Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee kabisa nishukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia mchana huu kwa lengo mahususi kabisa la kutaka kuishauri Wizara na Serikali katika maboresho ya bajeti zilizowasilishwa pamoja na bajeti hii tunayoijadili wakati huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee pia nipongeze maamuzi mbalimbali yanayofanywa na mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu, kwa ajili ya manufaa ya Taifa hili. Na moja kubwa kabisa ni hili suala la Liganga na Mchuchuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa Mjumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara kwa muda mrefu sasa. Awamu iliyopita, kipindi changu cha mwisho, nilikuwa Mjumbe hapo na sasa hivi pia nimeendelea kuwa Mjumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Liganga na Mchuchuma limekuwa likirudi mara nyingi sana, lakini hata hivyo, tulivyojaribu kuwashauri Serikali na wenyewe tulijitahidi sana kuongea humu ndani tukionesha kwamba Liganga na Mchuchuma ni sehemu ambayo inaweza ikatuletea mapato makubwa sana kama nchi. Lakini mama sasa ameamua kuwa jasiri na anataka mradi huu utekelezwe, na tunaomba sana ukatekelezwe kadri ya alivyosema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwakumbushe pia kwamba machimbo haya na miradi hii ya madini mikubwa ndiyo yenye uwezo mkubwa sana wa kuleta mapato mazuri kwenye nchi yetu. Nikumbushe pia kwamba mama kafanya maamuzi mengine magumu sana kwenye Mradi wa Mbunyu uliopo kwenye Jimbo la Ndanda, kwenye Kata ya Chiwata, kwa sababu utekelezaji wake nao umekuwa wa kusuasua lakini utanufaisha Mkoa wa Mtwara, Wilaya ya Newala Vijijini, Wilaya ya Ruangwa pamoja na Wilaya ya Masasi. Kwa hiyo tunaomba kabisa na wenyewe wakauangalie waone namna ya kutaka kwenda kuutekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu pia wakati wa utekelezaji wa Mradi wa Liganga na Mchuchuma kutakuwa na reli pale inayotoka Liganga kuelekea Mtwara kwa maana ya bandarini. Kwa hiyo, matumizi ya bandari yatakwenda kufanyika. Lakini sasa madini hayo ya mbunyu (graphite) yatakayokuwa yanatoka Chiwata, ni rahisi kuyashusha pale Kata ya Chigugu nayo yakapakiwa kwenye reli hii yakaenda bandarini Mtwara na kuweza kusafirishwa kwa ajili ya ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kufanikiwa kutokana na namna ambavyo Mheshimiwa Dkt. Mwigulu ameleta hii bajeti yetu, na nimuombe Mheshimiwa hapa asiingie kwenye mtego ambao Mawaziri wengine labda waliopita walikuwa wanaingia. Mara nyingi tumekuwa na utaratibu wa kupunguza ama kuongeza kodi, lakini ni mara chache sana tumekuwa tuna utaratibu wa kufikiria kuhusu vyanzo vipya vya mapato kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo moja nilikuwa nalifikiria tu peke yangu, kwamba tuna haja ya kuishauri Serikali ili iweze kupata vyanzo vipya vya mapato, sasa sijui kama Mheshimiwa Waziri ameshawahi kufikiria. Ukiwa bandarini Dar es Salaam na maeneo mengine, utaona magari mengi sana yanakwenda nje ya nchi yamewekwa zile label za IT, zimeandikwa tu kwa marker pen.