Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Anastazia James Wambura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa mwisho jioni hii ya leo katika bajeti hii ya Serikali. Nianze kwa kusema naunga mkono hoja. Kabla sijaendelea, napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango na Naibu wake Mheshimiwa Masauni pamoja na timu nzima ya Wizara kwa kuandaa vizuri mpango huu. Hata hivyo, Mheshimiwa Waziri alitenda haki katika kuwasilisha. Hongera sana Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, sisi Wabunge ni wapika kura wake. Nadhani sote tutakubaliana kwamba hajawaji kutuangusha wapiga kura wake na anazitendea haki kura zetu za ndiyo ambazo tulimpa hapa. Hii ni kwa sababu Mheshimiwa Waziri Mkuu anafanya kazi bila ya kujali leo ni Jumamosi wala leo ni Jumapili. Kama tutakumbuka ni kwamba juzi tu hapa tarehe 6 Juni, 2021 tulikuwa naye Lindi katika Mkutano wa Wadau wa Korosho na alitoa tamko zuri sana kutoka kwa mama yetu. Kutokana na matamko haya, wakulima na niseme ni wakulima wote wa korosho pamoja na wadau wengine walifarijika sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo hivyo tu, Jumapili ya tarehe 13 Juni, 2021 tumemwona pia akiwa Singida na Wadau wa Alizeti na ambapo pia alitoa matamko mbalimbali ya kutia faraja kwa wakulima na wadau wa alizeti. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu na ninaomba tumwombee kwa Mungu kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia nitoe shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Jenista Mhagama ambaye alichukua swali ambalo aliniulizia mtu kwa niaba tarehe 01 Juni, 2021 linalohusiana na barabara ya kutoka Kibiti – Lindi hadi Mtwara. Hili linazungumzia uharibifu mkubwa wa barabara. Nashukuru sana na ninaomba tu kukumbushia kwamba kweli alifanyie kazi kwa sababu lile ni tatizo kubwa na Serikali ilitoa maelezo hapa kwamba sasa mbadala wake itakuwa ni kwamba magari yenye uzito mkubwa au mizigo mizito iwe inapitia katika Bandari ya Mtwara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo ambalo lipo pale, nafiri inabidi Serikali iliangalie kiupekee zaidi kwa sababu katika maeneo ya Kikula, Kilanjelanje, Mandawa na maeneo mengine, kuna uchimbaji mkubwa wa mawe ambayo yanatumika kama malighafi viwandani kwa ajili ya kutengeneza saruji. Sasa hapa katika haya maeneo utaona kuna uharibifu mkubwa sana, kuna mashimo makubwa ambayo ni hatarishi. Tukisema kwamba mizigo ile iwe inasafirishiwa Bandarini, kule hakuna Bandari ni lazima mizigo hii ipite barabarani kwa ajili ya kupelekwa viwandani. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali iliangalie hili kwa jicho la pekee ili kusudi tuweze kupunguza zile ajali ambazo zinatokea mara kwa mara kutokana na yale mashimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye bajeti sasa. Niseme tu kwa kweli bajeti hii iliyowasilishwa ina ubora wa kipekee ambao hata wachangiaji waliopita wameweza kutaja na kikubwa zaidi ni uendelezaji wa miradi yetu mikubwa ya kimkakati. Kwa sababu hiyo nampongeza sana Mheshimiwa Mheshimiwa Mama Samia Suluhu, Mama yetu mpendwa, Rais wetu pamoja na Makamu wa Rais kwa ujumla na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi nzuri ambayo wanawafanyia Watanzania. Mungu wetu atusaidie kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ubora wa bajeti hii, ninachokiona kikubwa ni uhitaji zaidi katika kujitegemea. Nasema hivi kwa sababu moja, bado tuna mahitaji makubwa. Tuna mahitaji katika kuendelezaji wa miundombinu mbalimbali katika Sekta ya Afya, sekta ya elimu, sekta ya barabara na kadhalika. Hata hivyo, tuna uhitaji wa kuongeza mishahara kwa Madiwani na kwa Watumishi kwa ujumla kama Mheshimiwa Mama yetu alivyoahidi siku ya Mei Mosi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili ambalo nalisema, la kujitegemea, naomba kurejea maneno ya mpendwa wetu Hayati Mheshimiwa Benjamin William Mkapa ambaye alikuwa ni Rais wa Awamu ya Tatu, alisema maneno yafuatayo, naomba kunukuu: “Napenda kuwakumbusha kuwa njia ya maendeleo imejaa jasho na vumbi. Tuzingatie utamaduni wa kupenda kufanya kazi kwa bidii, maarifa, ubunifu na kujituma. Lawama ni tamu ikitoka mdomoni, lakini peke yake haitapeleka mkono kinywani; na katika kila mfanyakazi akumbuke kuwa muhimu siyo muda anaoutumia kufanya kazi, bali kiasi cha kazi anayoweza kufanya katika muda aliopewa.” mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa hapa mimi niseme ni bidii, maarifa, ubunifu na kujituma. Kimsingi tukiyatekeleza haya, jibu la kwanza la kutupeleka kwenye kujitegemea litakuwa ni maendeleo ya viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo Blueprint ambayo ipo tayari, ilitengenezwa tangu mwaka 2018. Hii ingetusaidia sana katika uwekezaji kwenye sekta mbalimbali. Inazungumzia hasa taratibu za kuwezesha kuharakisha uwekezaji ili kufikia Tanzania ya Viwanda. Hata hivyo, ukiangalia utaona tunasuasua na ninyi ni mashahidi. Hata wale wawezeshaji waliokuja Jumamosi wakatupa semina walisema kwenye viwanda tunakwenda katika pace ndogo sana. Sasa naomba tujiulize, tumekwama wapi? Nami naomba tu sasa tuombe Mungu wetu atusaidie ili tutoke hapo na kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ina viwanda 35 vya korosho vyenye capacity ya kubangua tani 50,000 kwa mwaka. Pamoja na kupewa fursa ya kununua malighafi katika minada ile ya awali, wenye viwanda hivi wamekuwa wakibangua chini ya asilimia 10 tu ya korosho yote ambayo inazalishwa katika nchi yetu. Tuseme kwa mfano kama mwaka 2020 korosho iliyozalishwa ilikuwa zaidi ya tani 200,000, ilikuwa ni tani kama 210,000 hivi, lakini ubanguaji haukufikia hata tani 20,000. Kwa hiyo, hii ni below 10%. (Makofi)

