Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nkenge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FLORENT L. KYOMBO: Mheshimiwa Spika, nikushukuru kwa nafasi ya kuchangia katika Wizara yetu ya Fedha. Niungane na Wabunge wenzangu kuipongeza Wizara hii chini ya uongozi wa comrade Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha, lakini pia na ndugu yangu Mheshimiwa Masauni, Katibu Mkuu pamoja na viongozi mbalimbali wa Wizara hiyo ikiwa ni pamoja viongozi wa taasisi ndani ya Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Spika, mimi nitajikita katika Fungu 45 ambayo ni Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi chini ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ambapo Ofisi hiyo imepewa majukumu kupitia Ibara ya 143 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jukumu kubwa la Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ni kuhakikisha kwamba inafanya ukaguzi wa mapato na matumizi kama yalivyoidhinishwa na Bunge lakini pia kutoa taarifa Bungeni na hapo Bunge lako Tukufu linapata fursa ya kuweza kuitafsiri na kuishauri na kuisimamia Serikali yetu. Hayo yote yamekuwa yakifanyika kwa weledi mkubwa kupitia Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kwa nafasi ya pekee niendelee kuipongeza Serikali, nilikuwa napitia bajeti mbalimbali katika miaka iliyopita katika Ofisi ya CAG ambapo tumeona mwaka 2019/2020 Ofisi yetu iliweza kupewa bajeti yake kwa asilimia 109 ya ile bajeti ilikuwa imejiwekea. Hivyo tukiona ufanisi wa kazi wa Ofisi ya CAG kama inavyofanya tunajua ni kwamba Serikali imeweka mkono wake kuhakikisha kwamba Ofisi hiyo inafanya kazi vizuri.
Mheshimiwa Spika, lakini mwaka 2020/2021 bajeti ya CAG iliongezeka kidogo na tunaona mpaka tarehe 30 Aprili, Ofisi hiyo iliweza kupewa fedha na Serikali kwa asilimia 92. Naamini katika miezi michache iliyobaki hiyo bajeti yake itaweza kukamilika kwa asilimia 100.
Mheshimiwa Spika, katika eneo hili tunaona CAG anafanya kazi kwa kushirikiana na Bunge lako Tukufu kupitia Kamati za Kudumu ambazo zinafanya kazi na Ofisi ya CAG. Hivyo tuendelee kuipongeza Wizara ya Fedha kupitia Ofisi ya CAG kwa ushiriki mzuri pamoja na hizi Kamati ambazo zinafanya kazi pamoja na Ofisi hiyo za PAC, LAAC pamoja na Kamati ya Bajeti na Kamati zingine za kisekta kadri ambavyo wanakuwa wanaona ushirika unatakiwa. Kwa hiyo, tumeendelea pia kuimarishwa katika uweledi ili tuweze kutafsiri taarifa za CAG vizuri na kuweza kuleta mchango mzuri katika Bunge lako Tukufu ili Bunge lako sasa liweze kuishauri na kuisimamia Serikali yetu.
Mheshimiwa Spika, nikiangalia kwa undani Ofisi ya CAG, mtaji mkubwa ambao inauhitaji kuupata ni kupitia wataalam wake, hasa Wakaguzi wetu kuwa na weledi zaidi katika kufanya nao kazi. Hiyo inatokana na kujihuisha kutokana na taratibu zingine za Kimataifa ambazo sisi kama Tanzania ni waumini wa taratibu hizo. Tunao mfumo wa IFRS
- International Financial Reporting System ambao ndio tunaufuata, lakini tuna IPSAS ambao ni International Public Sector Accounting System ambao tunaufuata. Wataalam wetu hawa wakiwezeshwa vizuri, kila muda wakawa wanahuishwa vizuri katika mafunzo ya Kitaifa na Kimataifa, tunaamini tutapata taarifa ambazo ni nzuri, ambazo zimeenda kwa kina na kuweza kuishauri Serikali vizuri pamoja na kuisimamia.
