Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Vwawa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi ili niweze kutoa mchango wangu. Nitajitahidi kutoa mchango kwenye maeneo karibu manne. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri Katibu Mkuu na timu nzima kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiifanya katika kusimamia hii Wizara.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, naelewa kwamba Wizara hii ina majukumu mengi ambayo imepewa, lakini nadhani majukumu haya yamegawanywa kwenye makundi mawili; kuna suala la mipango, kuna masuala ya usimamizi wa fedha. Kwangu mimi napenda nishauri, Mheshimiwa Waziri wewe ni mtaalamu, hizi nafasi; mipango na fedha, usipoziangalia vizuri unaweza ukajikuta unatumia muda mwingi kwa asilimia 99 kwenye masuala ya usimamizi wa fedha, halafu ukasahau mipango. Ndiyo maana hata ukiangalia jina lako linavyoitwa, ni Waziri wa Fedha na Mipango. Wengine wanashauri ingekuwa Waziri wa Mipango na Fedha. Kwa sababu mipango ndiyo inayo-drive kuleta fedha. Sasa hilo ni la muhimu sana ukalitilia mkazo unapotekeleza majukumu yako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naelewa tutakuwa na siku karibu saba za kujadili mipango na fedha na ukusanyaji wa mapato. Kwa hiyo, sitalisemea sana, bali nitazungumza maeneo mengine yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, wengi wamemzungumzia CAG na kazi zake na sina haja ya kurudia, lakini umuhimu wa CAG ni mkubwa mno. CAG ndiye anafanya kazi kwa niaba ya Bunge, ndiye anayeenda kuangalia bajeti tulizozipitisha kama kweli Serikali na taasisi zimetekeleza kama zilivyopitishwa na Bunge; ndiye anaenda kufanya ufuatiliaji kwa niaba ya Bunge, anakuja kutuletea ripoti; na kwa vigezo vya Kimataifa CAG anatakiwa awe huru, awe na rasilimali za kutosha, aweze kufanya kazi yake vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunalo tatizo. Ukiangalia fedha anazopewa CAG kwa ajili ya kwenda kutekeleza majukumu ya kikatiba, yale ya kudhibiti na kukagua mahesabu ya Serikali; Idara zote, Wizara zote, Wakala zote, Balozi zote, nakadhalika, fedha ni kidogo sana. Hii nafikiri tuangalie mbele huko tunakokwenda namna tutakavyomwezesha CAG wetu aweze kupata rasilimali za kutosha ili akatekeleze majukumu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hivi ukiangalia kwenye ripoti aliyoitoa, amesema amekagua mashirika 165, lakini mashirika hayako 165, yako zaidi ya hayo. Balozi hakukagua. Zote hazikukaguliwa na mambo mengine. Kwa hiyo, hatuwezi kuwa na uhakika juu ya matumizi ya fedha za Umma katika maeneo yote hayo. Kwa hiyo, ni vizuri tukamwezesha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hilo lazima tumuandalie, tumpe uwezo wa rasilimali fedha na watumishi, hana watumishi wa kutosha huyu CAG ana watumishi wachache na watumishi wenyewe wengine hawana uzoefu wa kutosha, wengine hawajui hata zile kazi, ukiangalia kwenye bajeti hata ya CAG ya kuwajengea uwezo bajeti ni kidogo kwa hiyo, hata uwezo hawajengei, anawatuma kwenda kukagua wanaanza kuuliza huku wanamuuliza ndiyo waanze, ni kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nafikiri hili suala tuliangalie vizuri ili CAG, apewe rasilimali za kutosha lakini pia watumishi wa kutosha wenye uweledi akawajengee uwezo wafanye kazi ya kitaaluma ili heshima ya Bunge letu iwe kubwa, heshima ya nchi yetu iweze kupatikana hapo ndipo Utawala Bora utakuwa umeimarika nilidhani hiyo ni kitu muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika kuwajengea huwezo unajua, anapowajengea CAG uwezo na Wabunge pia tutajengewa uwezo na ndiyo maana tunasema akijua kule na sisi atujengee uwezo ili atuambie anapo tuambia kule tuwe na uwezo sasa kujua kipi muhimu kipi siyo muhimu, kipi tuchukue hatua, kipi Bunge lifanye nini? Hiyo, itatusaidia sana katika kutekeleza majukumu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la tatu ambalo nilitaka kuchangia ni kwenye upande wa utoaji wa fedha za Serikali, fedha za maendeleo, fedha za maendeleo imekuwa ni kigezo na bahati nzuri umeshalisemea, hatuwezi tukawa tunapanga kila siku, tunapanga mipango mikubwa tunapitisha mabajeti makubwa ikija mwisho wa mwaka utekelezaji fedha zilizoenda sifuri, zilizoenda asilimia 10, zilizoenda asilimia 5. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa kwa namna hiyo tutamuajibikashaje yule anayehusika na hiyo Taasisi au Wizara kwamba hakutekeleza hayo majukumu. Kwa hiyo, hili nadhani tutalijadili vizuri sana tutakapokuwa kwenye Bajeti Kuu na mipango tutakavyoliangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la nne ninalotaka kusema ni kuhusu usimamizi wa Fedha za Umma, usimamizi wa fedha za umma nitachangia kwenye maeneo mawili; la kwanza ni mifumo ambayo imetayarishwa, mifumo ambayo inayotakiwa kutayarishwa na Serikali kwa ajili ya kusimamia fedha za umma. Katika mifumo ambayo ipo sasa hivi dunia nzia inatumia teknolojia watu wamebuni mifumo mingi sana. Bahati mbaya kwa nchi yetu baadhi ya mifumo imekuwa ni mifumo inayotengenezwa kwa ajili ya kupiga Fedha za Umma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nadhani ni wajibu wa Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha inakuja na mifumo itakayokuwa inaweza kusomana, itakayokuwa na uwezo wa kusimamia fedha za umma vizuri, haiwezekani mfumo huu hausomani na wa huku wala useme hivi mara useme hivi, hilo ni tatizo kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini eneo la pili katika hilo la usimamizi wa fedha za umma tunaye mkaguzi wa ndani Internal Auditor General, Internal Auditor General kwa mujibu wa taratibu wa fedha, huyu ndiyo msimamizi wa kuhakikisha anakagua mifumo yote iliyoko kwenye taasisi kama inafanya kazi sawa sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, najua hata sisi Wabunge wengi hatuelewi tunafikiri CAG anaenda ku-discover fraud, anaenda kugundua wizi au ubadhilifu siyo kazi ya msingi wa CAG, siyo kazi yake. Kazi ya kugundua kama kuna ubadhilifu yaani kuna frauds kuna misappropriation, kuna errors in the books of account, mifumo haifanyi kazi ni kazi ya mfumo wa ndani ambayo ni ya Internal auditor. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa huyu internal auditor akiwa na uwezo wa kufanya kazi yake vizuri mifumo ikakaka vizuri CAG anapoenda pale kazi yake inakuwa ni nyepesi anaweza akatoa hata hati kwa kuangalita tu mifumo iliyoko pale akaridhika na kazi iliyofanyika. Kwa hiyo, ni vizuri huyu Internal auditor general akapewa uhuru…
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, mumsikilize vizuri Mheshimiwa anavyotofautisha hivi vitu kwa sababu tuko baadhi yetu huwa tunachanganyaga hivi vitu, tunafikiri halmashauri ikipata hati sijui inamashaka au nini kwamba kuna wizi ndiyo anafafanua vizuri hakuna mwingine wizi wowote ni mifumo na mahesabu yalivyowekwa kihasibu nakadhalika, endelea Mheshimiwa kuweka vizuri. (Makofi)
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ahsante sana kwa ufafanuzi kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge ninachotaka kusema ni kwamba huyu mfumo wa ndani huyu Internal auditor general ndiyo muhimu kuliko hata CAG, ni muhimu mno kwa sababu yeye ndiye ataangalia kama kuna wizi, ataangalia kama kuna makosa, ataangalia mifumo kama inafanya kazi, ataangalia kama inasomana, ataangalia namna ya ku-share taarifa na kadhalika, hii ndiyo kazi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini bahati mbaya sana hatujamuwezesha vya kutosha hana watumishi wa kutosha na ukienda wale Internal auditor walioko kwenye halmashauri, walioko kwenye taasisi they are not independent hawaripoti kwake straight wanaripoti kwa wale watarajiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nataka