Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Dr. Ashatu Kachwamba Kijaji

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Kondoa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema aliyetujaalia neema ya uhai na jioni ya leo tunahitimisha mchakato wa Wizara ya Viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nikushukuru wewe mwenyewe kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia machache katika Wizara hii. Tatu naomba niseme naunga mkono hoja asilimia mia moja hotuba iliyoletwa na bajeti iliyowekwa mezani na Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Naomba nikupe pongezi sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yako nzuri ambayo uliiwasilisha vilivyo, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme masuala machache ambayo yameonekena kwamba yanatakiwa kusemewa na Wizara yangu ya Fedha.
Sehemu ya kwanza kabisa naomba nianze na maoni ya Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira alipopendekeza kwamba Serikali itoe fedha zinazoidhinishwa na Bunge kwa wakati ili kupelekea utekelezaji wa bajeti zetu katika Wizara zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inakubaliana na wazo hili, inakubaliana kabisa na mapendekezo haya na tunaona umuhimu kama Serikali wa kutoa pesa hizi kwa muda muafaka pale inapohitajika. Pia naomba nilikumbushe Bunge lako Tukufu kwamba utoaji wa fedha za bajeti unategemea upatikanaji wa mapato kwa mwaka husika, hivyo naomba pia tukubali kwamba sote na tunafahamu ni mashahidi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ya Chama cha Mapinduzi tumedhamiria vilivyo kukusanya mapato, kuziba mianya yote na sote tunaona sasa tunaweza kukusanya zaidi ya asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti katika hilo, Serikali ya Awamu ya Tano pia imedhamiria kwamba Tanzania ya viwanda inawezekana na tunaanza mwaka huu na tumedhamiria kuanza kweli na ndiyo maana tumekuja na asilimia 40 kwa ajili ya bajeti ya maendeleo. Tunaomba sana kama Serikali mtuunge mkono bajeti zetu, tupitishe, tumedhamiria na tumeonesha kwamba tunaweza kukusanya na sasa tunazipeleka pesa katika maendeleo asilimia 40. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja namba mbili ilikuwa ni Serikali na mamlaka zake ipunguze utitiri wa tozo na ushuru ikiwemo kuziondoa zile zisizo na tija. Mapendekezo haya pia tumeyapokea, tumeanza kuyafanyia kazi na kama sote sisi ni mashahidi tulimsikia Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema tozo zisizo na tija zote zitaondolewa. Naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu kwamba kikosi kazi kiko kazini na kikao cha kwanza cha kushughulikia tozo hizi zisizo na tija kinafanyika kesho na tuna uhakika mpaka tunaleta bajeti ya Wizara ya Fedha hapa tutakuwa tumeainisha tozo zote zisizo na tija na zote zitafutwa ili tuweze kwenda kwa mwendo unaohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninawaomba tu Waheshimiwa Wabunge mtuunge mkono pale ambapo tutaleta mapendekezo yetu na muweze kutushauri ili tuweze kwenda mbele kwa ajili ya maendeleo ya watu wetu, maendeleo ya Watanzania na Tanzania kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya tatu ilikuwa imetoka kwa Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani ambaye aliomba majibu ya kina yatolewe kuhusu ukomo wa bajeti. Akaenda mbele zaidi kuita kwamba uhuni wa Waziri wa Fedha katika kutenga ukomo wa bajeti. Naomba niseme hakuna uhuni hapa, kilicholetwa kama ukomo wa bajeti hakijatoka Wizara ya Fedha peke yake, haya ni maamuzi ya Serikali kwamba asilimia 40 sasa inakwenda kwenye maendeleo na asilimia 60 inakwenda kwenye matumizi ya kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilikumbushe