Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nadhani ni wakati muafaka kwa Waziri wa Fedha kutuambia kwamba kama makusanyo ya mapato yetu ni mazuri kwa kiwango hicho, asilimia 82 tunaambiwa mpaka sasa, inakuwaje ni changamoto kubwa sana inapokuja kwenye suala la utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Spika, kwangu haiingii akilini kama tunajisifu performance ya makusanyo yetu, lakini ukija kwenye bajeti ya Kilimo utekelezaji ni less than fifty percent, ukija Viwanda na Biashara, ukija Maji, ukija Ujenzi, yaani tunakusanya vizuri, lakini ikija kwenye utekelezaji wa maeneo ambayo ni muhimu na nyeti, kwa mustakabali wa Taifa letu performance hairidhishi kwa nini?

Mheshimiwa Spika, la pili, niungane na hoja ya Kamati kwamba, kichaka cha uhakiki kinaumiza sana wakandarasi wetu wa ndani, kinaigharimu sana Serikali kwa sababu ya riba ama kwa sababu ya adhabu kwa kutekeleza mikataba nje ya muda.

Mheshimiwa Spika, protocol ya Afrika Mashariki kama ambavyo imeelezwa, ilielekeza wazi kwamba uhakiki ukishafanyika, wananchi ama wakandarasi weather ni wa ndani ama wa nje wanatakiwa walipwe ndani ya siku 90 baada ya uhakiki. Kama hawatalipwa ndani ya hizo siku 90, hilo deni litaenda ama hayo madai sasa yaliyohakikiwa yatatoka kwenye madai, yataingia kwenye deni la Serikali ili hawa wakandarasi wawe na uhakika wa kulipwa kwa sababu kwa taratibu za nchi yetu, deni la Serikali ni first charge, yaani lipo la kwanza. Kama tukipitisha bajeti la deni la Taifa, tumekadiria linaenda kulipwa trilioni nane mpaka 10, kama tumeweza kukusanya trilioni 20 ama 30 kitu cha kwanza cha kulipa ni deni la Serikali ikifuatiwa na mishahara ya watumishi na vitu kama hivyo.

Mheshimiwa Spika, sasa leo ni bahati mbaya sana Serikali badala ya kutimiza wajibu wake kuweza ku- encourage wafanyabiashara, wakandarasi wa ndani ili biashara ziweze kukua ama waweze kukuza mtaji, Serikali ndiyo inaminya. On very serious note Kamati ya bajeti imeona lakini tunaomba leo Waziri atuambie commitment ya Serikali ya kukubaliana na mapendekezo ya Kamati ya Bajeti kwamba kuwe na deadline ya uhakiki.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa naangalia tu kwa mfano madeni tu ya kawaida katika Sekta ya Ujenzi, ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambaye amefanya ukaguzi maalum wa miradi ya maendeleo, anatuambia madai ya wakandarasi ambao hawajalipwa kwenye ujenzi peke yake ni trilioni 1.03, ikijumuisha milioni 224 riba ya adhabu kwa Serikali kushindwa kutekeleza mkataba kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa unajiuliza common sense ya kawaida, tuna Wachumi nchi hii wabobezi, tuna Wanasheria nchi hii wabobezi, hivi ni akili kweli, unaingia mkataba kujenga barabara ukijua uwezo wako wa kifedha, unashindwa kulipa ndani ya muda, unatozwa adhabu kwenye Sekta ya Ujenzi milioni 200, yaani hii ni adhabu, hivi hizo ni, yaani najiulizaga nasema ni akili au, nikitumia lile tope watu wanakasirika, lakini tujiulize hii milioni 200 sijui na nne, ingejenga kilometa ngapi za barabara. Huu ni mfano mmoja kwenye ujenzi; tukienda kwenye maji habari ndiyo ile ile; tukienda kwenye kilimo, habari ndiyo ile ile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, REA, Serikali inadaiwa na wakandarasi mpaka mwaka 2020, tunajisifu hapa umeme vijijini, umeme vijijini, tunapiga swaga kama vile kila kitu ni perfect, kumbe huku wakandarasi wanaumia. Tunadaiwa kwenye REA trilioni moja, umeme vijijini, hapa sijazungumzia kabisa wakandarasi wanaotoa huduma kwenye Wizara zetu matrilioni.

