Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vunjo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, nimewasikiliza wenzangu vizuri sana lakini kabla sijasema hapo, nitumie fursa hii pia kumpongeza Waziri, Naibu wake, Katibu Mkuu na uongozi mzima wa Wizara.
Mheshimiwa Spika, lakini pia tumpongeze yule aliyekuwa anashikilia Wizara hii, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, ambaye aliweza kusimamia Ilani ya CCM tukaweza kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati na tukapata ushindi sisi tunaoingia sasa kama Wabunge. Naona ni vigumu sana kujua walifanyaje wakaweza kutekeleza miradi hiyo na hali kwamba deni letu likabakia bado himilivu.
Mheshimiwa Spika, mimi nilikuwa najua kwamba bajeti ni sheria, lakini naamini hii ya kwetu siyo sheria, kama inatungwa bajeti tumekaa hapa miezi mitatu tunatunga bajeti hapa halafu tunaambiwa imetekelezwa kwa asilimia 50; nani anashikwa, nani anapelekwa kortini? Nani anawajibika kwa hilo? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nafikiri lazima sisi wenyewe tujue kwamba sisi ndio tunatakiwa tuwajibike pengine kwa sababu hatukuweza kuisimamia Serikali ikaja na bajeti ambayo inatekelezeka kwa asilimia mia moja, ahadi zinazotolewa hapa zikatekelezwa kweli. Wewe utaahidiwa mradi lakini mradi hautatekelezeka kwa sababu kama mapato hayatapatikana hatutapata hiyo miradi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina shaka sana kwa sababu tunajua kwamba kazi kubwa ya Wizara ya Fedha ni kutafuta mapato, matumizi tumeshajua, kwa hiyo ni kutafuta mapato yatakayokidhi utekelezaji wa bajeti ile. Sasa mapato yanatokana na kodi au kukopa.
Mheshimiwa Spika, sasa nafikiri sana Waziri achakarike aanze kutafuta mikopo, siyo ya ndani. Naona wenzetu alipokuwa Mheshimiwa Msuya alikuwa kila saa yuko nje anatafuta fedha za kuweza kutekeleza bajeti, siyo lazima upate yote ndani, na ukipata yote ndani ndiyo inasababisha haya mambo tunayoona sasa kwamba mwenzangu anasema kwamba riba ziko juu sana.
Mheshimiwa Spika, bahati mbaya amesema kwamba Benki Kuu ndiyo inapangia benki viwango vya riba, lakini Benki Kuu kusema kweli haipangii mabenki viwango vya riba isipokuwa wanakuwa ni waelelezaji kwa zile riba ambazo wanatoa kwa dhamana za Serikali.
Mheshimiwa Spika, nimeona kwenye bajeti ya Mheshimiwa Waziri hakuna ongezeko la mshahara, badala yake mishahara inapungua… lakini nataka niseme kwamba pengine ni muda sasa wa kufikiria ongezeko la mshahara kwa wafanyakazi wa Serikali. Kwa sababu ni miaka mitano na … tulisikia Mheshimiwa Rais akisema kwamba ataona namna, lakini kama hatujaingiza kwenye bajeti inakuwa kwamba ni matatizo. Hakuna Wizara hata moja iliyoonesha kwamba kutakuwa na ongezeko la mshahara, na mimi nataka Waziri wa Fedha aliangalie kwa upya aone litafanyikaje. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika kupunguza makali ya utekelezaji wa miradi yetu, naamini kwamba Serikali inatakiwa kuangalia upya msimamo wake wa kurejesha kwa Msajili wa Hazina yale mashirika yaliyokuwa yamebinafsishwa sekta binafsi ikashindwa kuyaendesha halafu Serikali inarudisha. Kitu ambacho kimeshindikana kwa sekta binafsi kwa biashara, Serikali haitaweza.
Mheshimiwa Spika, unless unasema kwamba hiyo ni mkakati kama Air Tanzania. Kama ni Air Tanzania twende kwa sababu tunajua ni mkakati, basi. Lakini lazima tuangalie ni mashirika yapi; ni viwanda au ni taasisi zipi ambazo zilikuwa zimebinafsishwa halafu zikarejeshwa, tuone mkakati wake uko wapi. Kama upo then tuendelee lakini siyo hivyo, tunaona kwamba Msajili wa Hazina ametoa ruzuku na nyongeza kwa mitaji ya mashirika takribani shilingi bilioni 27. bilioni 27 ni hii 500 tumepewa kwenye majimbo yetu mara tatu? Kwa hiyo, naomba hiyo iangaliwe vizuri.
