Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Nusrat Shaaban Hanje

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi ili na mimi nichangie kwenye Bajeti Kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi bajeti hii ni bajeti ya kwanza katika Awamu ya Tatu ya Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, na ni bajeti ya kwanza kwenye Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan. Kwa utaratibu huo maana yake tukiangalia, Mheshimiwa rafiki yangu, kaka yangu, ndugu yangu Mwigulu, Mheshimiwa Waziri mwenyewe ameiita bajeti ya kimkakati. Hata hivyo naomba nimbadilishie kidogo, hii bajeti pamoja na kwamba unasema ni ya kimkakati lakini ni bajeti ambayo mimi naiita bajeti ya tamu-chungu; yaani tunang’atwa halafu tunapulizwa, yaani tunatekenywa huku tunafinywa. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, yes, bajeti hii kimsingi kuna mambo makubwa ambayo hayajawahi kuzungumzwa katika bajeti za miaka kadhaa mitano tukirudi nyuma. Kuna vitu ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa mara kwa mara na Waheshimiwa Wabunge mpaka na wananchi wetu huko, ambavyo vilikuwa havijaingizwa lakini kipindi hiki tunaviona. Pia, at the same time kuna vitu ambavyo kimsingi, vimewekwa kwenye lugha za kiuchumi sana, unaweza kuona havikuumizi, lakini kimsingi vinaumiza Watanzania kwa kiasi Fulani, nitaelezea.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukiwa tunazungumzia Bajeti Kuu ya Serikali mwaka 2021/2022 ni muendelezo wa mipango ile ya miaka mitano mitano ambayo imeshapita, na sasa hivi tuko watatu, maana yake tumetoka wa pili. Hatuwezi tukazungumza leo bila kuangalia tulipotoka, tulipo na tunapotaka kwenda. Kwa hiyo ni lazima tujifanyie evaluation kama nchi, kwamba tumetoka wapi, tupo wapi na tunataka kwenda wapi. Kwa sababu ni muendelezo, ndiyo maana tukasema ni awamu kwa awamu, awamu ya kwanza, ya pili na ya tatu. Hivyo tumekuwa tuna tatizo kubwa sugu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tunapanga mipango ya maendeleo ya miaka mitano mitano, tunatengeneza bajeti/tuna-formulate bajeti za kutusaidia ku- implement mipango; lakini kumekuwa kuna tatizo sugu la kutopeleka fedha za miradi ya maendeleo kama zinavyopitishwa na Bunge hili. Hili nalisema kwa nia njema ya taifa langu na ninalipenda sana taifa langu. Kimsingi Watanzania ukiangalia comments zao baada ya bajeti kusomwa kuna vitu wanavifurahia. Ninachosikitika mimi ni kwasababu, ninajua kuna mahala itafika tutakwama na tutarudi mwakani kusoma bajeti ya mwaka 2022/2023 tukiwa kuna sehemu hatujatekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninasema hivyo kwa sababu, mathalani, zipo Wizara ambazo zinachangia Pato la Taifa kwa kiasi kikubwa na zinagusa maisha ya Watanzania kwa kiasi kikubwa sana, ambazo utekelezaji wake wa bajeti ni chini ya asilimia 30 kwa miaka mitano consecutively, tangu mwaka 2016, mpaka mwaka huu tunaozungumza sasa hivi, 2020/2021. Kwa hiyo, unaona ni namna gani tunavyozungumza kwamba kuna shida sehemu. Tunapanga bajeti, tunapitisha vizuri, tunashangilia, tunafurahi lakini tukitoka hapo utekelezaji wake ni chini ya asilimia 30.