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sijui kama wasaidizi wako wameshawahi kujiuliza siku moja wakiamua vile vibao viandikwe kwa kutumia vibao halali vya number plates tutakusanya VAT shilingi ngapi na kiasi gani kingekwenda kusaidia kwenye maendeleo ya wananchi wetu. Kwa sababu watu hawa pia wamekuwa wanaharibu barabara. Lakini ukiandika kwa ile marker pen pale unachajiwa shilingi 10,000 tu ambayo inakwenda moja kwa moja kwa mwandikaji na Serikali pale haipati kitu chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona hapa tunaongeza kwenye kodi ya mafuta kwa maana ya road toll ili wananchi wakalipe. Na mpaka sasa Mheshimiwa Waziri ukumbuke Watanzania karibia milioni 2.5 ndio wanaolipa kodi, katika milioni 60. Na tumekuwa na taratibu sasa za kuwabana sana wafanyakazi pamoja na wafanyabiashara. Kwa hiyo, tunawakamua kwa nguvu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tujaribu kuangalia vyanzo vipya vya mapato ili viweze kuwasaidia hawa watu kupokea. Kwa hiyo niombe kabisa hili jambo la number plates mkaliangalie, mkaangalie pia hili wazo la mama kwamba Liganga na Mchuchuma sasa ianze kufanya kazi vizuri. Nia yetu na nia yako kama Waziri iwe ni uboreshwaji wa sera za mapato na matumizi na kutafuta vyanzo vipya vya mapato ili iweze kusaidia nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, umeongea vizuri sana suala la ETS. Lakini pia umeongea kuhusu suala la industrial sugar, na Jirani yangu hapa, dada yangu Mheshimiwa Hawa naye amelisema, na Waheshimiwa wengine huku nao nimesikia wakiwa wanalisema. Sasa ni vizuri na wewe mwenyewe kwenye taarifa yako umesema umeamua kuondoa kabisa hii tozo ya asilimia 15 kwenye industrial sugar ili iweze kuwasaidia wafanyabiashara kuweza kupata an extra working capital. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukumbuke kwamba Serikali sasa inadaiwa. Ile ambayo mliishikilia zamani mnasema nini kuhusu hii? Kuanza kuwapatia kuanzia sasa na kuendelea wakati huko nyuma zaidi ya miaka kumi hamjawahi kuwa- refund na yenyewe ni ngumu. Na pale umeonesha kidogo kwamba inapunguza mapato ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikukumbushe tena ile ilikuwa ni tozo ambayo mwisho wa siku ilitakiwa iwarudie wenyewe. Haikuwa mapato ya Serikali, Serikali mlikuwa mnaitunza. Sasa mfikirie namna ya kuwarudishia ili waongeze mitaji kwenye uzalishaji wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni sawasawa na VAT. Sijasikia hapo vizuri mkakati wako mahususi wa kuona VAT refunds zinarudi kwa hawa wawekezaji, zinarudi kwa hawa wafanyabiashara ili waweze kukuza mitaji yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la kuongeza mapato ni suala la ETS. ETS Waheshimiwa Wabunge ni Electronic Tax Stamp ambayo imekuwa inawekwa kwenye vinywaji. Na sisi kwenye Kamati tumeongea mara nyingi. Tunaishauri Serikali kwa mara nyingine, mkataba huu haukuwa bora sana, unasimamiwa na Wizara ya Viwanda na Biashara, sasa hatuna uhakika hili jambo linawahusu ninyi moja kwa moja, linawahusu watu wa Viwanda na Biashara, lakini mkakae na kujadiliana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hii ya kuhesabu chupa moja kwa shilingi 10 wakati Serikali inakwenda kukusanya kodi ya shilingi tatu kwa kuhesabiwa kwa shilingi kumi; tunamnufaisha nani? Kama tunaona kuna uhalali wa kufanya hilo jambo basi niishauri Wizara yako kimkakati kabisa sasa kazi hii ikafanywe na TRA, iwe sehemu ya kuongeza mapato. Kwa sababu hakuna haja ya kutumia gharama kubwa kutayarisha utaratibu wa kukusanya kodi halafu unakwenda kukusanya kodi ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, ukipata muda nitakuelewesha kwenye hili kwa sababu wafanyabiashara walikuja kulilalamikia. Kuna kampuni inaitwa SIPA ndiyo inayofanya kazi ya kuhesabu vinywaji tuseme.