Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu. Naomba nikiri kwamba leo ninasimama kwa unyenyekevu mkubwa kuliko siku zote nilizosimama hapa Bungeni kuchangia bajeti. Kwa nini? Mnaijua sababu. Imeletwa bajeti ya kipekee kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni kipindi changu cha tano, sijawahi kuona bajeti ya sura hii. Hii ni bajeti ambayo ni ya kipee, ni bajeti ambayo imekwenda kugusa Watanzania wote. Hii ni bajeti ya kwanza ya mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Mama Samia ni mama mwenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikwambie kitu kimoja. Mimi ninayeongea hapa ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, ngoja nisimame vizuri; ninayoongea siyo maneno yangu, haya leo nimetumwa na wananchi wa Same Mashariki. Wameniambia nije hapa Bungeni, utanisaidia nipige magoti kidogo niishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi, nimshukuru Mama yetu Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu. Kwa nini? Jamani, sisi tangu tumeanza Bunge hili, kila Mbunge anayesimama, anazungumza TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeizungumza TARURA miaka mingi, jamani TARURA iongezewe pesa, kila Mbunge amezungumza. Sasa tabia ya akina mama iko hivi, mnisikilieze vizuri. Akina mama, hata kama ana homa, amelala kitandani, mtoto akilia, mama ananyanyuka. Anamwangalia mtoto, kwa nini analia? Wabunge mmelia sana. Mama ana kazi nyingi, lakini amenyanyuka. Ana kazi nyingi sana. (Makofi/ Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumelalamika sana na barabara za vijijini. Mimi ni mhanga wa kwanza ambaye barabara zinanitesa, kumbukeni hotuba zangu kabla ya bajeti kuanza. Maana yake mtoto analia, ana njaa saa saba iko mbali ya chakula cha mchana, hapa katikati unamwambia kula hiki kidogo. Bajeti inaanza Julai, mama akasema jamani nimewasikieni Wabunge na ugomvi wa TARURA, embu chukueni shilingi milioni 500 hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, naomba niwaambie kitu kimoja. Jambo alilofanya mama Samia Hassan, limegusa sana wananchi. Kwangu wamefanya sherehe siku tatu kwa sababu ya barabara. Sasa naomba niwaambie kitu kimoja, mama amefanya upande wake, ametoa kila Jimbo shilingi milioni 500. Waheshimiwa Wabunge, Bunge linakwisha tarehe 30, nendeni majimboni mkazisimamie shilingi milioni 500. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa onyo kwa Mameneja wa TARURA Wilaya, hizi shilingi milioni 500 isipotee hata shilingi moja. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Kabisa! (Makofi)

MHE. ANNE K. MALECELA: Waheshimiwa Wabunge, kasimameni imara. Kwa nini nasema hivyo? Ili tuone kitu mama alichofanya, kionekane kizima kizima, lakini mkiziachia zikidokolewa, mtakuwa mnamuumiza aliyezileta hizi pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wangu wamenituma nisema hayo. Kwa kweli kwa ajili ya wananchi wangu, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu tunaomba upumzike sasa. Wananchi sasa umewachanganya. Wananchi wamechanganyikiwa na mapenzi yaliyoota ni makubwa sana.

Tunaomba mwendo huu mlioanza Serikali ya Awamu ya Sita, mwende nayo mpaka mama amalize awamu zake zote mbili. Tunawasihi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa unyenyekevu mkubwa, hili la shilingi milioni 500 Waheshimiwa Wabunge tafadhali, baada ya tarehe 30 hizi safari zenu za Dubai, sijui India, sijui wapi, hapana. Majimboni, tukazisimamie hizi shilingi milioni 500. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa wale ambao hawana matatizo ya barabara hawachanganyikiwi. Naomba niwaulize, tangu tumeanza Bunge hili, kuna hotuba nimesimama nisiongee barabara?

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna.

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna. Kero kubwa ni barabara kwenye jimbo langu. Mama yetu amekwenda akagusa wananchi wangu kwenye mioyo. Furaha iliyoko Same Mashariki haijapata kutokea. Sasa naomba nirudi kwa Serikali niwashauri kitu kimoja. Tusichukulie mambo kiutani utani. Let us work!

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali kuhusu kukusanya mapato. Ni kweli mnakusanya, lakini tunaposafiri kwenda nchi za wenzetu, tujifunze. Mimi nilikwenda China kabla hawajafunga China. Nikienda China nakaa kama siku 5, 6 au 10. Siwezi kuzunguka China mwenyewe, lazima nizunguke na mkalimani. Nikafika mahali nikawakuta wazee wanauza mahindi. Nikamwambia yule mkalimani, ngoja ninunue mhindi hapa. Akanichukulia mhindi mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri anisikilize. Nilipopewa ule mhindi, nikaula, nikaupenda. Nimepokea ule mhindi, nimeuweka mdomoni, nikamwona yule mzee anayeniuzia, anaandika kitu kwenye simu yake. Nikamwuliza yule mkalimani, anafanya nini? Akasema analipa kodi. Yaani pesa niliyolipa, tayari analipa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, kuna pesa nyingi sana tunaziacha. Tafuteni njia ya kukusanya pesa. Huyu Mchina, mzee mtu mzima, akaja mtu wa pili mimi nimesimama pale, akanunua mhindi. Mzee anatoa mhindi, anaandika. Anakusanya, lakini anakusanya kodi kwa furaha, tena ana raha. Jitahidini mkatoe elimu kwa wananchi, walipe kodi bila ya shuruti. Waone raha kulipa kodi. Hilo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuna jambo kidogo naomba nizungumze tofauti. Hili suala la kulipa kodi kwenye majengo rudini mkaliangalie vizuri Mheshimiwa Waziri. Huko mitaani tusidanganyane, kuna mkanganyiko. Kinachohitajika ni kwamba Waziri mkaliangalie vizuri hili jambo mliweke vizuri kwa wananchi lieleweke, wananchi wawe na raha. Hatupendi bajeti hii ya kwanza ya Mheshimiwa Mama Samia Hassan Suluhu iwe na maneno maneno huko nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina uhakika, Mheshimiwa Mwigulu nakuheshimu, ukaangalie vizuri, utakapofunga hapa ukijumuisha, Watanzania wakuelewe kwamba hii kodi anayekwenda kulipa ni nani; kati ya mwenye nyumba na mpangaji? Iwe straight inaeleweka, lakini tusiseme kwamba imekuwa rahisi, hapana. Sisi kazi yetu ni kuwashauri nyie. Mitaani hii kidogo imeleta mkanganyiko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na ninapiga magoti tena, nimetumwa na wale wananchi wa Same Mashariki, ahsante sana. (Makofi)