Mheshimiwa Naibu Spika, mathalani bajeti ya Wizara ya Kilimo kwa miaka mitano mfululizo, consecutively, tangu 2016 average ya bajeti yake ya miradi ya maendeleo imepelekwa asilimia 19.3 tu. Sasa tunategemea Watanzania wengi wameajiriwa na sekta hii, pia tunategemea ndiyo sekta inayolisha Watanzania asilimia 100, na vilevile Wizara hii inachangia Pato la Taifa asilimia 27.7 na sasa tunapeleka fedha katika kiwango hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na tumekuwa tukilalamika kwamba bajeti iongezwe, lakini hata ile ndogo inayotengwa haipelekwi pia kwa wakati nabadala yakeinapelekwa mwishoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ina-good faith kwa ajili ya taifa letu ni lazima tuone kwamba ni namna gani hizi Wizara ambazo tunasema zinaajiri asilimia kubwa ya Watanzania na kwamba zinachangia Pato la Taifa kiasi kikubwa, tunapeleka fedha kiasi gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya pili ambayo ina tatizo kwenye kupelekewa fedha ni Wizara ambayo kimsingi imebeba dhima kuu ya kauli mbiu ya Chama cha Mapinduzi, na hapa nipo na Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Tanzania ya Viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu viwanda na biashara, kutoka ukurasa wa 56 - 60 kwenye hii Ilani ya Chama Cha Mapinduzi wamezungumza kwa undani na kufafanua masuala ya viwanda na ya biashara; lakini utekelezaji huu wa bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara consecutively in years ni asilimia 20. Kwa hiyo maana yake Serikali ya Viwanda, Tanzania ya Viwanda asilimia 80 ya bajeti haijatekelezwa kwenye miradi ya maendeleo na tunazungumzia kauli mbiu ambayo tunaenda nayo; kwa hiyo kuna changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ya tatu ni kuhusu mifugo na uvuvi ambayo inachangia asilimia tisa ya Pato la Taifa; bjeti yake yaani imetekelezwa kwa asilimia 21 consecutively kwa miaka mitano ambao ndio Mpango wa Pili wa Maendeleo; sasa ni changamoto kwa kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia Wizara ya Afya ambayo ndiyo inayotoa nguvu kazi ya taifa bajeti yake imetekelezwa kwa asilimia 18.1 tu. Watanzania wakiwa wagonjwa hatutaweza kuzalisha. Bajeti ya mwaka 2020/2021 ya afya Wizara iliomba shilingi bilioni 360 lakini mpaka Machi mwaka huu 2021 walipelekewa shilingi bilioni 83 tu za kutibu Watanzania ili Watanzania wawe wazima wazalishe; ni changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi ninajua kabisa, nikiwaangalia Mawaziri ninaona nia yao ni njema, changamoto ni tuna kasungura kadogo tunagawana hako hako, ndiyo shida. Kwa sababu ili tupate fedha za bajeti tupeleke kwenye miradi ya maendeleo ni lazima tukusanye kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na Mwalimu Nyerere alishawahi kusema, kwamba, Serikali ambayo haikusanyi kodi kimsingi haiwezi kwenda kokote. Mimi ninajua kuna changamoto, na najua nia ni njema; tunatenga fedha zinatakiwa zije ziende zote, lakini tunashindwa kupeleka kwa sababu hatuna fedha. Sasa Mamlaka ya Mapato Tanzania kimsingi inatufelisha kwa kiasi kikubwa. Mpaka leo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wana matatizo yao mengi kule ndani, na inawezekana kuna mianya ya rushwa pengine ndiyo maana tunashindwa hata kufanya evaluation ya kodi. Kwa sababu wanaolipa kodi, wewe unafahamu, ni asilimia tano tu ya Watanzania milioni 60, haiwezekani.

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu wale ambao wanalipa kodi ambao ndio mnajua system zao, ni walimu, ni wafanyakazi wa Serikali, mnajua system zao za mishahara, ndio wanakatwa. Kwa hiyo ni Watanzania wachache wanaoendelea kunyonywa kwa kulipa kodi, kuna wengine wengi ambao hawalipi kodi kwa sababu hamna utaratibu mzuri wa kuwafuatilia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka ya Mapato Tanzania imeshindwa kufanya ukaguzi wa walipa kodi. Mimi leo ninaweza nikatoa taarifa za uongo za biashara yangu, nikalipa mara ya kwanza na nikaendelea kufanya biashara miaka mitano, bado nitaendelea kulipa kiwango kile kile, niwe nimekua, niwe sijakua hakuna nia njema. Tulisikiliza wote hotuba ya Mheshimiwa Rais, nia yake, na kwa sababu alizungumza. Kwamba wigo wa ulipaji kodi ni mdogo sana, tunahitaji kupanua wigo, kwa sababu lengo ni kupata fedha tukapeleka kwenye miradi ya maendeleo, kwa hiyo ni changamoto kimsingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi naomba nimshauri Mheshimiwa Waziri, kwamba, kuna wale wawekezaji ambao tunategemea kuwa ni sehemu ya sisi kupata kupata mapato ili tuweke kwenye miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu wana kesi na kuna kesi ziko mahakamani. Mpaka sasa tuna mashauri ya rufaa mahakamani, yanayosubiri kuamuliwa ya muda mrefu, tunadai takriban trilioni 360 na dola za kimarekani milioni 181. Hizi fedha ni za muda mrefu sana, na tumekuwa tukiimba kwamba zikipatikana zote zitasaidia kuendesha nchi miaka 10, na nini story zinanoga. Lakini kimsingi inawezekana mkatafuta mazingira ya kuongea na hao watu, either wasamehewe hizi kodi, waendelee kufanya biashara katika mazingira mazuri, au mtafute namna bora ya kuangalia. Lakini kwa sababu ya muda nashukuru, sitaunga mkono.