Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Aloyce John Kamamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buyungu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuchangia kwenye Wizara hii ya Fedha; na kwanza kabisa naunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya ya kutuongoza Watanzania, na kwa uchapaji kazi wake; na kwa hakika anavyochukua hatua kwa haraka sana katika masuala ya Kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwapongeze Mheshimiwa Waziri, rafiki yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu, na Naibu wake, rafiki yangu Mheshimiwa Eng. Masauni. Kwa kweli mnachapa kazi vizuri, mnasikiliza, mnafuatilia na mwisho mmekuja kutoka na bajeti ambayo ni shirikishi. Mmewakiliza Wabunge wote mkafuatilia changamoto zinazowakabili katika maeneo yao na mwisho bajeti hii ambayo mmeitoa ni bajeti shirikishi inayojibu matatizo ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya kuchangia ni mengi lakini nitachangia katika maeneo machache na yale ambayo yametolewa na wenzangu kuhusu vyanzo vya kodi na taratibu zake, ulipaji wa madeni ya posho kwa Madiwani, na yote ambayo yamechangiwa na wenzangu, naomba sana myazingatie na myafanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitachangia maeneo machache na moja nitachangia sana katika eneo la ukamilishaji wa miradi. Ipo miradi mbalimbali, miradi ya kimkakati. Wakati nachangia mara yangu ya kwanza kabisa Bungeni, hoja yangu ya kwanza ilikuwa ni ukamilishaji wa miradi ambayo imeanzishwa. Ipo miradi kama reli ya kisasa (SGR), ununuzi wa ndege, ufufuaji wa viwanda, miradi ya umeme hasa Mradi wa Mwalimu Nyerere na ukamilishaji wa shughuli mbalimbali hasa katika jimbo langu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jimbo langu tuliahidiwa kama ambavyo wenzangu wamezungumza, lami ya kilometa tatu na pale tayari kuna milioni 75 pale kwa ajili ya ujenzi wa barabara. Fedha zipo pale, lakini katika ujenzi ule imepelekea mradi ule kifusi kijazwe katika barabara na kwa maana ile hakuna shughuli za biashara zinazofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mazingira yale hata Serikali sasa inakosa kodi, biashara haifanyiki na kwa kuwa haifanyiki wananchi wale hawawezi kulipa kodi kama inavyostahili. Niombe sana Mheshimiwa Waziri apeleke fedha za kukamilisha mradi ule ili wananchi wafanye biashara na sisi kama Serikali tuweze kupata kodi. Hii inakwenda sambamba na umaliziaji wa barabara kama ambavyo nimezungumza ni umaliziaji wa miradi. Kuna barabara inayotoka Kankoko kwenda Kinonko kwenda Nyakiyobe kwenda Ngwarama, kwenda Kabare na kufika kwenye mpaka wa Muhange. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hilo limejengwa soko kubwa, kuna milioni 585, majengo yamekamilika, lakini hatuyafaidi vizuri kwa kuwa hakuna barabara inayokwenda pale. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri katika bajeti hii kwa kuwa ndio anamalizia malizia atenge fedha za kumalizia barabara ile ili soko liweze kufanya kazi na sisi ile biashara ya mpakani tuweze kupata kodi. Kwa hiyo ni kuweka fedha, lakini wakati huo huo Serikali nayo itapata fedha kupitia mpaka ule kupitia kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo; katika nchi yetu kilimo kinatoa ajira katika eneo kubwa sana, lakini yapo mambo ya kufanya. Moja; ni kuajiri watenda kazi, hatuna Maafisa Kilimo kwenye vijiji. Naomba sana katika bajeti hii Mheshimiwa Waziri anapohitimisha aangalie makandokando, vifedha vichache vinavyobaki, basi aweze kupeleka fedha kwa ajili ya ajira ya watumishi katika Sekta ya Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inakwenda sambamba na