Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Fedha. Wizara ya Fedha na jukumu la kusimamia uchumi wa nchi, lakini ina sera mahususi kwa mambo mengi kama yalivyoorodheshwa katika instrument yake na mojawapo ikiwa ni kuweka mkakati wa kusimamia utekelezaji wa kupunguza umaskini.

Mheshimiwa Spika, katika suala zima la ukusanyaji wa mapato kwa maana ya zoezi zima la ulipaji wa kodi, naendelea kuishauri Wizara kuweka mazingira mazuri, rafiki, kodi zinazolipika, bila shaka na kwa imani kubwa wafanya biashara wote watalipa kodi kwa amani kabisa, bila kuwepo na kusukumana, kuwekeana kodi kubwa kubwa, kupelekeana task force zinazoumiza wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiamini kupitia makosa yaliyofanyika huko nyuma ya kupeleka task force, kuongezea watu kodi, kulazimisha watu kulipa kodi wakati alishalipa kodi, tuna imani kabisa kupitia Rais mama Samia haya mambo hayatajirudia na wafanyabiashara watafanya biashara zao katika mazingira mazuri na rafiki na watapenda. Kwa sababu, huko nyuma ilikuwa ikifikia kwamba, mfanyabiashara akimwona afisa wa TRA anaenda, ni sawa sawa na amemwona simba mlangoni kwake. Sasa tutoke huko iwe mfanyabiashara akimwona afisa wa TRA, awe anamfurahia na kumkaribisha na kama ni kuhakiki kodi, kama ni masuala ya kodi, yanazungumzika katika namna rafiki na namna ambayo itamwezesha mfanyabiashara awe na amani pale ambapo anafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ni sambamba na kusema kwamba, wote tunawajibika kulipa kodi ile ambayo tunapaswa kulipa. Baada ya utangulizi huo, napenda kuiuliza Wizara, hivi wafanyabiashara wa maduka ya kubadilishia fedha waliwakosa kitu gani kwa nchi hii? Niliwahi kuongea katika Ofisi ya Waziri Mkuu jambo hili hili na nataka leo nilirudie kwa sababu ni Wizara husika. Waliwapora wafanyabiashara wa maduka ya kubadilishia fedha katika Mkoa wa Arusha, Mkoa wa Kilimanjaro na Dar es Salaam. Sina hakika kama waliwapa sababu sahihi ya kwa nini walipeleka task force na nguvu kubwa kuwanyang’anya fedha wafanyabiashara hawa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukisikia kwa pembeni, ni kwamba, walikuwa hawakulipa kodi. Hivi inawezekanaje, pamoja na machinery zote walizonazo mtu anafanya biashara hii kwa miaka kadhaa, halafu inatokea tu kwamba leo hawajalipa kodi. Haya, kuna hisia nyingine kwamba, maduka haya yalikuwa yanatumika kupitishia fedha haramu, sasa kama yalikuwa yanatumika kupitishia fedha haramu, je, ni kweli wafanyabiashara wote wa nchi hii wa maduka ya fedha walikuwa wanatumika kupitisha fedha haramu? Kama sivyo, kwa nini waliwaadhibu wote? Kama ndivyo, maana yake kuna upungufu mahali na kama kuna udhaifu na upungufu mahali, ama ni wa kisera, ni wa kisheria, wamechukua hatua gani kwa hicho kilichosababisha kupelekea hapo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nataka Mheshimiwa Waziri atuambie baada ya kuhitimisha hoja hii, wale wafanyabiashara ambao walikuwa innocent, ambao walikuwa na leseni za biashara, ambao walikuwa wanalipa kodi, ambao wamewanyang’anya fedha zao, nini hatima ya wafanyabiashara hawa ambao walikuwa wanaendesha biashara hii kihalali kabisa? Tunataka kufahamu wafanyabiashara hawa fedha zao ziko wapi na watawarejeshea lini? Halafu, wapo wengine ambao waliwalazimisha mfano, wamechukua labda bilioni moja, mnalazimisha kwamba, alichukua labda milioni 600 unamlazimisha asaini fedha ambayo haikuchukuliwa kihalali. Hii sio sawa, tunataka kupata majibu ya hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama sera ya Serikali inasema ni kupunguza umaskini, hivi wanapunguza umaskini au wanaongeza umaskini! Naona wanaongeza umaskini. Kwa hiyo, hili halikubaliki, lazima wafanye marekebisho na lazima wakutane na hawa watu. Namshauri Mheshimiwa Waziri akutane na hao wafanyabiashara, waongee nao, wasemezane nao, hawa watu wajue hatima ya fedha zao ambazo wamezipata kihalali ni nini ili wajue wanafanya nini.