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano chupa moja ya Coca-Cola inatakiwa ilipiwe kodi ya shilingi tano, anayekwenda kuhesabu chupa na kumwambia TRA kwamba Coca-Cola wamezalisha chupa 20 katika chupa moja analipwa shilingi 10; hii siyo sawa. Muone namna sasa ya kuondoa ili kama inawezekana na kuna ulazima wa kufanya hivyo basi TRA wakafanye hii kazi ili iweze kuwanufaisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ni nzuri kama walivyosema wengi, lakini tuombe sana sasa – na Wabunge wengi hapa wamesema ni kazi nzuri – basi ile shilingi mia iliyotengwa kwenye mafuta lazima tuhakikishe inakwenda kuwa ring fenced na iende huko TARURA kwenda kufanya kazi kwa wakati. Utaratibu wa kupeleka baada ya miezi sita, baada ya mwaka mmoja na wakati mwingine unaambiwa wanapeleka kwa Zimamoto siku za mwisho kabisa za kumalizia bajeti, siyo mzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wana shida kubwa sana ya barabara huko vijijini, wananchi wana shida kubwa ya madaraja pamoja na vivuko. Sasa hela hii ikikusanywa na ukija hapa utueleze kwamba pesa iliyokusanywa kwa ajili ya miradi ya maji na miradi ya barabara awamu iliyopita, kwa maana ya bajeti iliyopita, imekwenda mpaka sasa kiasi gani. Hiyo chenji iliyobakia itapatikana lini ili mkakamilishe… kwa sababu hii ndiyo miradi…

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Shabiby.

T A A R I F A

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba haohao SIPA wanaotafuna sasa hivi upande huu ndiyo haohao walikuwa wana tenda ya vinasaba. Kwa hiyo bado wanaendelea kutafuna. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Cecil Mwambe.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaikubali taarifa hiyo. Na nataka nimuongezee tena hapa Mheshimiwa Waziri kwamba watakapokwenda kufanya review ya hizi kodi mbalimbali wanazoziingiza kwenye mafuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo dada yangu pale, Mheshimiwa Paresso, amesema, wakaangalie sasa kwamba mpaka sasa kwenye mafuta kuna kodi zisizopungua 16. Zinakaribia sasa hivi kufikia shilingi 900, tunakaribia kwenda shilingi 1,000. Kwa hiyo kwenye bei ya mafuta ya shilingi 2,5000, shilingi zaidi ya 700 inakwenda kama kodi Serikalini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sasa mkafanye review tuangalie vyanzo vipya vya mapato, tupunguze hizi kodi mbalimbali ambazo mwisho wa siku zinakwenda kumgandamiza mwananchi. Kwa sababu kwa namna yoyote ile, unapoongeza shilingi 100 kwenye mafuta wasafirishaji nao karibuni utasikia wameongeza gharama za usafirishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nauli kwa mfano kutoka Ndanda kwenda mpaka Masasi badala ya kuwa shilingi 2,500 au 1,500 tuliyoizoea sasa hivi, tunaweza tukaanza kuchajiwa shilingi 3,000 kwa sababu gharama ya mafuta imeongezeka. Na lazima hapa ukumbuke kwamba tunapoongeza hizi gharama za mafuta lazima tuone namna ya ku-balance tutafute sehemu nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze sana bajeti yako, na nikushauri tena kwamba weka malengo katika miaka mitano hii mama ikimpendeza na Mungu ikimpendeza, ukiendelea kuwa hapohapo basi twende kwenye utekelezaji wa budget deficit iwe single digit. Badala ya sasa ambapo tumetekeleza bajeti kwa asilimia 75 mpaka 80, tunatamani siku moja tuambiwe bajeti yetu imetekelezwa kwa asilimia 95 na kuendelea, ili tuwe tuna single digit, ndiyo tutakuja kuona manufaa makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii tunapanga hapa tunaomba ikatekelezwe kama tunavyosema. Wakati mwingine inatokea ama mnachelewesha kupeleka pesa, mnataka tena watu kule chini waanze tena kuleta taarifa juu; hili siyo jambo jema. Utakapokuja kwenye mid-year review au quarterly review basi tuone Waziri unapeleka pesa kadri zilivyopangwa hapa na Wabunge ili zikafanye kazi inayokusudiwa na tuone matokeo chanya kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru sana kwa nafasi uliyonipatia. Ahsante kwa muda wako. (Makofi)