Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Kwanza kabisa nami niungane na wenzangu kuipongeza sana Serikali. Ni mara ya kwanza kuingia katika Bunge hili Tukufu lakini kwa yaliyotokea kwenye hii bajeti kwakweli yanafurahisha sana. Na kwa upande nimpongeze Waziri wa Fedha nimpongeze mwenyekiti wa Kamati na Wajumbe wote wa Kamati ile ya bajeti, mmejitahidi sana angalau kujibu yale ambayo tuliyokuwa tunayazungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimefurahishwa kwanza kuhusu lile suala la mikopo, nimefurashishwa mno. Kuondoa zile sijui retention zile adhabu kwenye mikopo, nimepigiwa simu yaani nifuraha nifuraha huko vyuo vikuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuongeza mikopo kutoka bilioni 464 mpaka 500, niwapongeze Serikali. Na kama Mheshimiwa Waziri wa Fedha alivyoahidi, amesema watoto wote wenye vigezo watapata mikopo kupitia ule mradi wa HIT.
Mimi ninaamini kutakuwa na mabadiliko makubwa sana, si kwa vyuo vikuu tu lakini na kwa wale wanaomaliza. Na ndiyo kutokana na hii miradi nafikiri sasa fedha za research itapatikana. Niipongeze sana Serikali yangu, kwakweli I just love you people.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nije kwenye suala moja, Mheshimiwa Waziri wa Fedha naomba kwenye hili unisikilize vizuri sana nashauri, kuna ulipaji wa madeni wazabuni na wakandarasi, na niiombe sana Serikali haya madeni mnayolipa mzingatie na lile suala la Nelson Mandela kuna tatizo kubwa sana kwenye kile chuo Wizara ya fedha pamoja na Kampuni inayoitwa PPL walichukua mkopo wa mabilioni ya fedha takriban bilioni 38.7 kwa ajili ya ujenzi wa kile chuo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, walipochukua ule mkopo wakaipa ile kampuni PPL wao pia wakaingiza kampuni nyingine na kugawana kazi na wakampa mzabuni anayeitwa ELERA Construction, yeye ashughulikie na viwanja vya michezo. Sasa huyu hajamaliza vile viwanja vya michezo na anadai ile fedha, takriban milioni mia nne na kitu, ambayo ni retention. Sasa wale wamesema hawaweze kumlipa kwa sababu hajamaliza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikuombe Mheshimiwa Waziri, kuna vurugu pale, wanashindana je, nani amlipe huyu na nani ambaye hataki kumlipa. Kwa hiyo kuna vurugu kati ya Wizara ya Fedha, Ardhi pamoja na Wizara ya Elimu, na Ardhi nafikiri inahusika. Sasa nimuombe Waziri alimalize hilo, na nikimaliza kuzungumza hapa Mheshimiwa Waziri nina document nitakupa uandike umalize lile tatizo la Nelson Mandela kwa sababu huyu mtu anataka retention lakini kazi hajamaliza, wewe ukimsimamia najua hilo litakwisha nafikiri umenielewa hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine nije kwenye ujenzi wa miundombinu. Mimi nakushukuru, kwenye elimu mmetoa bilioni 406 kwa ajili ya kuangalia miundombinu katika elimu. Niiombe sana Serikali na hasa Waziri wa Fedha pamoja na Waziri wa Elimu, kaeni pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niombe majengo yaliyojengwa UDOM, Waheshimiwa wenzangu mtakumbuka, UDOM ile ilijengwa kwa speed kali mno ili kuwaokowa watoto wengi waingie vyuo vikuu; wazo lilikuwa zuri na ni jema, lakini niwaambie kitu, yale majengo yalijengwa mengine kwa speed ya ajabu kiasi kwamba si imara. Kuna nyufa na tiles zimebanduka. Niwaombe Waziri wa Fedha na Waziri wa Elimu nendeni mkatembelee pale UDOM mtasikitika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tufanya ukarabati kabla hali haijawa mbaya. Nendeni UDOM, lakini si huko tu kuna sehemu nyingi majengo yamechakaa; ukienda MUST ni balaa majengo yamechakaa, ukienda Hombolo barabara haifai na hizo ni barabara zote zinazoingia vyuo vikuu. Jamani mbona tumeviweka nyuma ebu wasaidieni ili nao waonekane kweli ni vyuo vikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hawa Hombolo wamepata eneo pale palikuwa kwa Mkuu wa Mkoa (RS); sasa muwasaidie, wanataka kutoa structure nzuri mno pale, nyinyi muwasaidie kwa kuwa-top-up ili waweze kujenga jengo zuri lenye tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nirudi kuzungumzia fedha mlizotenga kwa ajili ya sensa. Mimi nimefurahi mmetenga fedha za kutosha, bilioni 328 sio mchezo. Hata hivyo naomba sana m-develop device za kuweza kugundua watoto wenye ulemavu wanaofichwa wakati wa sensa ili tupate idadi kamili ya watu waliopo; sasa wale wanaofichwa ndani mtawagunduaje? Ninyi mtumie teknolojia, mtengeneze devices wakati wa sensa ili tupate idadi hata ya wale watoto wanaofichwa ili waweze kusaidiwa na Serikali yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho niipongeze Serikali kwa kuingia kwenye hizi blocks. Nakumbuka Mheshimiwa Naibu Spika alisema nini Kiswahili chake, nimejaribu kutafuta hili neno blocks sijui ni vipande. Nipongeze kwa kuwa kwenye hizo blocks; tuna PAP tuna IPU maziwa makuu na SADC.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo SADC yenye ina nchi kama 15. Sasa unaona tukishakuwa blocks nyingi kiasi hiki mimi ninaamini kwanza tutaleta mahusiano mazuri na vilevile tutaondoa na vikwazo visivyo vya kikodi. Wazungu wale waliotoka Songea wanasema none tariff barriers zitaondoka (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa kufanya hivyo, na pia kwa kujikita huko mimi ninaamini tunaweza kufungua masoko vizuri na kuwa na urafiki wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi baada ya kusema hayo nikushukuru sana, ahsante sana. (Makofi)