meneja wa Mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwisho kama nilivyosema, jukumu la kuinga mkono Serikali yetu ya Awamu ya Sita na kuiwezesha kutekeleza miradi ni la Watanzania wote na tutalifanikisha kwa kulipa kodi. Niwaombe tulipe kodi, lakini niombe pia, zipo taarifa vituo vya mafuta vimeanza wakati mwingine kuuza mafuta hata bila kutoa risiti. Serikali iiwezeshe Mamlaka ya TRA waipe kibali iajiri watumishi wengi zaidi ili wapange kwenye suala zima la ukaguzi, iwawezeshe kifedha. Vile vile Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, iwezeshwe kama ambavyo kwenye bajeti hii imewasilishwa.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, mwisho, nawapongeza Fungu Namba 7 la Ofisi...

SPIKA: Mheshimiwa subiri kidogo, kuna taarifa. Mheshimiwa Waziri wa Fedha.

T A A R I F A

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, naomba kutoa taarifa kwenye Bunge lako Tukufu kwamba hotuba anayoitoa Mheshimiwa Mbunge ya kuhusu kulipa kodi kwa hiari ni jambo la msingi sana na tunatamani hata tuongee na wenzetu wa elimu waanze kuwafundisha watoto kuona pride ile ya kulipa kodi kwa hiari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nchi za wenzetu mtu akisahau risiti hata kama alishaenda mbali anairudia, lakini sisi watu wetu bado wanatamani wapewe bei zile zisizo na risiti na kwa maana hiyo namteua kuwa balozi wa walipa kodi kwa hiari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Subira taarifa hiyo unaipokea.

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, taarifa hiyo nimepokea na nimepokea uteuzi wa Balozi wa walipa kodi kwa hiari na nimuahidi Mheshimiwa Waziri wa Fedha Dkt. Mwingulu Nchemba na Serikali ya Awamu ya Sita nitaifanya kazi hiyo kikamilifu baada ya Bunge hili, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, nitaendelea kuhamasisha kwa Mkoa wetu wa Pwani na kwa Halmashauri ya Chalinze na Halmashauri zote, kupita kila eneo kuhamasisha ulipaji wa kodi ya hiari, property tax, kupitia kwenye vituo vya mafuta.

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa heshima hiyo aliyonipa kuwa balozi wa kwanza wa kulipa kwa hiari ndani ya Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)