Mheshimiwa Spika, sasa niseme hivi; mimi nafikiri katika mambo yote ya kukusanya kodi ambayo ni kazi kubwa ya Wizara, mahali penye leakage kubwa ni kule kwenye Serikali za Mitaa. Serikali za Mitaa hawakusanyi, na wakikusanya zinaingia mifukoni mwa watu. Kwa nini tunawaambia kwamba waingie kwenye GEPE, muda mwingi kule kwenye vijiji vyetu kwenye halmashauri hakuna mawasiliano, hawana Point of Sale za kukusanya hayo mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo unakuta kwamba ukimpa mfanyakazi Point of Sale akatembea nayo barabarani huko, haina hata risiti ile roll imekwisha, unakuwa ni mtaji kwake na ukimnyang’anya analia machozi ya damu, anakwambia umrudishie hiyo Point of Sale kwa sababu anajua kwamba ni njia rahisi sana ya kupata mtaji wa bure. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na naomba kwamba ili mradi hatuwezi kusambaza Point of Sale za kutosha kwenye halmashauri zetu, kwenye vijiji kwa sababu na kule wanakusanya kodi, tusiseme kwamba tutakaa tu tuangalie halafu tutakusanya kodi au tutaongeza wigo wa kodi. Naamini kwamba kwa wale walio kwenye wigo wanalipa na wanafuatiliwa lakini kwenye sehemu nyingi watu hawafuatiliwi.
Mheshimiwa Spika, na kitu kitakachotupa mapato kwenye mwaka huu ni usimamizi mzuri. Kwa sababu kwa muda mfupi hatuwezi kuongeza wigo wa walipa kodi, hatuwezi kuongeza kwa siku tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa niseme pia kwamba kwenye suala hili la riba za Serikali, kwa sababu unajua kitu kinacho- drive deni la Serikali zaidi ni riba kubwa. Na ninasema kwamba uhimilivu wa hili deni hautakuwepo kama riba zitakuwa kubwa. Na riba zimekuwa ni asilimia 15.9, alisema mwenzangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wanapokea hiyo, mkopo, kama ni mkopo umelimbikiza mwaka mmoja unaongezeka kwa asilimia 15 na zaidi. Kwa hiyo, inakuwa kwamba hutaweza kabisa kulipa. Tunalipa asilimia 25 ya mapato yetu kwenye ku-service deni hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nafikiri hivi; njia pekee ni kwamba sasa tukubali kwamba inflation au mfumuko wa bei ni asilimia tatu. Na kwa kawaida huwezi kuwa na zaidi ya asilimia nane hapo kwa sababu unaongeza hapo asilimia tano, asilimia tano ndiyo inakuwa ni riba ambayo inakubalika. Inakuwa inflation plus five percent ni eight percent, kwa hiyo, ukiwa juu ya pale ni matatizo, ni majanga kwa sekta binafsi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninachowashauri Benki Kuu na Waziri wa Fedha ni kwamba ile coupon rate ya dhamana za Serikali wanayotoa Benki Kuu, kwa sababu wanasema tuna option na riba itakuwa ni asilimia 15.6. Kwa hiyo, kila mtu anakwenda ku-bid, ananunua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ile coupon rate inayotangazwa asitangaze tena sasa ya asilimia 15, atangaze asilimia kumi; mabenki na wawekezaji wengine hawana mahali pa kuwekeza fedha zao salama zaidi ya kuweka kwenye dhamana. Kwa hiyo, ina maana kwamba watakwenda watu watanunua tu, hakuna njia nyingine kwa hiyo watanunua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na ni kweli kwamba hiyo faida watakayopata bado ni kubwa kwa sababu ni risk free, hawana gharama yoyote, wanakusanya tu bure. Kwa hiyo, naamini kwamba kama tukisema kwamba, okay, kuanzia minada inayokuja, coupon rate yetu itakuwa ni asilimia kumi, anayetaka aje, asiyetaka asije. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya muda watakuwa na maukwasi yamerundikana wataamua kuja kununua kwa asilimia 10. Na hiyo itasaidia pia kushusha riba za mabenki binafsi kwa sababu riba zimelegezwa kwenye riba hizi za dhamana za Serikali. Kwa hiyo, hakuna njia nyingine ya kushusha riba kwenye mabenki kama siyo kufanya hicho, kwamba hatutauza dhamana kwa juu ya asilimia kumi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hivi wanauza treasury bills chini ya asilimia tano, za mwaka mmoja. Sasa kwanini na zilikuwa asilimia 14? Sasa ameshusha, inakuaje kwamba wameshusha hizo za na nanii, na tunajua kwamba upeo wetu wa inflation ndiyo hiyo asilimia tatu. Hakuna sababu ya kushindwa hicho kitu. (Makofi)
Niombe kwamba ikiwezekana, hasa kwenye mambo ya ugawaji wa fedha, wenzangu wamesema, lakini ukweli kama hatutagawa fedha kwa vipaumbele au kwa kuzingatia kasma, hatutakwenda mbali…
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Charles Kimei.
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: …kwa hiyo Wizara ipeleke kufuatana na jinsi ambavyo imepitishwa.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)