Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Ahmed Mabukhut Shabiby

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gairo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa kabla sijasahau, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Naunga mkono kwa sababu yale ambayo niliyazungumza sana siku za nyuma ambayo yalikuwa hayafanyiwi kazi, namshukuru mama yetu pamoja na Waziri wake wa Fedha kwa kuyashughulikia. Kwa mfano, mimi sio mpenzi wa kuweka majina kwenye magari, lakini mlipoweka shilingi milioni 10 mlikuwa mnapoteza sana mapato kwa plate number za binafsi. Tulitoa ushauri, tunashukuru safari hii mmeufanyia kazi. Mabango yote ya matangazo iwe ya kwenye magari, iwe kwenye maduka na hili nalo mmelifanyia kazi. Kwa hiyo, nakuunga mkono Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kazi nzuri uliyoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima nizungumze, kwenye hii Wabunge wengi walizungumzia habari ya pesa kuongezwa kwenye mafuta kwa ajili ya kwenda TARURA. Mimi ni msafirishaji wa mizigo na abiria. Shilingi 100 haiwezi ikaleta madhara ya kuongeza nauli wala kuongeza kitu chochote.

Nimejaribu kuongea na wamiliki wa vyombo mbalimbali vya usafiri hasa TABOA nao wakaniahidi kabisa, wakasema hilo ni jambo zuri sana kwa sababu hiyo pesa inapelekwa sehemu ambayo ni muhimu, sehemu ya TARURA. Kwa sababu huwezi ukaikwepa ile shilingi 100/=. Utakwepa shilingi 100/= lakini ile gari ikitembea kwenye njia mbovu itavunja vitu zaidi ya ile shilingi 100/=. Kwa hiyo, utakwepa shilingi 100/= lakini gari inaweza ikavunja vitu mara 20 ya ile shilingi 100/=. Kwa hiyo, barabara zikiwa safi, gharama nyingi sana zitapungua. Nataka nikuhakikishie kwamba hii haitaongeza gharama ya aina yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilishawahi kusema hapa katika Bunge hili kwamba Wachina hawakupata maendeleo hivi hivi kama mnavyofikiria. Miaka ya nyuma kidogo tu hapo walikuwa sawasawa na Watanzania, lakini wale hata walipokuwa wanaamua kuvaa suti, siku moja wote wanavaa chew and lie zote za rangi moja. Ilikuwa agizo la nchi yao. Wakiamua kuvaa suti moja wiki, ni wote. Masharti hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni lazima tufunge mkanda. Hili narudia, wewe unalikumbuka. Kama tunataka kweli maendeleo kwenye hii nchi, ni lazima kufunga mkanda, siyo kuzungumza. Maana Wabunge wote sisi kazi yetu ni kuishauri Serikali. Kuna watu wengine wanaitwa wachambuzi wako huko nje; na kuna watu wengine wanatoa mawazo. Sasa unatoa mawazo, mbadala wake nini? Unazungumza kodi hii, wananchi hapa watateseka, nini na nini; na nchi inataka pesa. Nini unaleta mbadala wake? Kama hutaki kodi hii iende kwenye simu, iende kwenye mafuta, mbadala wake unaochangia ni upi? Ukilalamikia kitu, lazima ulete na mbadala. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utakuta kuna mchambuzi hajawahi kufanya kitu cha aina yoyote. Mtu anachambua hapa, anasema wananchi kwenye simu watapata shida; wakati hajasoma hata hiyo yenyewe inazungumza nini? Imeshasema, kuanzia shilingi 10 mpaka shilingi 200. Mimi na- recharge kwenye simu yangu shilingi 50,000 sasa nikikatwa shilingi 200 kuna ubaya gani? Mtu anaweka shilingi 2,000, shilingi 1,000 anakatwa shilingi 10, kuna ubaya gani kuchangia maendeleo ya nchi yake? Hata hivyo, watu hawaelewi, wanapotosha. Utakuta kwenye vyombo vingine vinaandika tu, yaani hata haelewi, shilingi 200, kila siku shilingi 200/=. Kama kitu huelewi, acha kuzungumza. Kama unataka kupinga, lete mbadala wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ndani ya bajeti hii nakumbuka mama ameahidi kule Mwanza siku ya Mei Mosi kwamba mwakani ataongeza mshahara. Hatuna walimu, tunalalamikia walimu; tunalalamikia maji kama Mheshimiwa Mbunge pale alizungumza vizuri sana; tunalalamikia vitu vingi; na bajeti hii tunatakiwa tupate shilingi trilioni 36 kwa ajili ya kuleta hivyo vitu. Sasa kama huna mbadala wa kuleta hiyo pesa, wewe unalaumu tu, sasa tufanyaje? Nchi isimame! Haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hii bajeti ni nzuri sana, wala haina shida ya aina yoyote. Hata ile kuweka kodi ya viwanja ni vizuri, tena hata baadaye tuje tuangalie na kodi ya ardhi, ije iingie huku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme tu, TRA wanafanya kazi nzuri sana. Namjua Kidata, ni mlokole na ni mtu mzuri sana pamoja na Makamishna wake, lakini huku chini kuna matatu; na siyo tena kwa mameneja wa mikoa. Hawa watu wengine tu wako TRA lakini wamesumbua sumbua na nafikiri sasa hivi kidogo kumetulia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lililopo, TRA kulazimishwa kutumia na vyombo vingine ambao hawana utaalam wa kodi; unamshauri TRA akachukue TAKUKURU, TAKUKURU anaelewa nini kuhusu mambo ya kodi? Unamchukua TRA unamshauri, unamwambia atakula rushwa, yuko na watu wengine wa vyombo vya usalama, wanajua nini katika masuala ya kukusanya kodi? Kodi ni