Mheshimiwa Spika, kitu ambacho Kamati ya Bajeti inasema, hivi viporo vinatokana na the so called uhakiki, Serikali inajua, wakihakiki wanatakiwa ndani ya siku 90 walipe. Kwa hiyo wanachoamua wanakauka hawahakiki huku wanaumiza watu. Mbaya zaidi tunakuwa hatupati taarifa sahihi ya deni la Serikali. Tunadangayana hapa deni la Taifa lilikuwa trilioni 59 juzi la Serikali siyo la Taifa, maana tukiweka huko la Taifa tunafika trilioni 70 la Serikali.

Mheshimiwa Spika, juzi nasika Waziri Mheshimiwa Mwigulu jana ameingia mkataba, maana tunaenda tirioni 60 point kadhaa, lakini madeni kama haya yangeingizwa kwenye utaratibu waliokubaliana kwenye protocol, tungejua Taifa tunadaiwa nini, matokeo yake tunajidanganya, deni letu ni himilivu, lakini tuna madeni yaliyojificha kwenye kichaka. Naomba Mheshimiwa Waziri atujibu seriously hiyo siyo ajenda yangu, ni haja ya Kamati ya Bajeti, Kamati ya Mheshimiwa Spika.

Mheshimiwa Spika, la pili, dhuluma iliyojificha kwenye kichanga cha kusafisha. Wakati sisi tunakuwa enzi hizo ilikuwa ni jambo la kawaida kabisa na ambalo lililindwa na mfumo, Halima nimemaliza zangu form four nina ndugu yangu pale, ndugu yangu anakuja kutumia cheti cha Halima. Akishatumia cheti cha Halima, anaenda kusoma diploma, degree ama masters, anasoma PhD ndiyo ilikuwa life style. Kwa sababu kiteknolojia tulikuwa hatuna mfumo wa kufanya tracking, siyo kwamba sasa hivi DNA tu unaweza kujua nani kafanya nini, mfumo ambao Serikali iliutekeleza ikaulinda yenyewe.

Mheshimiwa Spika, kilichotokea, maskini ya Mungu, watu wameenda wakaenda wakasoma degree zao, wengine wakaenda wakasoma PhD professionals lakini ametumia cheti cha Halima. Leo wanaitwa wenye vyeti fake, yes is true kwa sababu alitumia cheti change, lakini Serikali inadhani ni fair kibinadamu. Unajua saa nyingine unaweza ukajikuta unapata laana kwa kudhulumu tu. Serikali inadhani ni fair, watu kama hawa kufukuzwa kazi na kunyimwa hata shilingi mia, is it fair kibinadamu? Yaani mfumo tumeutengeneza wenyewe, kwa kutumia mfumo tumeenda tumewasomesha wenyewe licha ya kwamba alichukua cheti cha Halima cha PhD anatumia lakini ni hapana, ni kwamba alichukua cheti changu na wengine tulikuwa nao wanasiasa, lakini wakachuniwa tu kwa sababu wana political influence, hivi Serikali inadhani ni fair?

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia nia njema ya Mheshimiwa Mama Samia aliyoionyesha kwa wale waliomaliza darasa la saba wakatolewa kwenye mfumo kwamba walipwe stahili zao, naomba Mheshimiwa wa Fedha atuambie mustakabali wa watumishi hawa waliolitumikia Taifa hili kwa jasho na damu ukoje? Hivi wako tayari kudhulumu mtu ambaye ametumia muda wake wote wa maisha yake kufanya kazi ya utumishi Serikalini, akabakiza miaka miwili astaafu, mshahara wake wenyewe ni tia maji tia maji...

T A A R I F A

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Taarifa, ndiyo Mheshimiwa Mpemenwe.

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji, Mheshimiwa Mdee yeye ni Mwanasheria mzoefu na anajua kwamba sheria huwa haina excuse, huwezi ukatoka ukaenda ukaibah ukasema nimeiba kwa sababu nilikuwa na njaa.

Kwa kuwa ameshakiri yeye mwenyewe kwamba hawa watu walitumia vyetu ambavyo siyo vya kwao, halafu anakuja mbele ya Bunge lako kuja kuzungumza kitu cha namna hii na ukizingatia kwamba yeye ni Mwanasheria, naomba aifute tu hiyo kauli.

