Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Condester Michael Sichalwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Momba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kutoa mchango wangu. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ni mwingi wa rehema na huruma zake kuendelea kunipa kibali na nafasi kusimama tena kwenye Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nami niwasilishe maombi yangu kwa Serikali ikiwa ni pamoja na kuishauri Serikali. Kupitia Jimbo langu natoa mchango huu kwa kuwa najua utakuwa unabeba taswira na azma nzima ya Taifa, natokea kwenye eneo la mpakani, tumekulia eneo hilo na kuona kwamba zipo fursa nyingi za ajira, biashara, maendeleo na vitu mbalimbali kutokana na watu ambao wanatoka mpakani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni nini naomba kuishauri Serikali kupitia Wizara hii ambapo wao ndiyo wanatoa fedha na kusimamia rasilimali nyingi za Watanzania. Kuna haja kubwa ya kutazama na kurudia kupitia tena kuona vile ambavyo tunaweza tukaendelea kuimarisha na kuwekeza kwa kiwango kikubwa mpakani.

Mheshimiwa Spika, nataka kutolea mfano wa baadhi ya maeneo ambapo kuna border post (mipaka) za Holili, Namanga na Tunduma yenyewe nitolee mfano, wakazi ambao wanatoka Tunduma hawalimi, hawavui, hawafugi, hawafanyi chochote, kikubwa ambacho wanakifanya pale ni biashara. Sababu ambayo imechochea kuwepo na msukumo mzuri wa biashara Tunduma ni uwepo wa lile gate ambapo kuna mpaka kati ya nchi ya Zambia na Tanzania ambayo nyuma yake inazibeba nchi zote za SADC. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo ipo kwa bandari ya Dar es Salaam kuna ma-gate zaidi ya moja, Serikali inaonaje kuongeza ma-gate kwenye sehemu nyingi za mpakani ambazo zinapelekea kuwepo na mrundikano wa watu, lakini wakati mwingine huduma hizi za forodha kushindwa kutolewa kama inavyostahiki na wakati mwingine Serikali kupoteza mapato? Kama ilivyo Tunduma na sehemu zingine kama Namanga kumetokea uwepo wa wimbi kubwa la watu, watu wengi kupata ajira bila kujali elimu, umri au itikadi ya kitu chochote, imeonekana watu wengi wanapata sana ajira.

Mheshimiwa Spika, mfano watu ambao wanatoka Tuduma ajira zipo kwa wingi kwa watu ambao hawajasoma, kwa watu ambao wamesoma, wafanyabiashara kutoka kila pembe ya nchi hii wameenda kujikita pale wanafanya biashara. Waliofungua hoteli, vituo vya mafuta na huduma za kubadilisha fedha za kigeni, wote hawa wanajipatia riziki.

Je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka kwenda kutuwekea gate kwenye Jimbo la Momba ambalo pia litaenda kusabababisha Watanzania wengine na watu wengine ambao watataka kuwekeza ndani ya nchi yetu kuendelea kupata huduma kama ambazo wanapata katika sehemu zingine za mipaka? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini naomba kuwepo na gate kwenye Jimbo la Momba. Naishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi imetujengea Soko la Kimataifa la Mifugo na Mazao mahali pale. Eneo ambalo limejengwa soko kutoka linapoanzia Jimbo la Tunduma mpaka unapolimaliza Jimbo la Momba ni zaidi ya kilometa 80 lote ni eneo la mpaka. Ina maana kwamba cha kwanza hata ardhi ambayo inayopatikana maeneo yale itakapopimwa itaonekana ni ardhi ambayo ina fursa kwa kuwekeza kwa sababu kila Mtanzania na watu mbalimbali watatamani kwenda kuwekeza pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwenye eneo lile kuna njia za kutumia gari zaidi ya kumi ambazo zinatoka kutoka nchi ya Tanzaia kuingia nchi Zambia. Je, Serikali haioni watakapoweka gate pale itasababisha Wizara ya Ulinzi kuongeza usalama wa eneo lile? Pale Tunduma au sehemu zingine zinapotoa bidhaa kutoka Bandari ya Dar es Salaam wakati mwingine wanapitisha kinyume na taratibu kwa sababu njia zile zipo nyingi. Je, Serikali haioni kwamba tutakapopata gate itatuongezea fursa nyingi, watu watapata ajira lakini pia wawekezaji ambao watataka kufungua hoteli na vituo vya mafuta, shughuli za kibenki zitaongezeka mahali pale na mimi naamini hata ajira ambazo tunaendela kuzi-promote na kuzisema kwa Watanzania hawa zitapatikana. Kwa sababu mama lishe watatokea pale, kwa sababu pale kuna mnada wa mifugo watu mbalimbali wataendelea kujipatia riziki mahali pale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi ninaendelea kuona kwamba ipo namna, tuma watu wa SADC na COMESA waende kuutembelea mpaka ule, wakague na wajiridhishe uwezekano wa kuongeza geti pale. Kama ambavyo tunaendelea ku-promote kuongeza bandari nyingine hata kule Bagamoyo ili kuendelea kutoa huduma nzuri kwa ajili ya bandari yetu ya Dar es Salaam ipo haja pia kwenye mpaka kati ya nchi yetu na Zambia kuongeza geti kwa sababu lipo moja tu pale Tunduma. Wakati mwingine wafanyabiashara wanakaa muda mrefu pale zaidi ya wiki mbili kwa sababu kumeonekana kuwa na mrundikano na huduma hazifiki inavyotakikana hivyo inapelekea hata kupoteza mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kuiomba hata Wizara ya Mama yangu Mheshimiwa Jenista kwamba…