niwaeleze danger iliyopo, huyu Internal auditor ameajiriwa yuko anaripoti kwa mkurugenzi akikuta mkurugenzi ametumia fedha vibaya na yeye kazi ya Internal auditor ni kumshauri mkurugenzi hata mshauri kwamba mzee hapa umekula au anafanyaje? Na huyo accounting officer anatuchua hatua? Hawezi hili ndiyo maana tukasema iazishwe office ya Internal auditor general na wale wakaguzi wote wa taasisi waende wakaripoti huko wafanye hiyo kazi kwa hiyo, nadhani ni kitu muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hivi mifumo yetu ni mibaya ukiangalia mahesabu yetu yanayofungwa kwenye halmashauri, kwenye taasisi hayakaa vizuri na kwanini hayajakaa vizuri? Kwa sababu watu hawajaelewa na bahati mbaya hatujaweka fungu la kuweza kuwajengea uwezo wahasibu wetu huko. Sasa hivi watu nafikiri ukimpeleka mhasibu kwenda kusoma ni kama unatupa fedha sasa matokeo yake…
SPIKA: Mheshimiwa nakupa dakika tano ufafanue hili jambo. (Makofi)
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana ninachotaka kusema wahasibu tunapoona taasisi fulani haijafunga mahesabu yake sawa sawa mahesabu yamekaa vizuri kwa kawaida siyo kazi ya mkurugenzi mkuu ni kazi ya wale wauhasibu, wasimamizi wa fedha wale. Sasa wale usipowajengea uwezo wasipojua International Account Standard wasipozijua, wasipojua International Auditing Standard watafanyaje kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana mahesabu yetu ukiangalia yamekaa kiajabuajabu kiukweli kuna wengine wamekuta huko yuko huko anasema ninauzoefu sana kwenye uhasibu, anasema unamiaka mingapi? Anasema anamiaka 25 kumbe alikuwa anaandika voucher tu miaka 25. Sasa miaka 25 alafu unauzoefu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika sasa ukimpa kazi nenda kafunge mahesabu ni changamoto kubwa na Wizara ya Fedha, Mheshimiwa Waziri wahasibu wote wako chini yako, wahasabu wote nchi nzima wako chini ya Wizara ya Fedha, mwenye uwezo wa kuwajengea uwezo ni wewe, mwenye vyuo, vyuo vya Uhasibu viko chini yako. Sasa kinachoshindikana kuwajengea uwezo ili wafanye kazi nzuri, ili waitekeleze majukumu yao vizuri waitendee vema Taifa hili ni nini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna IFM pale, una Tanzania Institute of Tanzania (TIA) unakile cha Arusha una vyuo vyote vya uhasibu viko chini yako. Mheshimiwa Waziri hebu wajengee uwezo hawa muwafundishe wajuwe hivi vitu wakafanye kazi na sisi tunakuwa tumefanya kazi vizuri naamini tunakuwa tumekwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumeona Mashirika mengi hayakushindwa kufunga mahesabu ni tatizo la mashirika yenyewe, wale viongozi wakuu ni tatizo la wale ambao wamekuwa charged na haya majukumu, unakuta kuna Director wa Financial, kuna Chief Accountant anaitwa CPA, mwambie afunge vitabu my friend, mwambie tu IPSAS wewe kamuulize tu IPSAS ina standard ngapi? Anakwambia ziko 42 ume-comply na zipi, anasema ngoja mpaka nikaingie kwenye mtandao, kama unajua utaingia kwenye mtandao vipi? Ukienda IFRS ina standard kibao, audit ina standard kibao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilitaka kusisitiza kwamba tukiwajengea uwezo hawa suala la utawala bora na usimamizi wa fedha za umma utaimarika vizuri sana na utakaa vizuri na hiyo itasaidia.
Mheshimiwa Spika, la mwisho kama utaniruhusu ili nitalilema vizuri nitakapokwenda kwenye bajeti kwa sababu tunasema sasa hivi imefika mahali hizi Serikali za Mitaa zenye uwezo zinaweza zikafikiriwa kupewa zile tunaita dhamana treasury bonds zile municipal bond wakipewa zile kama wanakitu cha msingi cha kwenda kuzalisha na hawana fedha wanaweza kuruhusiwa kupewa, wakapewa dhamana ya miaka 10, miaka 15 wakakopa, wakafanya hicho na watakuwa na uwezo wa kujenga mambo mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana na naunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)