Mheshimiwa Spika, napenda pia, kufahamu, wame- cease hii biashara ya maduka ya kubadilishia fedha, lakini wanayarejesha. Wanayarejesha kwa masharti magumu sana, wanataka kurejesha kwa kusema mtu ambaye anataka sasa kuendesha maduka ya kubadilishia fedha, awe na mtaji wa bilioni moja, hii inawezekana kweli? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndio maana nasema hii sera waliyojiwekea ya kusema wanataka kupunguza umasikini, hivi wanapunguza ndio wanauongeza? Hizi biashara za kubadilishia fedha yalikuwa ni maduka hasa mipakani kwetu Namanga, Holili, Sirari, Tunduma na maeneo yote ya mipakani, yalikuwa ni maduka ambayo kwa namna moja au nyingine yalikuwa yanatoa ajira pia kwa vijana wetu. Vijana walikuwa wana maduka madogo wanabadilisha fedha twenty-four, seven, leo unamwambia awe na mtaji wa bilioni moja. Sasa nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri, ni busara hii ya kupunguza umaskini au ni busara ya kuongeza umaskini? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama haitoshi wanaweka masharti kwamba, mtaji uwe bilioni moja, halafu uwe na Mkurugenzi, wewe ambaye unataka kuanzisha duka hili la Bureau de Change, uwe na Marketing Manager, uwe na Internal Auditor, haya ni mambo ambayo hayawezekani. Hivi kwa nini, tusiiache hii biashara huria, watu wafanye lakini kuwepo na control measures, ambayo itasimamiwa na BOT, kuhakikisha kama kuna harufu ya fedha haramu, kuwepo na hiyo measures ambayo itadhibiti jambo hili. Sio kwamba, tunawakatisha watu wasifanye biashara hizi, tunataka tu eti benki ndio ifanye na tunajua benki ikifika saa 9.00, saa 10.00 wamefunga. Sasa ikifika saa 9.00, saa 10.00 amefunga, mtu ambaye anataka kwenda kubadilisha fedha anaenda kupata wapi hii huduma? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaongea habari ya kukuza utalii, tunatambua sekta ya utalii, mtalii anashuka Airport na KLM ya saa 6.00 usiku pale Kilimanjaro. Anataka kesho yake kwenda porini, safari, anataka kubadilisha fedha, atasubiri hiyo benki kesho yake ifunguliwe saa 2.00 ndio akabadilishe fedha ndio aweze kuendelea na utaratibu mwingine? Kwa hiyo, nafikiri iko haja ya kulitazama na kuachia biashara hii huru, watu waendelee kufanya hii biashara, lakini kwa kudhibiti ule upungufu uliojitokeza, kwa kuweka mikakati thabiti ambayo inaweza ikamfanya kila mtu akaingia kwenye biashara hii, tukaendelea kukuza ajira, tukaendelea kuhakikisha tunawapatia vijana wetu ajira na mazingira rafiki zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nichangie pia, suala la wakandarasi. Wabunge wengi wamechangia kwa hiyo, niongezee kwa kusema kwamba, kwa kweli wakandarasi wanaodai fedha Serikali walipwe. Hawa wakandarasi wengine wameenda kuchukua fedha benki, wanadaiwa na mabenki, wamefilisika leo kwa sababu Serikali haijawalipa kwa wakati. Wanafanya uhakiki, uhakiki gani wa miaka mitano, sita jamani, uhakiki gani ambao hauishi! Haya ni mambo ya kushangaza sana! Ndio maana nikasema, narudi kwenye ile ile sera ya Serikali. Hivi unampa mkandarasi kazi, unataka umnyanyue kiuchumi, hapo hapo unamkandamiza, humlipi, maana yake unampa umaskini, humwongezei faida yoyote, husaidii uchumi wa mmoja mmoja kuweza kukua. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa, Mheshimiwa Esther Matiko.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nataka nimpe taarifa, Mheshimiwa Paresso kwamba sio tu kwamba wanafilisika, bali hata hao wakandarasi unajua wanakuwa wana watu wamewaajiri. Kwa hiyo, inabidi wawapunguze kutoka makazini, lakini wengine kwa sababu, wana majumba na vitu vingine ambavyo wameviweka kama guarantee kule benki wakishachukuliwa wanaamua kujiua. Kwa hiyo, kuna Watanzania wengi sana ambao wamepoteza maisha, kwa sababu ya madeni ambayo yamekaa zaidi ya miaka minne mpaka mitano, Serikali ikisema inahakiki hayo madeni. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Paresso unapokea hiyo taarifa?

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, naipokea hiyo taarifa. Ni kweli kabisa, wakandarasi hao wako wengine wameweka nyumba zao dhamana zinachukuliwa, zinapigwa mnada. Wengine wanakata tamaa hawaoni matarajio na matumaini yoyote ya fedha zake kulipwa anaamua kujiua. Haya mambo yapo, tunayakuta kwenye jamii, tunakutana na hao watu. Ni wakati sasa, Wizara walichukulie jambo hili kwa uzito na kwa umuhimu wa kipekee kuhakikisha kwamba, wakandarasi wote wanalipwa fedha. Wanajua mimi sio Mchumi, lakini impact tu inaonekana, ukiwalipa wakandarasi maana yake pia, unarudisha mzunguko wa fedha kwenye jamii. Tunataka tuone hilo lifanyike na jamii iweze kupata hiyo impact ya wakandarasi hao kulipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema, Wizara ni vyema sasa na wale wafanyabiashara ambao walipelekewa task force, wakaambiwa walipe sijui malimbikizo ya kodi ya miaka sijui mingapi iliyopita, narudia kusema na kuishauri Wizara na Serikali kwa ujumla kwamba, hao wafanyabiashara, tunaomba sana hizo task force zisichukuliwe kama sehemu ya kodi, waachane na hiyo biashara, wapewe comfort ya kufanya biashara. Kama kuna haya madeni wanayodaiwa huko nyuma, nafikiri tunafungua ukurasa mpya wa kuwapa wafanyabiashara mazingira mazuri na rafiki ya kufanya kazi, lakini na wao wakijua wana wajibu wa kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. (Makofi)