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Condester.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nataka kumpa taarifa Mbunge wa Jimbo mdogo kuliko wote humu ndani kwa akina mama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, anachokizungumza Mbunge hapa ni jambo kubwa na la maana. Kwa mfano, sisi kule Mara yaani mtu atoke Serengeti mpakani wa Masai arudi apite Kirumi aende Tarime border ndiyo aende kutoa mzigo wake. Hivi nani anaweza kusafiri umbali mrefu hivi ili kupeleka hela Serikalini? Kwa nini Serikali sasa isifanye kama anavyozungumza ikague mipaka ya nchi yetu nchi yote ione wapi pa kwenda kuweka wafanyakazi ili watu tuendelee kupata fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzi amezungumza hapa Mheshimiwa Tarimba kwamba kwa mwezi mmoja wenye siku 30 na siku nne, yaani siku 34 wafanyakazi wa Wizara ya Fedha wametumia shilingi bilioni 39. Sasa kwa nini wasidhibiti mipaka hiyo wakaweza kutafuta fedha nyingi ili waweze kupata mapato ya kutumia? (Makofi)

SPIKA: Taarifa inatosha.

Waheshimiwa Wabunge, kabla sijampa nafasi Mheshimiwa Condester, kuhusu hili suala la Wizara ya Fedha na matumizi yaliyofanyika kama Mheshimiwa Waziri Mkuu alivyowatembelea naomba kwa sasa tusiwahukumu kwa sababu bado ni jambo linalofanyiwa kazi halafu taarifa itapelekwa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu labda baadaye tutakuja kupata taarifa halisi. Sasa kwa kuwa linafanyiwa kazi tukipitisha hukumu kabisa nadhani tutakuwa a little bit unfair. Kwa hiyo, naomba hilo tuliache kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Condester, unapokea taarifa?

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, naipokea taarifa ya Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kuiomba Serikali kwamba kama vile Serikali ambavyo inatupia jicho la umakini pale Tunduma kwa sababu inajua inavyonufaika na zile nchi ambazo zipo SADC sasa watashindwaje kulichukua ombi hili na kulitekeleza? Kama mpaka wa Zambia na Tanzania nyuma umebeba mipaka mingine kwa nini tuwe na gate moja? Kwa nini tusingekuwa hata na mageti matatu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu tumeshapewa hela nyingi pale lilipo Soko la Mazao la Kimataifa basi kuna haja kubwa Serikali kutuwekea gate pale. Naamini Watanzania kutoka sehemu mbalimbali watanufaika, vijana wetu wa Kitanzania watapata ajira, mama zetu ambao wanatafuta riziki ndogo ndogo watajipatia pale kama ambavyo ipo Tunduma kwamba hata watu ambao siyo wasomi lakini ni matajiri wa kutosha kuliko hata wasomi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo mahali ambapo naendelea kuliombea liwepo gate ndiyo sehemu ambapo kuna barabara ambayo inaenda mpaka kwenye ile Bandari ya Karemii. Nchi ya Tanzania ilikuwa inapata changamoto kubwa sana…

T A A R I F A

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri wa Fedha, nimekuona.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwa ridhaa yako, naomba nimpe taarifa mchangiaji, Mbunge anayeongea ujengaji wa hoja wa kwake ni wa viwango vya Wabunge wazoefu sana. Kwa kweli ndiyo maana Jimbo la Momba walimpitisha kwa kishindo na waendelee kumchagua. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, kwa jinsi alivyojenga hoja, naomba nitoe taarifa kwamba Wizara pamoja na Mamlaka ya Mapato tutatembelea lile gate analolisema na tupate mfano ule aliousema ili tuweze kuzungukia na mageti mengine ili tuweze kutengeneza utaratibu wa kukusanya fedha na kuwawezesha wananachi wetu waweze kufanya shughuli zao kwa uangalifu. (Makofi/Vigelegele)

SPIKA: Mheshimiwa Condester ziara hiyo itafanyika, lakini kwa ruhusa ya Spika. Endelea Mheshimiwa. (Kicheko)

MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, nashindwa hata cha kusema, natamani hata kutoendelea kuchangia kwa sababu pale tukapojengewa gate ndani ya Jimbo la Momba hata siku nikifa nitahisi kwamba Mwenyezi Mungu kile alichonituma kuwatendea ndugu zangu wa Jimbo la Momba kitakuwa kimetia kwa sababu nitakuwa Mbunge wa kwanza kabisa kuwafanya ndugu zangu wa Jimbo la Momba kuishi kwenye mazingira ya biashara. Katika vijiji vyetu vyote 72 tulivyonavyo hatuna mji hata mmoja vyote ni kijijini hata mahali ambapo natokea, kwa hiyo, mtakuwa mmetusaidia sana kupata mjini ndani ya Jimbo la Momba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naendelea kuishukuru sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi na nisema kwa kauli hiyo nawashukuru sana wapiga kura wa Jimbo la Momba ambao kwa mara ya kwanza walimsimamisha Mbunge mwanamke na mdogo kwa umri na wakanipa heshima na wakaniamini. Kwa kauli yao walikuwa wakisema tunamtaka mtoto mdogo na mama ambaye tukimtuma anatumika. (Makofi/ Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia 205. (Makofi)