SPIKA: Mheshimiwa Halima, taarifa hiyo unaipokea.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, si unajua tena nanilii anajua, mimi naomba niendelee. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nimesema hivi kibinadamu sheria tuna tunga binadamu, watu wametengeneza mfumo ambao ulikuwa unaruhusu hayo mambo kufanyika, watu wakaenda kusomea taaluma kwa kulipiwa na Serikali hii hii, wamehudumia Taifa hili kwa miaka 10, 15, 20,30 wanawatoa kapa, siyo ubinadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la tatu, huduma za Mfuko Mkuu Fungu la 22, pamoja na mambo mengine unawajibka kusimamia na kulipa malipo na michango ya mwajiri kwa watumishi wote wa Serikali pamoja na taasisi zake. Mheshimiwa Waziri wa Fedha, Wizara yake ndiyo ina jukumu la kuhakikisha kwamba michango ya wastaafu watarajiwa inapelekwa kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Mheshimiwa Spika, sasa leo nataka Mheshimiwa Waziri anieleze, maana juzi Mheshimiwa Mhagama alipiga mkwara mzito na nilimkubali, akasema waajiri wote na nitafanya ukaguzi mahususi na mkirejea waajiri ambao ni wa vyombo vya habari na waajiri wengine ambao hawapeleki michango ya watumishi. Sasa leo nataka Serikali iniambie hivi kwa nini na yenyewe haipeleki michango ya watumishi wao? Hivi uhakiki ule wataufanya kwa sekta binafsi ama watafanya na kwao?

Mheshimiwa Spika, ni aibu CAG anatuambia kwa sababu ndiyo amepewa mamlaka ya kukagua kwamba kwa mwaka wa fedha ulioishia mwaka 2019 ambao ripoti ilitoka mwaka 2020, walikuwa hawajapeleka michango shilingi bilioni 171; PSSSF milioni 61, NHIF milioni 24, WCF bilioni 85.

Mheshimiwa Spika, taarifa aliyoitoa juzi inaonesha kwamba hamkuwasilisha Taasisi za Umma zaidi ya shilingi bilioni 20.9 na michango ya PSPF ikiwa ni shilingi bilioni 7.7. Sasa sisi tunajua namna gani kwanza hii mifuko inaumizwa sana kwa Serikali kukopa, lakini hailipi. Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, tunajua namna gani hii mifuko inaumizwa sana; kwa sasa hivi tumeanzisha utaratibu tunasema tunajenga viwanda, lakini tunajenga viwanda kwa kutumia mabilioni ya hii mifuko, hatukatai. Bahati mbaya viwanda sasa hivi vinatangeneza hasara; hiyo ni ajenda nyingine tutakuja kuizungumza. Ila tunatujua tusipopeleka fedha, tunaathiri ukwasi wa mifuko na tunaathiri wastaafu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami naomba Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, rafiki yangu, ukija hapa, maana hili siyo tatizo la Mheshimiwa Jenista, hili tatizo ni lako mtoa pesa. Mheshimiwa Jenista yeye anawasimamia tu hawa. Utuambie Mheshimiwa Mwigulu Nchemba ni kwa nini hupeleki fedha za wastaafu? Utuambie ni lini hizi fedha za wastaafu zitalipwa kwa ukamilifu wake? Zamani ilikuwa mtumishi akistaafu, ndani ya miezi sita amepata kwake anatulia nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hivi mtumishi akistaafu, yaani anakufa kabla hajapata. Akifa ndiyo warithi sijui wanaitwa nani hao, watu wa mirathi hawa; kwa hiyo, naomba sana, hili jambo ni nyeti, zito, linaumiza wananchi wetu, tuambiwe haya madeni yataenda kulipwa lini? Kubwa zaidi Mheshimiwa Jenista nilikuwa nakuomba, ile fimbo uliyokuwa unaenda kuwachapia waajiri wale ambao hawapeleki michango yao, isiishie sekta binafsi. Tunaomba upite humo humo Serikali ili utuletee ripoti hapa Bungeni, maana uliji- commit hapa kwenye Serikali hii, watu sugu wa kutoa hii michango ni akina nani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho siyo la umuhimu limezugumzwa na Kamati hapa, ukomo wa kuajiri ama ikama ya ajira. Kuna maeneo ambayo watumishi wakiwa wamepungua, yanaweza yasiwe na madhara makubwa sana, lakini kuna maeneo ambayo Serikali mnatakiwa mhakikishe idadi ya watumishi inakuwa kama ambavyo wanahitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi kweli ni akili pale ambapo mamlaka iliyopewa jukumu la kukusanya mapato, tumekaa hapa tunasema hatuna vyanzo vya mapato, mapato hatukusanyi ipasavyo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, naomba nimalizie.

Mheshimiwa Spika, ni akili kwa TRA kuwa na upungufu wa wafanyakazi? Hivi ni akili kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anayekagua pesa zetu na matumizi yake kuwa na upungufu wa wafanyakazi?

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, naomba hili liangaliwe kwa umakini na tupate majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)