Mheshimiwa Spika, nikiangalia katika bajeti ya Fungu 45 katika suala la kuweza kuwa-equip Wakaguzi wetu waweze kusimama vizuri kwa kusimamia sheria zetu za nchi yetu, lakini pia na standards za Kimataifa, sioni kama tuna nia ya dhati ya kuweza kuwafanya Wakaguzi wetu, pamoja na ueledi walionao leo, pamoja na uzoefu wa kazi walionao, kuendelea kupata elimu zaidi na kuendelea na standards za Kimataifa ambazo zinabadilika baada ya muda mfupi mfupi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikiangalia katika bajeti hii, naona katika sehemu zote nimepitia katika Idara mbalimbali za Ofisi ya CAG, hakuna sehemu ambapo unaona wataalam wetu wanaenda kupata mafunzo hasa ya nje. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna maeneo madogo ambayo yameonesha kwamba, kuna mafunzo ya nje kupitia Idara ya Utawala, lakini ni fedha kidogo sana. Pia kuna huduma za kiufundi katika ukaguzi, zimewekwa fedha kidogo sana. Kwa hiyo, ukiangalia mabadiliko ya nchi yanavyokua, tunahitaji kuhakikisha kwamba, wataalam wetu au Wakaguzi wetu katika Ofisi ya CAG wanaendelea kupewa mafunzo ambayo yatawafanya wafanye kazi kwa weledi na hivyo kuweza kuleta taarifa ambazo ni nzuri katika Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikiangalia pia, CAG hawezi kufanya kazi peke yake anafanya kazi na Bunge lako Tukufu. Utaungana na mimi Bunge hili jipya la Kumi na Mbili lina asilimia 67 ya Wabunge wapya. Na asilimia hiyo 67 ndio Wabunge wameenda kwenye kamati ambazo zinafanya kazi na CAG. Kwa hiyo, nilikuwa nauona kama mwaka wa fedha 2021/2022 ni mwaka ambao Serikali ingejikita kuongeza bajeti kule kwa CAG kuweza kuwa-equip Wakaguzi wetu, lakini kuweza kuwapa mafunzo vizuri Wajumbe wa Kamati ambazo zinafanya kazi na CAG, ili sasa baadaye tuendelee kupata matunda mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia katika maeneo hayo, hakuna kinachoonyesha kwamba, kuna nia ya dhati kuhakikisha kwamba, Wakaguzi wetu pamoja na Wabunge ambao wanahitaji kukaa na kutafsiri taarifa za CAG ili ziweze kutusaidia katika kufuatilia miradi ya maendeleo, katika kuangalia hesabu za Serikali, haipo. Kwa hiyo, pia mama yetu Rais wetu mpendwa, mama Samia Suluhu Hassan, amemwelekeza CAG aendelee kupanua wigo wa kuweza kufanya ukaguzi. Hata hivyo, ukiangalia bajeti aliyopewa mwaka, 2021/2022 haionyeshi nia hiyo ya dhati. Mwaka jana alipewa bajeti ya bilioni 80, lakini mwaka huu imeongezwa ni bilioni 80.9. Sasa hata maelekezo ya Mkuu wa Nchi hatuyaoni yaki-reflect katika bajeti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe kitu cha kwanza, Ofisi ya CAG iongezewe fedha, lakini ofisi hii iendelee kuongezewa fedha kwa ajili ya wataalam wetu kuendelea kujifunza mafunzo ya ndani lakini pia na mafunzo ya nje. Kama ni suala la hali ya kidunia ya corona, tunashukuru Serikali yetu ya Awamu ya Tano, iliweza kutupa mafunzo mazuri na Serikali yetu Awamu ya Sita inaendeleza. Maana yake tunatakiwa kuendelea kuishi na huo ugonjwa na ndio maana hata Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ameunda Tume nzuri ya Kudhibiti Corona imekuja na maoni, wale ambao wanaenda kufanya kazi watachanjwa na kazi ziendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hakuna kizuizi ambazo kitafanya Wakaguzi wetu washindwe kwenda kupata mafunzo kwa ajili ya kuweza kutoa ushauri mzuri. Hakuna mafunzo ambayo yatazuiliwa kwa Waheshimiwa Wabunge wa Kamati zinazohusika, washindwe kwenda kupata mafunzo kwa sababu, ya kisingizio cha Corona. Corona tutaishi nayo na ni sehemu ya maisha yetu.
Mheshimiwa Spika, nikiangalia katika majukumu makubwa ya Ofisi ya CAG imejiwekea jukumu ambalo ni la msingi ambao ni kutoa mafunzo kwa Kamati zote ambazo inafanya nazo kazi ambazo ni Kamati ambazo ziko chini ya ofisi yako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika mafunzo hayo ni kufundisha Kamati hizo pia, kwa ajili ya kufuatilia miradi ya maendeleo. Kwa hiyo, katika eneo hilo likiweza kuboreshwa vizuri, basi tunaamini kazi ya CAG itaweza kufanyika kwa weledi na wanaokuwakilisha katika Kamati kwa niaba yako ili kuleta maoni yao hapa, basi watakuwa wanafanya kazi kwa weledi na tunaamini sasa nchi yetu itasonga mbele kwa kuwa inasimamia fedha ambazo zinaidhinishwa, inasimamia fedha ambazo zinakusanywa na inasimamia fedha ambazo zinatumika katika taasisi zetu mbalimbali, katika halmashauri zetu, mashirika pamoja na taasisi nyingine za Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelee kwa kusema kwamba, nikiangalia katika maeneo mengine, fedha iliyokuwa imetengwa ya mafunzo katika kipindi kilichopita, sasa hivi hata mafunzo ya ndani kwa CAG imepungua. Kwa hiyo, maana yake hatuoni nia ya dhati ya wataalam wetu ndani ya Ofisi ya CAG kuweza kupata mafunzo hayo.
Mheshimiwa Spika, vilevile nikiangalia katika kitengo cha uratibu wa shughuli za Bunge ambacho kinatuhusu sisi katika kupata mafunzo, nimeona katika kasma 22010 imewekwa bajeti kidogo ya mafunzo ya ndani ya Kamati zako, lakini hakuna kasma yoyote ambayo inahitaji Wabunge waende ku-share mawazo na usimamizi kama Kamati hizo nchi za nje. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niendelee kusisitiza suala hili ni la msingi na naliongelea kwa nia ya dhati sio kwa sababu, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PAC, lakini ni kwa sababu ya nia ya dhati kwamba, Wakaguzi wetu wapate mafunzo, Kamati zinazohusika zipate mafunzo ili tuweze sasa kuishauri Serikali vizuri na malengo mahususi ya nchi yetu yaweze kufikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi na naunga mkono hoja. (Makofi)