Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Ndaisaba George Ruhoro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ngara

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. NDAISABA G. RUHORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba ya bajeti, awali ya yote napenda kuanza kumshukuru na kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi mzuri ambao ameuonesha tokea awe Rais wetu na kwa kazi nzuri sana ambayo anaendelea kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya muda mfupi Mama Samia ameonyesha uongozi mzuri uliotukuka na jamii ya Kimataifa imetambua kwamba Tanzania tuna Rais kweli kweli Rais Mama. Vilevile, napenda niweze kuwapongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na Naibu Waziri wake na viongozi wengine wote wa Wizara, kwa kuweza kutuletea bajeti ya kisayansi kwenye Bunge letu hili. Bajeti ambao kwa kweli imegusa maeneo mbalimbali ya vipaumbele ya nchi, imegusa makundi mbalimbali kwa kweli mimi nina washukuru sana kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Ngara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili bajeti hii iweze kutekelezeka, ni wazi kwamba lazima tupanue wigo wa kodi na ni lazima maeneo yote nyeti ya makusanyo ya fedha yaweze kuboreshwa ili kodi iweze kukusanywa. Kwa minajili hiyo Jimbo la Ngara ni miongoni mwa Majimbo ambayo yamekaa kimkakati, Jimbo la Ngara linapakana na nchi mbili za Rwanda na Burundi na kutoka Ngara kwenda Goma - DRC ni kilomita 355 na kutoka Ngara kwenda Juba ni kilomita 1,094. Hivyo, tunao mwingiliano mkubwa wa maeneo yote haya na biashara ya mpakani kwenye Jimbo la Ngara imeshamiri kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vituo vya forodha vinavyotakiwa kufanya kazi kwenye Jimbo la Ngara ni vituo vinne lakini mpaka sasa ni viwili tu vianavyofanya kazi yaani kile cha Kabanga na kile cha Rusumo. Kulikuwa na kituo cha forodha cha Mgoma ambacho kilianza kufanya kazi miaka ya nyuma lakini baadae kituo hiki kilifungwa na TRA upande wa Tanzania waliondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wenzetu wa upande wa Burudni wamejenga jengo kubwa sana la kisasa, wameweka taasisi zao za mamlaka wa mapato pamoja na Uhamiaji kwa upande wa Burundi. Upande wa Tanzania, kuna mtaalamu alitoka TRA Makao Makuu wamekuwa wakienda pale Mgoma, kwenda kutembea, kwenda kufanya assessment na ripoti wanazoaifanyia assessment hazijawahi kutoka na kinachoendelea hatujui ni kitu gani. Nimuombe Mheshimiwa Waziri atoe maelekezo TRA, taarfia iliyoenda kuchukuwa pale itoke na kituo hiki kiweze kunya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kamati ya kushughulikia masuala ya magendo ya Mkoa inaitwa ‘fast’, kazi yake ni kwenda kukamata wafanya biashara ambao kwa kweli ule mpaka ni lazima wafanyabiashara wautumie kwa magendo, kwa maana ni ngumu mfanya biashara kusafiri zaidi ya kilomita 50, kwenda kutafuta huduma za forodha, wakati anaweza kupitisha kwenye njia za panya mzigo wake wa kilo 10 kilo 20 na akaweza kuupitisha. Hivyo badala ya kuhangaisha hawa wafanyabiashara, ninaomba sana Wizara ya Fedha na Mipango, iweze kutoa maelekezo kama zamani huduma ya forodha ilikuwepo, na kulikuwa na majengo ya kawaida yanayotumika na upande wa pili wa Burundi wapo tayari kwa ajili ya biashara mapakani sisi tunakwama wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri atakapokuwa ana-conclude, kwa kweli tunaomba uwatendee haki wananchi wa Ngara na wafanyabiashara wote kwa kuruhusu kituo hiki cha forodha cha Mgoma, kiweze kuanza kutoa huduma za forodha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande mwengine, tuna kituo kingine cha forodha cha Murusagamba, kilijengwa mwaka 1990, baadae kikaungua, mwaka 2016 kikajengwa upya baada ya kuwa kimeungua, baada ya hapo TRA Mkoa na TRA Ngara wakaomba kupewa namba maalum ya utambulisho wa kituo hicho yaani Identification Code Number. Tokea mwaka 2016 Mheshimiwa Waziri hiyo namba hatujapewa kwenye kituo chetu cha forodha cha Murusagamba. Kamishna wa TRA ameishikilia hiyo namba, nakuomba Mheshimiwa Waziri hiyo identification number ya kituo chetu cha forodha cha Murusagamba iweze kuletwa ili kituo chetu kianze kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na modem, ile modem ilichukuliwa kutoka kituo chetu cha forodha cha Murusagamba ikapelekwa Kerwa, ikatumika