watalaam kupima udongo. Kwenye kilimo ni sehemu ambayo ajira inafanyika kwa ukubwa sana, lakini wananchi wetu ili mradi anaona ardhi hajui ardhi ile inafaa kwa zao gani, analima tu. Niombe taratibu zifanyike, ardhi ipimwe, ionekane inafaa kwa zao gani, ndipo wananchi waweze kulima pale. Hii iende sambamba na uongezaji wa thamani ya mazao kwa maana ya kupeleka mashine za kuchakata mazao mbalimbali kama muhogo, mahindi na kadhalika ili mazao yetu yaweze kuongezewa thamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pembejeo ni muhimu sana kwenye kilimo, lakini hazipelekwi kwa wananchi kama inavyostahili. Hii inakwenda sambamba na mbolea, lakini kuna suala la dawa, wananchi wanaanza kilimo bila mbolea, inafika muda ambao mbolea ingeweza kutumika kwa ajili ya kumfanya mwananchi alime vizuri hawezi kulima vizuri kwa sababu hana mbolea. Kwa hiyo mbolea ipelekwe, lakini dawa vilevile ziweze kupelekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika wilaya ambayo natoka Wilaya ya Kankoko ili kumbukumbu ziwepo, ni katika wilaya ambayo tunalima sana zao la alizeti. Kwa hiyo wakati inaandaliwa mipango mbalimbali kwa ajili ya kilimo cha alizeti, basi Wilaya ya Kankoko nayo iangaliwe na iwekwe kwenye mikakati. Hii inakwenda sambamba na Mkoa mzima wa Kigoma ambao zao letu ni chikichi, tuongezewe nguvu ya kutosha ili zao hili la chikichi liweze kulimwa kwa kiwango kikubwa na kujibu changamoto ya mafuta ambayo inakabili nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni pamoja na zao la miwa ambalo kwa kipindi kirefu limezungumzwa katika Mto Malagarasi, eneo lile ni zuri sana na linafaa kwa kilimo cha miwa. Niombe nalo katika mkakati wa jumla kuongeza uchumi wa nchi liweze kuwekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la elimu, tumefanikiwa sana kwenye upande wa elimu, lakini Walimu hawatoshelezi. Kuna idadi ya Walimu imetajwa ya 6,000, hawa hawatoshi. Niombe katika mkakati wa jumla walimu waongezwe ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za Walimu kwa sababu wanakaa mbali ikiwa ni pamoja na kujenga madarasa hasa mwishoni mwa mwaka inafika hatua sasa ni kukimbizana. Inafika hatua Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa hawawezi kwenda likizo kwa sababu wanatakiwa sasa wasimamie ujenzi wa madarasa. Naomba sana madarasa haya yajengwe mapema ili wanafunzi nao wawe wamejiandaa vizuri kwa ajili ya kuanza masomo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa mabweni kwa ajili ya wasichana; watoto wa kike wana changamoto nyingi pamoja na kwamba na wa kiume nao changamoto nyingi. Sasa niombe Waziri wa Elimu akisaidiana na TAMISEMI na Wizara ya Fedha kama ambao wanashikilia kihenge kikuu, waweke mkakati wa makusudi kujenga mabweni hasa maeneo ya vijijini ili watoto wetu wa kike waweze kupata sehemu ya kuishi vizuri na waweze kusoma, watumie muda mwingi kusoma badala ya kutumia muda mwingi kukimbizana na changamoto ambazo zinawakabili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii iende sambamba na ukamilishaji wa maboma ya maabara, maboma ya madarasa pamoja na maboma ya nyumba za Walimu. Naomba sana Serikali ichukue hatua ya makusudi ili kukabiliana na changamoto hizi na nina hakika watoto wetu watasoma vizuri na wataweza kukabiliana na changamoto ambazo zinawakabili na mwisho elimu itaweza kuwafikia vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwangu nilitaka nichangie hayo, lakini yachukuliwe kwa ujumla wake ili kufanikisha maeneo yote kukamilisha miradi kwa wakati, lakini kuongeza nguvu katika madarasa na nyumba za Walimu ambazo zinajengwa katika shule zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)