Bunge lako Tukufu kwamba ukomo wa bajeti hautolewi na Wizara ya Fedha, unapita katika vikao maalum, tunaanza na vikao vya wataalam, nimewasikia Wabunge wakisema kwamba Mawaziri tunafika pale na tunawadharau wataalam, hapana. Kikao cha kwanza kabisa cha jambo lolote huwa ni wataalam wetu, wanatuletea mapendekezo na mwisho Baraza la Mawaziri linapitisha ili kuleta hapa. Kwa hiyo, hata ukomo wa bajeti haukuwa uhuni, ila ilikuwa ni maamuzi sahihi kabisa na lengo sahihi kabisa la Serikali yetu ya Awamu ya Tano kwamba sasa tunahitaji kuiona Tanzania ikikimbia, Tanzania ya viwanda inawezekana chini ya Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja namba nne pia ilitoka kwa Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwamba tupitie upya utaratibu wa kufanya uplifting ya kodi, naomba niseme pia katika tatizo hili, siyo tatizo in such au naweza kuita ni tatizo kwa sababu ya wafanyabiashara au sisi final consumers. Sisi ndiyo tunapelekea kuwa na hii uplifting na mimi siiti ni uplifting kwa sababu tunakwenda kwa standard, tunakwenda kwa sheria, hatuendi tu bila kufikiri, ukadiriaji wa bidhaa zinazoingia nchini, tunafahamu unafanyika chini ya Kifungu cha 122 cha Sheria ya Forodha ya Afrika Mashariki. Hivyo tatizo hii linaonekana kwamba ni kubwa ni kwa sababu tu kama nilivyosema wafanyabiashara wengi au watumiaji wengi wa bidhaa za kutoka nje, huwa wanafanya under invoicing yaani wanapoleta pale hawasemi ukweli bidhaa hii imelipiwa kiasi gani kutoka kule ambako imetoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo sheria hii niliyoitaja haikutuacha hivi imetupa mwongozo, linapotokea tatizo kama hili sheria inaipa Mamlaka ya Mapato ya Tanzania uwezo sasa wa kuangalia kutoka kwa country of origin ya ile bidhaa, bidhaa ile inauzwa kaisi gani na pia tunaangalia data base ya bidhaa zinazolingana, zinazofanana na bidhaa hiyo ili tuweze kufanya ukadiriaji halisi wa dhamani ya bidhaa ambayo imeingia nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo naomba pia niwaombe Waheshimiwa Wabunge, kwa pamoja tushirikiane hii ni nchi yetu, tuipende nchi yetu, tunahitaji maendeleo siyo maendeleo kwa Chama cha Mapinduzi tu, ni maendeleo kwa ajili ya Taifa letu kwa ujumla na watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatutaweza kuendelea kama tusipoweza kulipa kodi husika, kodi ambayo inaendana na bidhaa tunazoingiza nchini, hivyo, kama Mamlaka ya Mapato tutaendelea kusimamia sheria hii, hatuwezi kuwaumiza wateja wetu lakini tunasimamia sheria na pale ambapo mteja anafikisha bidhaa yake, pale kwetu tunafanya uthaminishaji kwa sheria hii na analipa kodi anayostahiili kulipa, hatuna sababu ya kumuumiza mteja wetu katika jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia limeongelewa tatizo kwamba kumekuwa na vikwazo kwa wafanyabiashara kutoka Zanzibar kwamba bidhaa zao zinatozwa kodi mara mbili. Naomba nilisemee pia jambo hili. Hakuna kodi zinazotozwa mara mbili kwa bidhaa zinazoingia Zanzibar kuletwa Tanzania Bara, kama mtakumbuka Waheshimiwa Wabunge, nilijibu hapa mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba kinachofanyika ni ukadiriaji kwa sababu sheria inayotumika kule upande wa Zanzibar siyo sawa na mifumo tunayoitumia huku Bara, kwa hiyo kinachotokea hapa bidhaa inapoingia Zanzibar inakuwa haijathaminishwa kwa kiwango kile kinachotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo inapokuja huku hatutozi kodi mara mbili tunachokifanya sasa ni kuangalia ile tofauti ya kodi iliyotozwa kule thamani ya bidhaa ile Zanzibar na thamani ya bidhaa huku kwa hiyo tunachaji ule utofauti tu wa kodi ile ambayo haikuchajiwa na siyo kodi mara mbili. Serikali inawaangalia wafanyabiashara kutoka