elimu na ndiyo maana kuna Chuo cha Kodi. Unapoleta mtu mwingine kwa wafanyabiashara, kwanza sura yake peke yake inatisha. Unaweza ukamuua yule mfanyabishara hata kabla ya kukusanya kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tuangalie hii. Mambo ya task force ambazo hazina mpango ni za kutisha. Mfanyabishara na TRA wanatakiwa wawe pamoja kueleza kwa lugha nzuri, mtu atalipa kodi. Kwa wafanyabishara nao, Mheshimiwa Waziri nimeona ulianza kuzungumza pale kwamba sasa hivi watu kwenye account wasiingiliwe, wasikamatiwe vitu vyao, lakini kuna mfanyabiashara mwingine anaenda TRA, anapigwa kodi shilingi milioni 200, anapeleka mahesabu yake, inakuja kodi labda mpaka shilingi milioni 80, anapewa miezi sita ya kulipa, anaomba mwenyewe au mwaka, lakini unaisha mwaka hajalipa hata shilingi 100/=. Sasa unategemea hiyo pesa itapatikana vipi? Kwa style gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi kubembeleza mtu ambaye amekubali mwenyewe, kasaini mwenyewe halafu kodi yake mwenyewe halipi. Halafu unasema asichukuliwe kitu wala asikamatiwe mali au asichukuliwe hela yake benki. Hivyo vitu viwili tofauti. Lazima hilo tuliweke sana Mheshimiwa, usije ukaanza kuwa mpole mpole sana ukataka kufurahisha watu kwenye sheria. Sheria ing’ate huku na huku, pande zote mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme na Serikali nayo isiwe na fitina na wananchi wake. Sekta Binafsi ndiyo Sekta ambayo inaajiri watu wengi. Sasa kama ninyi Serikali mnataka kufanya kila kitu, basi sameheni na kodi. Punguzeni kodi. Maana sasa hivi ukitaka, ukienda sijui matangazo; vyombo vya binafsi havipewi matangazo. Wanapewa vyombo vya Serikali, halafu vyombo vya Serikalini hatusomi, maana wanajisifia wenyewe kwa wenyewe tu. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, utakuta matangazo. Halmashauri inaweza ikatoa tangazo inataka Mkandarasi kwenye magazeti sita, hajapatikana Mkandarasi, lakini ikienda kutolewa kwenye gazeti binafsi au kwenye media yoyote binafsi, tayari utakuta Wakandarasi 80 au 40. Kwa hiyo, mnakula hela zetu za Halmashauri bila sababu kwa kutulazimisha taasisi zetu za Serikali zifanye matangazo kwenye sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija kwenye Wakandarasi, mnataka nini? Kwa mfano, pale kwangu Gairo hakuna Engineer wa Wilaya. Kuna technicians. Unamwambia ajenge hospitali ya wilaya, ikibomoka! Ooh, tunatumia force account, hatuna wataalam. Pelekeni basi kwanza wataalam. Yote hiyo ni Mkandarasi asipate pesa wakati anaajiri watu wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwa hawa wenzangu kama akina Mheshimiwa Vita Kawawa wenye kumbi nakadhalika; aah, hatutaki kumbi, tunataka sisi tufanyie maofisini. Ofisi zote za Serikali sasa hivi zinanukia chapati tu kwa sababu ya haya mambo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, jamani sasa kama ninyi mnataka kodi kwa watu binafsi na ndiyo wanaajiri watu wengi, lakini hamtaki wapewe kazi, sasa watafanya kazi gani? Ukienda kule bandarini, kuna TASAC, hawataki wale clearing and forwarding wafanye kazi; anaingilia sheria hata siyo zake. Iliundwa ifanye kazi ya sheria, mizigo ya Serikali shehena za dawa na vitu vingine, lakini sasa wanaingia wanataka wafanye kazi wao. Sasa watu watafanya kazi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tuangalie na hizi kazi. Ujenzi ni JKT, halafu mafundi wenyewe ni hawa hawa. TEMESA wanataka kazi za Serikali. Kwa mfano, Gairo, generator imeungua, nimeenda kwa fundi anataka shilingi 700,000/=, wamekuja TEMESA wanataka shilingi 4,000,000/= halafu fundi ni yule yule niliyekubaliana naye mimi shilingi 700,000/=. Sasa Serikali sehemu nyingine mnapigwa kwa ajili ya kukunja roho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nataka nikwambie kwenye mambo ya VAT ya maduka na sehemu nyingine. Utakuta hapa pana mtu amesajiliwa VAT, kuna mtu hajasajiliwa VAT. Kwa hiyo, akinunua huyu biashara kwa sabbau hana VAT anauza kitu shilingi 10,000, duka la pili anauza shilingi 11,800 maana yake ameshaweka ile shilingi 1,800. Sasa ni nani atakwenda kununua kwa huyu aliyezidisha bei kwa shilingi 1,800?

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu wanayonunua hii ni moja labda kule kwenye kiwanda, lakini kwa sababu huyu amesajiliwa VAT atauza shilingi 11,800 na kwa sababu huyu hana usajili wa VAT, anauza kwenye duka hilo hilo kwa shilingi 10,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, jaribu kutafuta kwa hawa wanaoleta vitu kwa jumla kwenye viwanda; kama VAT, basi waangalie technique yake wanafanyaje kiutaalamu? Kwamba VAT ipigwe kule kule, ikija huku watu wote wameshalipa VAT. Uangalie tu utafanyaje asilimia zile kwamba hii akiuza ile VAT ya kwanza itatoka kiwandani na ya pili itakuwaje ili ilipishwe kule kule moja kwa moja? Ikija huku kila mtu na kila kitu kiwe kwa VAT ili competition ya maduka iwe iko sawa. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)