Kerwa na baadae ikachukuliwa ikapotelea hewani, mpaka sasa hivi modem yetu Mheshimiwa Waziri ya kituo cha forodha cha Murusagamba hatujui imepotelea wapi. Nakuomba Mheshimiwa Waziri, modem yetu irejeshwe kwenye kituo chetu cha forodha cha Murusagamba ili kituo hiki kiweze kuwa automated, kianze kusoma na wafanyabiashara waache kupata taabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfanyabiashara anapokwenda na gari lake la mzigo anafika Murusagamba analipaki pale, inabidi asafiri umbali wa kilomita 123 one way, kwenda kupeleka nyaraka zake zipigwe muhuri kwenye kituo cha forodha cha Kabanga na baadae arudi tena asafiri kilomita 123 jumla kilomita 246 kutafuta huduma ya forodha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekwamishwa na vitu viwili ambavyo ni identification number na hiyo modem, naomba utoe maelekezo hivi vitu viletwe ili kituo chetu cha Murusagamba kiweze kutoa huduma kwa ajili ya wananchi wa Jimbo la Ngara, kwa ajili ya wafanyabiashara na wakati huo huo kiweze kusaidia kukusanya mapato ya Serikali ambayo yanahitajika ili bajeti hii ulioileta Mheshimiwa Waziri iweze kutekelezeka katika kipindi chote hichi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niongelee eneo la urasimu lililokuwa likiwakumba wadau wa maendeleo hasa NGO. Kwenye ukurasa wa 29 wa hotuba ya bajeti Mheshimiwa Waziri ameonyesha bayana kwamba kumekuwa na ukiritimba kwa wadau wa maendeleo wanapokuwa wanaleta fedha zao kwaajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo wanakutana na figisu figisu kule Wizara ya Fedha na kulikuwa na sheria ambako inataka msaada unapokuja ndani ya nchi on entry ule msaada uweze kukatwa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka dunia ilikuwa inatucheka, kuna haja gani ya kukata kodi kwenye msaada unapoingia moja kwa moja pale BOT wakati msaada huo huo unaendelea kuukata kodi nyingine kama vile PAYE withholding tax na kodi nyengine baada ya msaada ule unapoingia kwenye matumizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ulimwengu mzima ulikuwa unatushangaa Tanzania, yupo mfadhili mmoja kwenye bajeti yake anatenga zaidi ya dola milioni 500 kuzisaidia nchi zinazoendela kama Tanzania, sisi na figisu figisu zetu tunaendelea nazo Kenya mpaka wakaongezewa fedha zetu zaidi ya dola milioni 200 wakapelekewa sisi tunaendeleza figisu figisu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye hotuba yako Mheshimiwa Waziri umeweka vizuri sana tunaomba futilia mbali hiyo sheria ambayo inasema tutoze kodi moja kwa moja on entry wakati fedha hizo zinaongeza wigo wa kodi kwenye Taifa letu. Nakuomba Mheshimiwa Waziri wala usipate kigugumizi, futilia mbali hizi sheria, watu wanatushangaa ule ni msaada! Mataifa ya nje yanatenga fedha zao kuja kutusaidi nchi zinazoendelea, tunakwenda kukata kodi ya moja kwa moja, wakati tunao uwezo wa kukata kodi hivyo hivyo tukaipata baada ya fedha hiyo kuingia kwenye matumizi. Kwa kweli hapa umeitendea haki nchi na Mheshimiwa Rais tunampongeza kwenye eneo hili, nenda futilia mbali hiyo sheria inayotaka tukate kodi kwa sababu imekimbiza wadau wetu wa maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalonapenda kuliongelea, ni mradi wa kielelezo wa Kabanga nikel ambao umeoneshwa ukurasa wa 16 wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Baba yangu alipozaliwa alikuta kuna kitu kinaitwa mradi wa Kabanga Nikel, akakua akamuoa Mama yangu wakanizaa na mimi, nami nimezaliwa nimekuta kuna mradi wa huu wa Kabanga nikel, mimi pia nimekua nimeoa na nimepata mtoto wa kwanza anaitwa Ndairagije nae amekuta kuna mradi wa Kabanga Nikel. Nimekaa nimepata mtoto mwingine anaitwa Irakoze naye amekuta kuna mradi wa Kabanga Nikel. Kwa upande wa Marais, amekuja Rais wa kwanza, wa Pili, wa Tatu, wa Nne, wa Tano na sasa hivi tunae Rais wa Sita naye amekuta mradi huu wa Kabanga Nikel mchakato unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba kwa kweli Kabanga Nikel wawezeshwe umeme upelekwe, leseni ya kuchimba haya madini itoke ili uwekezaji huu sasa Mama Samia anyanyue ngoma. Hii ngoma inanyanyuka na Mama Samia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wangu umeisha lakini ninaomba sana mradi huu hawa watu wapewe leseni ili uwekezaji uweze kuanza. Ahsanteni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga mkono hoja. (Makofi)