Zanzibar kwa jicho chanya kabisa, naomba mtuelewe Serikali ina nia njema na wafanyabiashara wake wa pande zote mbili za Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia iliongelewa tatizo la kwamba Serikali itoe temporary documents kwa magari yanayokuja Tanzania Bara kutoka Zanzibar. Hili pia napenda kulieleza Bunge lako Tukufu ni kwamba hatuna sababu ya kutoa tempoprary documents kwa magari yanayotoka Zanzibar kuja huku Bara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokifanya, magari yanayolipiwa ushuru wa dola ishirini siyo magari yanayotoka Zanzibar kuingia Tanzania Bara hapana. Ni magari yanayotoka nchi za jirani, nchi tunazopakana nazo kwamba watu wameingia nchini humu na magari yao wanataka kuyatumia na huwa tunawapa muda wa siku sitini, ndani ya muda wa siku sitini hiyo huwa wanalipa dola ishirini. Kwa magari yote yanayotoka Zanzibar kuingia humu nchini, kwa mfano Waheshimiwa Wabunge wamekuja na magari yao huku hakika huwa hawalipi hii dola 20, wanachotakiwa tu wao ni kueleza kwa Mamlaka ya Mapato kwamba ameingia nchini kwa muda upi atakaa hapa nchini, hivyo hakuna tozo yoyote anayotozwa mwenye gari anayetoka Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinacholalamikiwa kama nilivyosema mwanzo ni kwa gari zinazoingia huku moja kwa moja au zinazoingia huku kutoka Zanzibar kuja kuuzwa huku, kama nilivyosema mifumo yetu ya kodi haifanani kwa hiyo lazima tunafanya uthaminishaji upya kwa sababu hii ni gari inaingia sokoni kwa hiyo na pia kinacholipwa siyo kodi mara mbili kinacholipwa ni utofauti tu wa kodi ambayo ililipwa kule Tanzania Zanzibar na hatimaye inapoingia huku kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Raphael Japhary Michael pia aliongelea kuhusu tuiangalie upya tax regime kwa kupunguza cooperate tax na VAT kwa wafanyabiashara wa ndani, kwa sababu inapelekea compliance kuwa ni ndogo.
Naomba niseme kwamba kodi ya ongezeko la thamani ni kodi inayolipwa na mnunuzi wa bidhaa au huduma na wala siyo kwa mfanyabiashara, hivyo kodi hii wala haipelekei watu kutokulipa kodi au compliance kuwa ndogo hapana, kwa sababu mfanyabiashara ni agent tu wa kodi hii kwa Serikali. Fedha yake huwa inarudishwa kwake pale ambapo anakuwa amerejesha na amelipa kodi husika kule Serikalini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu cooperate tax, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, hutozwa kwa faida baada ya kuondoa gharama za uendeshaji kwa mujibu wa sharia, kimsingi pia naomba niseme kodi hii haiathiri gharama za uendeshaji wa kampuni, kwa sababu hii inakuwa ni ile faida ambayo mfanyabiashara ameweza ku-declare kwamba amepata faida ndipo anapolipa cooperate tax. Kwa hiyo, katika kodi hizi mbili pia hazizuii uwekezaji, wala hazisababishi compliance ya kulipa kodi kuwa ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho ambalo napenda kuliongelea jioni ya leo ilikuwa ni kutozwa kwa kodi ya VAT kwa transit goods. Jambo hili pia limeleta changamoto kubwa sana na naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba kwa mujibu wa Sheria ya VAT ya mwaka 2014, mizigo inayopita nchini kwenda nchi za jirani haitozwi kodi ya VAT, hivi haya malalamiko yanayoletwa kinachotozwa kodi ya VAT ni zile tunaita auxiliary services ni zile huduma za msaada kwa ajili ya bidhaa hii kuweza kufika kule nchini. Kwa mfano, tunapokuwa na ulinzi tunapokuwa na storage charges hizi ndizo zinazotozwa VAT na siyo mzigo ule wala transportation yake haitozwi kodi hii. Hivyo naomba pia Waheshimiwa Wabunge, tuwaelekeze wafanyabiashara wetu, tuwaelekeze ma-clearing agency kwamba mizigo ya transit haitozwi kodi ya VAT hapa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa nafasi hii.