Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Yahaya Omary Massare

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manyoni Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii nichangie katika bajeti hii kuu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Samia Suluhu Hassana aliyepokea kijiti kwa Dkt. John Pombe Magufuli, Hayati mpendwa wetu ambaye alitutoka pasipo sisi kutaka lakini kazi ya Mungu huwa haina makosa mara zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu mpendwa sana, sana kabisa mama yetu ambaye juzi tu ameonesha namna gani wanawake kuwa ni tea bags ambazo lakini bila maji ya moto haziwezi kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwa jinsi ilivyotufanyia vizuri katika Majimbo yetu. Jimbo langu ambalo nimekuwa mwakilishi kwa vipindi viwili, limefanyiwa mambo mengi sana na Seriakli yake chini ya Dkt. John Pombe Magufuli lakini sasa mama Samia Suluhu Hassan ameenda kuongezea kutuletea shilingi 500,000,000 kwa ajii ya kuboresha miundombinu iliyokuwa imechakaa katika barabara zetu za vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye ni kiranja wa Serikali na kiongozi wa Serikali katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano kwa jinsi alivyopokea mawazo ya Wabunge hususan katika kilimo cha alizeti na hivi juzi tu alikuwa Singida akizungumza na wadau mbalimbali juu ya kilimo cha alizeti ili kuondoa pungufu hili la mafuta ya chakula ambayo tunaagiza kutoka nje kupitia alizeti naamini kwa mikakati ambayo inapangwa sasa inaweza ikasaidia sana mikoa hii mitatu ambayo imewekwa kimkakati kuweza kulima alizeti zenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti hii haija-reflect sana kwenye kilimo lakini tafiti za mbegi ambazo zinatakiwa ziende zikalimwe katika mikoa hii mitatu ya Simiyu, Singida na Dodoma zinafanyika katika mikoa ambayo ina mvua nyingi. Niombe Wizara ya Kilimo ikiwezekana, tafiti za mbegu za alizeti ambazo zitalimwa katika mikoa hii mitatu zikafanyike katika miongoni mwa mikoa hii mitatu. Mkoa wa SIngida uwe kielelezo kwa sababu ndiyo waanzilishi wa zao hili na mbegu za kulima alizeti zizalishwe katika Mkoa wa Singida ili kuonesha matokeo chanya ya alizeti ambayo yatakuwa bora zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa katika kilimo hapo hapo, Serikali inatakiwa iongeze nguvu kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji. Tutengeneze mabwawa kukinga mito ambayo inapeleka maji katika mito, maziwa, mito inayopeleka maji katika mabwawa kama hili hapa Suruingai – Bahi na mito mingine ambayo iko katika mikoa hii ya katikati ambayo ni mikoa kame tuweze kupata kilimo cha umwagiliaji scheme nzuri kama iliyopo scheme ya Bahi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mkoa wa Singida nasi tunayo mito hata katika Jimbo langu. Niombe watu wa kilimo waje wafanye tafiti tuone ni eneo gani tunaweza tukaongezea hasa upande wa Jimbo ambalo natoka. Tuna scheme moja tu ya umwagiliaji ambayo ni scheme ya Itagata. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika mifugo, mikoa hii ambayo inaenda kulima alizeti, mashudu ya alizeti baada ya kukamuliwa ni chakula bora sana kwa mifugo. Wizara ya Mifugo nayo ije na mkakati wa kuhakikisha tunapata malambo ya kunyweshea mifugo yetu hasa katika Jimbo ambalo natoka limekuwa na wafugaji wengi, wengi wametoka kanda ya ziwa kwa sababu sisi tulikuwa tuna nafasi kubwa wamekuja kupata fursa ile ya majani na eneo pana la kuchungia mifugo. Tuna tatizo kubwa la malambo, lakini na majosho. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wizara hiyo ya Waziri Mkuu, nimpongeze sana Mheshimiwa jenista Mhagama kwa kazi nyingi na nzuri sana ambazo amekuwa akifanya katika Wizara hii ya Sera, Bunge, Vijana na watu wenye Ulemavu. Taasisi zilizo katika Wizara hii, mfano Taasisi ya OSHA ilikuwa ni kero kubwa sana kwa watu wenye viwanda, kulikuwa na tozo nyingi hasa unapoanza ujenzi wa jambo lako lolote OSHA walikuwa ni kikwazo. Leo wamepunguza tozo nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii ya Bunge lako tukufu kuwapongeza OSHA lakini na kumpongeza sana Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa kazi nzuri aliyofanya na kufanya sasa zile kero nyingi ambazo zilikuwa zinatokana na Taasisi hizi sasa ziweze kuwa ni changamoto ambazo zimeanza kuisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini taasisi nyingine iko chini ya Wizara hii ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Taasisi ya WCF, miongoni mwa Wabunge ni mashahidi jinsi walivyopata kupata compensation kwa matukio mbalimbali yaliyowapata ni mmojawao ambao nilifidiwa baada ya kupata ajali mbaya ya gari kupitia Taasisi hii ya WCF. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Jenista Mhagama na Wizara yake na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na Naibu mawaziri waliopo katika Wizara hiyo kwa kazi nzuri ambazo tumeendelea kuziona zikionekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jimbo langu huwezi kuzungumzia jambo lolote bila kuzungumza barabara. Sisi watu wa Mkoa wa Singida tunaunganishwa na Mkoa wa Mbeya kupitia barabara ambayo inapita katika Jimbo langu na ni barabara pekee ambayo imebaki ina urefu mkubwa. Ina kilometa 412. Katika kilometa 412, kilometa 219 ziko ndani ya Jimbo langu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishukuru Serikali kwa kuonesha nia ya kujenga kilometa 56.9 japo zimetangazwa kilometa 25 lakini kwa kilometa 25 maana yake itatuchukua zaidi ya miaka 20 kumaliza hizo kilometa 412. Niombe sasa Serikali ichukue juhudi za maksudi kuongeza kipande cha barabara cha kutoka Mkiwa – Rungwe, zile kilometa angalau zifikie kilometa 100 tunazozijenga kipindi hiki ili wananchi hawa nao waunganishwe na mtandao wa barabara, waweze kukimbizana na hali hii ya uchumi, waweze kuwa walipakodi wazuri lakini mazao yao yafike katika masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Singida pia unaunganishwa na Mkoa wa Simiyu kupitia daraja la Sibiti. Haijaonekana popote katika Bajeti ya Serikali, Bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwamba mnaenda kuanzia wapi. Niombe sana Serikali yangu ya Chama Cha Mapinduzi, Waziri wa Fedha unatoka Singida, uone watu wa Singida wanavyoweza kuunganishwa na mikoa mingine. Usije kuwa mpishi alilia kwenye… itoshe hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina jambo moja mahsusi ambalo nilikuwa nataka nizungumzie. Hapa katikati kulikuwa na ugaidi mkubwa katika hifadhi zetu na mapori tengefu. Watu wanaomiliki silaha hasa bunduki aina ya rifle walifika mahali ukisalimisha silaha ile unasafiri basi huwezi kuichukua tena lakini ukiuza silaha yako au ukinunua silaha kwa mtu mwingine au mtu aliyekuwa anamiliki silaha akafariki, warithi wake sasa hawapati vibali vya kumiliki silaha. Ni nini tatizo? Mtuambie zimepigwa marufuku? Silaha hazihamishwi? Hasa rifle, zote kuanzia 22 mpaka 458.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali basi ije na matamko ya kuonesha kwamba hwa watu wanaotaka kumiliki silaha kwa njia nzuri wanapata kumiliki silaha. Ahsante sana. Naunga mkono hoja ya Serikali. (Makofi)