Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya siku ya leo, nianze mchango wangu kwa kutoa shukrani za dhati kabisa kutokana na ile kauli ya Waziri Mkuu aliyosema msimu huu wa korosho korosho zote zitasafiri kupitia bandari ya Mtwara. Watu wa Mtwara, watu wa Kusini tunajua na tunathamini mchango huo kwa sababu tunatambua ni nini kinakwenda kutokea, hicho kilikuwa ni kilio chetu cha siku nyingi ndani miaka mitano korosho zilikuwa zinasafirishwa nje ya bandari ya Mtwara hivyo kusababisha mambo mengi ya kiuchumi kusimama Mtwara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kama korosho zitasafiri kupitia bandari ya Mtwara tunategemea watu wenye maghala watakodisha pale, tunategemea wafanyabiashara wadogo wadogo, mama lishe, wanawake wenzangu mimi Tunza, watafanya biashara pale na mambo mengine yatakwenda kuwa sawasawa. Nishauri bandari ile isiishie kutumika kwenye zao la korosho tu itumike pia kwenye mazao mengine na kwenye shughuli nyingine, kwa sababu Serikali imewekeza pesa nyingi pale ambazo ni kodi za Watanzania hivyo ikiendelea kutumika tunasema ile value for money itaonekana pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe shukrani za dhati kwa hilo na naiomba Serikali iondowe zile changamoto za makontena za tozo kubwa kubwa ili kusudi ivutie wafanyabiashara waje kuitumia bandari ya Mtwara nasi watu wa Kusini Watanzania halisi tupate kunufaika na hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo kwenye zao la korosho naiomba Serikali iangalie kwa undani suala la pembejeo kumekuwa na malalamiko mengi kama tunaenda kutumia bandari basi pembejeo nazo zipelekwe kwa wakati na kwa ubora na kwa uwingi unaotakiwa ili kusudi watu walime wapate korosho nyingi ili ile bandari inayokwenda kutumika sasa ipate manufaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungumzie kidogo TRA, unapotaka kupata pesa ni lazima uwekeze, usitegemee kupata pesa bila kuwekeza. Naishauri Serikali kama kuna mtu anakwenda TRA ukabahatika kufika na ukahudumiwa na mfumo bila kuambiwa mfumo, sijui mtandao uko chini, mtandao unasumbua, mtandao unafanya nini, ni bahati sasa Mheshimiwa Waziri wa Fedha hili ufanya maendeleo ni lazima upate pesa. Waliopewa dhamana kukusanya pesa ni TRA sasa tunaomba mboreshe mfumo wa TRA ili kusudi mtu ukitoka nyumbani siku hiyo, maana yake nisiwaambie kulipa kodi nako ni moyo, mtu ametoka nyumbani amebeba pesa yake anatamani aende TRA akalipe kodi anafika pale anaambiwa mfumo haufanya kazi, akirudi nayo ile pesa nyumbani hatuna uhakika kama kesho atarudi tena kwenda kuufuata mfumo unafanya kazi ama haufanyi kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naiomba Serikali kwa moyo wa dhati kabisa wekezeni kwenye mifumo hii inayotumika kukusanya mapato ili kusudi mtu anapoamua kwenda kulipa akifika pale alipe aondoke. Uwe ndiyo mfanyabishara hawezi kutamani kufika TRA akae masaa matatu, manne matano mwisho wa siku unamwambia mfumo haufanyi kazi akirudi nyumbani ile pesa anaingiza kwenye mzunguzuko wewe Serikali unakuwa hujapata chochote. Mkaimarishe kwenye vitengo vyote hata kule LATRA nako pia kuna usumbufu wa mtandao ukienda inawezekana usipate huduma, mitandao yetu haijakaa sawa sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wananchi watalipa kodi kwa hiyari wakiona maendeleo. Mfano watu wa Mtwara tumekuwa tukilia kila siku kuhusu ile barabara ya kutoka Mtwara Mjini inayopita Nanyamba, Tandahimba, Newala, inakwenda Masasi, kilometa 210 tu zimezungumzwa na Wabunge waliopita sisi wengine tumeingia hiki ni kipindi cha pili tunazungumza mpaka leo mmejenga kilometa hamsini, hivi kilomita 210 kwenye eneo ambalo zinatoka korosho! Korosho hizo zinazochangia Pato la Taifa la nchi hii kwa kiasi kikubwa kilomita 210 just kilomita 210 zinawashinda kitu gani, twendeni