Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Dr. Alfred James Kimea

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Korogwe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, lakini napenda tuweke taarifa sahihi, jina langu ni Alfred Kimea na sio Kimei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa hii nafasi, wenzangu wameongea mengi. Ukianza kufuatilia utaona kila mchango ambao unatakiwa kwenda kwa Wizara hii kwenye hii Bajeti Kuu ya Serikali, imeshaongelewa. Napenda tu niongezee machache na sehemu nyingine niongezee ambapo palishaongelewa kwa sababu mengi yameshaongelewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza napenda kumshukuru Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya. Tusiposhukuru kwa kazi kubwa anayoifanya, tutakuwa hatumtendei haki mama huyu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi kichache tangu tuwepo Bungeni mambo makubwa, aidha yameshafanyika au tumepewa ahadi kubwa kwa ajili ya kuendeleza majimbo yetu. Mfano tu kwenye jimbo langu la Korogwe Mjini, kwa kipindi hiki kidogo tumeshaandaliwa zaidi ya shilingi bilioni mbili kwa ajili ya sekta ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo langu ni la Korogwe Mjini, kwa kipindi hiki kidogo tumekwisha kuandaliwa zaidi ya bilioni mbili kwa ajili ya sekta ya maji. Sekta ya barabara ikiwemo TARURA tuna bajeti ya karibu 1,300,000,000 kwa hiyo, hii ni kitu kikubwa ni lazima tumshukuru Mama kwa kazi kubwa anayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwenye bajeti sasa, mchango wangu utakuwa wa sehemu mbili, moja nitapongeza lakini sehemu ya pili nitashauri sehemu chache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa pongezi kwa kweli tunamshukuru na tunampongeza kweli Waziri, wetu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu pamoja na kaka Mheshimiwa Engineer Masauni kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa kutuletea hii bajeti nzuri. Kwa kweli ni bajeti nzuri ambayo inatakiwa kupongezwa na ninazo sababu ya kupongeza hii bajeti siyo tu kama nafuata mkumbo wa watu wameipongeza bajeti na mimi nipongeze lakini ninazo sababu kabisa za msingi kwa ajili gani naipongeza hii bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kwanza ni kweli hii bajeti imekwenda kumgusa kila mtanzania. Kila Mtanzania ameguswa kwenye hii bajeti kuanzia wafanyakazi tumeona wanakwenda kupandishwa vyeo na hii tuliipigia kelele sana mimi nilikuwa mmoja wapo nilisema walimu hasa wa vyeo vikuu ambao mimi nilitoka huko nilikuwa mmoja wao walikuwa wanastahili kupandishwa madaraja lakini kwa muda mrefu hawakuwa wanapandishwa madaraja. Lakini hii bajeti sasa imekuja na dawa hiyo; walimu wa Vyuo Vikuu wanakwenda kupandishwa madaraja. Kwa hiyo, tunampongeza sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu kwa ajili ya kuona hiki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia bajeti hii imegusa au imezingatia maoni ya Wabunge na Wadau wengine wengi. Hajakaa tu chini kuandaa bajeti, hajachukua template za bajeti zilizopita, amekaa chini kuangalia Wabunge waliongea kitu gani, alikaa chini kuangaliwa wadau wanazungumza kitu gani akaja na bajeti nzuri ambayo imezingatia maoni ya watu hao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulishauri juu ya TARURA kuongezewa bajeti na kweli TARURA imekwenda kuongezewa bajeti. Tulishauri Wizara ya Afya iongezewe bajeti na wamefanya hivyo. Tulishauri miradi mikubwa iende kufanyika na kweli wanakwenda kuiendeleza ile miradi mikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ndugu yangu Mheshimiwa Waziri kwa kuwa umesema unakwenda kufanya vitu hivyo, kweli tunataka hivyo vitu vikafanyike. Mfano mmojawapo; tunakwenda kushika kodi kwenye line za simu na tunakwenda kuchukua kodi kwenye mafuta na alisema specific kwenye mafuta shilingi 100 inakwenda TATURA na kwenye line inakwenda kwenye huduma za afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania siyo watu wajinga, wanakwenda kuhesabu kitu gani kinakwenda kupatikana na kitu gani kinakwenda kufanyika. Kwa kuwa ulisema specifically hii inakwenda kwenye afya kweli tunataka iende kwenye afya. Tumesema hii inakwenda TARURA kweli tunataka hii iende TARURA. Kwa hiyo, tunakupongeza lakini tunataka kweli ahadi yako uende kuitimiza kwa ajili tuna mwaka mmoja tu, mwakani siku kama hizi tutarudi tena tukikupitishia bajeti nyingine tunataona hiki kitu umekifanya kwa namna gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sehemu nyingine ya mwisho, kwa ajili gani naipongeza hii bajeti kama kauli mbiu ya nchi yetu ni kuinua uchumi wa viwanda ni kweli bajeti hii imeonesha dhamira yake ya kwenda kuinua uchumi wa viwanda. Tumeona wakipunguza baadhi ya ushuru wa forodha kwa bidhaa ambazo zinakwenda kutumika kwenye viwanda vyetu. Lakini pia wameongeza ushuru wa forodha kwenye bidhaa ambazo zinatengenezwa Tanzania ili kuweza kuinua sekta ya viwanda kwenye nchi yetu. Kwa hiyo, tunaipongeza bejeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema mchango wangu utakuwa na sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni pongezi ambayo nimekwisha kutoa lakini sehemu ya pili ni maoni yangu kwenye baadhi ya maeneo machache ambayo naona yanahitaji kufanyiwa marekebisho. Ya kwanza, nitoe maoni yangu kwenye hii sheria ya kodi ya majengo. Kweli Mheshimiwa Waziri nakupongeza kwa hii kodi mpya au namna ya utozaji wa hii kodi mpya. Kama tunavyofahamu ni kweli kodi yoyote ambayo inaanzishwa ni lazima iwe nyepesi kukusanya. Kweli nakupongeza hii kodi ambayo umeianzisha itakwenda kuwa rahidi kukusanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kodi mpya inayoanzishwa ni lazima iwe na urahisi wa kulipa. Ni kweli walipo kodi wetu itakuwa rahisi kuilipia hii kodi ya majengo kuliko mwanzo ilivyokuwa. Lakini kuna principle nyingine ya kodi inaitwa principle diversity kwamba mtu yoyote ambaye anakusudia kulipa hii kodi kweli anatakiwa kulipa hiyo kodi na kweli kodi hii itakuwa vigumu sana kwa mtu yoyote ambaye kakusudia kulipa kukwepa kodi hii. Kwa hiyo napongeza kwa jitihada hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti kodi hii inachangamoto kidogo ambazo kidogo ambazo lazima Mheshimiwa Waziri waweze kuzi-address. Ya kwanza tunafahamu kodi yoyote kuna principle muhimu sana ambayo hii kodi inakwenda kinyume na principle hiyo. Principle ya Equity, kwamba watu wenye kipato sawa waweze kulipa kodi sawa; lakini watu wenye vipato tofauti basi kodi iwe tofauti, mwenye kipato kikubwa alipe kodi kubwa na mwenye kipato kidogo alipe kodi ndogo. Lakini Mheshimiwa Waziri utakubaliana na mimi kabisa kwamba kodi jinsi ilivyo wewe Mheshimiwa Waziri utakwenda kulipa shilingi 1,000 kwa mwezi, na yule bibi yetu kule nyumbani kwetu kwa Mndolwa, kule nyumbani kwetu Old Korogwe naye atakwenda kulipa sawasawa na wewe ulivyolipa. Hii siyo sawa kabisa Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo, lazima hii kodi ije itengenezwe namna kwamba mwenye kipato kikubwa atalipa kodi kubwa na mwenye kipato kidogo atalipa kodi ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, madhara ya hiki, moja itawadhulumu wale watu wanyonge; lakini namba mbili Serikali haitakusanya mapato yake sahihi kwa ajili mtu mwenye kipato kikubwa atalipa sawa na yule mwenye kipato kidogo. Nini kifanyike; maoni yangu, nadhani haya yataondoa ile shida ambayo Wabunge wengi wameiongea. Maoni yangu ni kwamba kwanza assumption zangu ni kwamba mtu ambaye anatumia unit nyingi atakuwa na kipato kikubwa kuliko mtu anayetumia unit ndogo. Sasa kwa namna gani mtu mwenye kipato kidogo atalipa kidogo na mwenye kipato kikubwa atalipa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, badala ya kusema unashika kodi shilingi 1,000 kwenye Luku achana na hiyo, shika kutokana na matumizi ya Unit, badala ya Luku shika hiyo kodi kwenye unit mtu anazotumia. Ukifanya hivyo Mheshimiwa Waziri; moja mtu mwenye kipato kidogo atalipa stahiki yake, mwenye kipato kikubwa atalipa stahiki yake. Namba mbili, ile issue ya maghorofa mtu ana ghorofa ngapi? Mtu ana apartment ngani, hiyo hutaizingatia tena kwa ajili mtu mwenye kikubwa atatumia sana na alipa kodi kubwa na mtu mwenye kanyumba kadogo atalipa kidogo. Kwa hiyo nashauri badala ya kukatwa hiyo kodi kwenye mita ikatwe kwa Unit jinsi mtu anavyotumia. Huo ndio ushauri wangu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kodi nyingine ambayo napenda kushauri kidogo ni tozo kwenye line za simu. Kengele ya kwanza naamini. Tozo kwenye line ya simu. Mheshimiwa Waziri, hapa tozo kwenye line ya simu lazima uwe clear hii kodi inakwenda kushikwa kwenye nini; kwa ajili kila kodi mpya inayoanzishwa lazima tujue base ya hiyo kodi ni kitu gani? Aidha, unakwenda kushika kodi kwenye line ambayo siamini kwamba umiliki wa line unaweza kumshika mtu kodi au unakwenda kushika kodi kwenye matumizi ya muda wa maongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama ni kwenye matumizi muda wa maongezi ile item uliyoisema kwa siku itakuwa siyo muhimu. Kama unakwenda shika hii kodi kwenye muda wa maongezi kuna mtu anaweza akaongeza muda wa maongezi mara kwa wiki, mwingine akawa anamiliki line tu lakini haongezi muda wa maongezi. Kwa hiyo ukisema unamshika ile kodi kila siku hutakuwa umemtendea haki. Kwa hiyo, naamini watakaoshika hii kodi per muda wa maongezi na pia inatakiwa um-charge mtu kwa jinsi anavyoongeza muda wa maongezi. Kwa hiyo, hayo ndio maoni yangu, naomba kodi hizo zifanyiwe kazi ili kodi zetu ziweze kuleta tija zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini cha mwisho kama muda upo, naomba nishauri kwenye ushuru wa forodha kwenye mafuta. Kweli Mheshimiwa Waziri naamini kabisa kodi hii ni kwa ajili ya kulinda viwanda vyetu lakini sasa hivi Tanzania bado tuna deficit ya mafuta. Kwa hiyo, kodi ni nzuri lakini ninachoona timing bado. Tuhimize watu wetu wazalishe mbegu za alizeti pale tutakapokuwa tuna-produce zaidi hapo ndio tuanze ku-protect hatuwezi kuanza ku-protect kitu ambacho hatunacho bado. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kodi hii ni nzuri na ninaiunga mkono lakini nahisi timing bado sasa hivi mahitaji ya nchi yetu ni karibu tani za ujazo 500,000, zaidi ya 500,000 lakini tuna produce 200,000 tu. Kwa hiyo, tukienda ku-protect sasa hivi kitu ambacho hakipo bado haiingia akilini kwa hiyo naomba tuwahimize watu wetu na tutakapokuwa tunazalisha zaidi hapo ndipo tutakapokuwa na nafasi ya kuweza kulinda viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa muda huu, naunga mkono hoja, mungu awabariki sana. (Makofi)