Mheshimwa Mwenyekiti, sasa ukiangalia tena utaona kwamba kuna baadhi ya wenye viwanda walinunua korosho ghafi na wakaiuza nje korosho ghafi badala ya kupeleka kubangua; na kuna baadhi ya viwanda havikubangua hata kilo moja ya korosho. Sasa nashauri tu tuongeze viwanda vya korosho hapa nchini viende sambamba na ongezeko la uzalishaji; tusiache ikawa ongezeko la uzalishaji wa korosho ni kwa ajili tu ya kusafirisha nje. Hata hivyo, tuondoe vikwazo ambavyo vipo katika ubanguaji wa korosho na kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna gesi asilia. Sasa sina hakika kama kweli haina sulphur hii gesi asilia. Nashauri kama kweli kuna sulphur ya kutosha, basi tuitumie hii viwandani ili iweze kuzalisha sulphur kwa ajili ya mbolea na viuatilifu. Kwa sababu mwaka huu tumenunua sulphur ambayo ni takribani shilingi bilioni 25,000/= na kila mwaka tunanunua sulphur kutoka nje. Kwa hiyo, inaweza ikatusaidia, tukianzisha viwanda vitatumia hii sulphur kutokana na gesi asilia tuweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo fursa nyingi sana. Kwa mfano, mikoa hii ya Dodoma na Singida tuna ubuyu ambao uko porini. Hatuupalilii, hatupulizi dawa; tuna ukwaju, hatuupalii, hatupulizi dawa; lakini tunaona wenzetu wa Uarabuni wanatutumia hapa tende zimekuwa packed vizuri sana. Niseme tu, ubuyu una matumizi mengi zaidi ya 300 na kikubwa katika afya. Una vitamini C nyingi sana. Tunapoenda hospitali wagonjwa wa Corona tunapewa Vitamic C tunamung’unya, lakini hata ukimung’unya ubuyu, gram 20 ambayo ni vijiko viwili tu vya unga wa ubuyu, tayari ni zaidi ya 58% ya daily recommended allowance ya vitamin C. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekti, ubuyu na ukwaju unasaidia sana kukinga magonjwa ya kansa, inasaidia sana pia kupunguza risk za maradhi ya moyo na matunda haya pia yanasaidia kuimarisha mifupa. Hata kwa wazee ni matunda mazuri sana. Kwa hiyo, kimsingi tufanye tu value addition, tuweke viwanda vya kusindika ubuyu na ukwaju kwa sababu kazi yake wala siyo ngumu kiasi kile, ni sawasawa na wanavyofanya wenzetu katika tende.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie kidogo.

MWENYEKITI: Malizia.

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri tu sasa kwamba tulinde mapori yetu tusichome moto ovyo, tusikate miti ili kusudi huu ubuyu na ukwaju uendelee kutusaidia. Pia hata watafiti waangalie namna gani ambavyo tunaweza tukaitunza katika kufanya uzalishaji wa kitaalam tuweze kuendelea kuyapata. Kwa kifupi kabla sijamaliza, niseme tu, tukianzisha viwanda vingi tutaongeza ajira na hasa kwa akina mama na vijana ambazo zitatupunguzia umasikini wa mtu mmoja mmoja lakini pia zitaongeza pato la Taifa kwa sababu viwanda vitalipa kodi ya mapato na VAT. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na nimeshamaliza. Nashukuru sana. (Makofi)