mkatutengenezee hizi hili na sisi tutakapokuwa tunalipa kodi tulipe kodi kwa kujivuna kabisa kwamba tunalipa kodi na maendeleo tunayaona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukienda kule Mtwara katika Mikoa inayoongoza ukosefu wa maji ni pamoja na Mtwara, mkatutekelezee mradi wa maji ya kutoka Mto Ruvuma ili tunapolipa kodi tujue kodi zetu zinatumika kutuletea maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda katika hii miradi ya REA kama kuna mkoa umefanya vibaya kwenye miradi ya REA ni Mkoa wa Mtwara, kuna vijiji vingi havina umeme tunashukuru Mheshimiwa Waziri wa Nishati alituita sisi Wabunge wa Mtwara kutuhakikishia kwamba Wakandarasi ambao wamekwenda safari hii watakwenda kufanya vizuri. Tunaomba msituache nyuma kila kitu, ukienda maji tatizo Mtwara, umeme Mtwara, barabara Mtwara tunaomba muende mkatutekelezee na hospitali ya Kanda ya Kusini tunaomba iende ikafunguliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatamani tupate huduma tukiwa kwenye Kanda zetu wala siyo lazima tufike Muhimbili, kule kukiwa kuko poa tutaishia huko huko ingawa huku kwingine tutakuja kufanya mambo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nishauri kwenye issue za fursa za mapato, mimi nimekuwa kwenye Kamati mbalimbali, Wakurugenzi wanapokuja kwenye Kamati tunawashauri mkatafute vyanzo vipya vya mapato, mimi naishauri Serikali kuwe na kitengo maalum chenye wataalam wa kuweza kufanya utafiti, analysis ya kutosha kujua kwa mfano ukienda Mkoa wa Mtwara Halmashauri fulani inaweza ikawa na fursa ya mapato moja, mbili, tatu, wawashauri wale halafu yale malengo yanayowekwa yale, wale Maafisa Mipango wetu yule mtu atakayefanya vizuri basi aonekane amefanya vizuri amefikia malengo na yule ambaye ajafanya vizuri aambiwe ajafanya vizuri na pia kuwe na training. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua mimi tatizo lingine ninaloliona sijui kwa sababu ni mwalimu huwa naona kama wafanyakazi wengi wa Serikali wakishaajiriwa hakuna mafunzo kazini, wakati mambo yanabadilika, mambo hayako vilevile watu wanatakiwa wapewe mafunzo waambiwe sasa hivi kama nchi tunaelekea huku tunaomba mfuatilie moja mbili tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, mimi Tunza ukiniuliza fursa ambazo zinaweza zikapatikana Mkoa wa Mtwara naweza nikakuambia tuna fursa ya gesi ule mradi wetu wa LNG ufanyiwe kazi, tuna fursa ya korosho lakini kwa masikitiko makubwa nakuambia hakuna kiwanda chochote cha maana kinachofanya kazi ya ubanguaji. Hizo ndiyo fursa tuna bahari hatuna bandari ya uvuvi, hatuna meli, hatuna viwanda vya samaki pesa tunazitoa wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliambiwa kiwanda cha mbolea mpaka leo hatukioni hizi ndio fursa za mapato ambazo mimi ukiniuliza layman tu ambaye sijui uchumi naweza nikakuambia, Wachumi wetu watushauri vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie jambo moja hili ni ombi kwa Serikali, katika Manispaa ya Mtwara Mikindani kuna mgogoro unaendelea kati ya wafanyabishara wadogowadogo ambao walikuwa wanafanya biashara soko la sabasaba Serikali imejenga soko zuri na soko la kisasa, wafanyabiashara walizoea kufanya biashara kwenye hilo soko la sabasaba sasa hapa pana mgogoro, wale wafanya biashara ni wafanyabiashara wadogowadogo, wengine ni wanawake wana mitaji midogo naomba Serikali iangalie suala hili kwa busara zaidi kuliko kutumia nguvu. Waone ni namna gani ya kukaa na hawa wafanyabiashara ili kusudi wafanye biashara zao kwa amani watumie lile soko letu la kisasa ambalo limejengwa lakini waangalie na huku wanawaachaachaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha nakuuliza swali langu la mwisho ile issue yetu ya export levy kutoka kwenye zao la korosho unatuachaachaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. (Makofi)