Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Conchesta Leonce Rwamlaza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kidogo katika hoja iliyo mbele yetu. Hoja ya Bajeti Kuu, Bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ni tafsiri ya pesa na mipango yetu. Tumepanga mipango sasa tunatafsiri mipango yetu katika pesa. Ili tuweze kusema kwamba, hii bajeti ni nzuri, tutaangalia pale itakapowagusa watu katika kuangalia matokeo yao. Siwezi kusema bajeti ni mbaya, nitakachosema ni kwamba, hii bajeti nitaweza kuona uzuri wake pale ambapo watu watakuwa wanaguswa katika makundi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mchango wangu nitauelekeza katika ustawi wa wazee kupitia bajeti hii. Bajeti inaenda kijinsia. Kwa hiyo, tunaangalia makundi mbalimbali ambayo yameguswa na bajeti vizuri; ukitazama wanawake, ukitazama vijana, wameguswa, lakini nimekuwa na mashaka kuhusu bajeti hii inavyowatendea wazee wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba, Serikali hii haijafanya vizuri sana katika ustawi wa wazee katika nchi yetu. Nasema hivyo kwa sababu gani? Kwanza, Serikali hii ilitengeneza Sera ya Wazee tangu mwaka 2003. Sasa ni miaka 18 hakuna sheria yoyote ambayo imetengenezwa ili kulinda sera hii ili wazee waweze kupata huduma zao kama sera inavyosema. Ukiisoma ile sera ina mambo kama 15 ambayo yanawagusa wazee ambayo ni huduma ya afya, matunzo kwa wazee, ushirikishwaji, uzalishaji mali, hifadhi ya jamii, mahitaji ya msingi, elimu na mambo mengine yako kama 15 ambayo yamegusa sera ya wazee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaangalia machache, kwanza nianze na huduma ya afya. Wazee wetu hawapati huduma ya afya vizuri katika nchi yetu. Katika bajeti nitajaribu kuonesha hapa kitu kilichosemwa na TAMISEMI kuhusu namna wazee wanavyohudumiwa, lakini ukitazama kwenye Bajeti Kuu n ahata kwenye bajeti ya Wizara ya Afya, hakuna mahali ambapo wametuonesha kwamba, wazee wanaweza kuingizwa katika bajeti hii ili tuweze kuangalia yaliyotajwa katika sera yao kama yanaweza kutimizwa, ili wao nao kama watu ambao wametumikia Taifa hili, kama watu ambao wamefanya uzalishaji, je, hii bajeti inawagusa ili waweze kustawi? Maana Serikali yoyote haiwezi kukwepa kuangalia ustawi wa watu wake, ni kitu cha msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye afya haitatekelezwa vizuri kwa sababu wazee walio vijijini hawaguswi na utaratibu mzuri wa kutibiwa kwa sababu, wao wanashindwa kutambulika kama wana miaka sitini na kuendelea. Kwa hiyo, kwao inawapa shida katika kupata matibabu na hata matibabu yanayotolewa, kwa mfano, halmashauri inawapa vitambulisho, ikiwapa vitambulisho yaani mimi niiteje, sijui niite concession au sijui niite nini? Labda niite ni exemption, inakuwa kama ni exemption kwa sababu hakuna sheria yoyote ambayo inamlazimisha mpeleka huduma na mtoa huduma kuhakikisha kwamba, anamsaidia mzee, hakuna kitu ambacho kinam-bound mtu kwamba, mimi nitatoa huduma kwa mzee kwa sababu kuna sheria fulani inanilazimisha kufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwa matunzo ya wazee. Wazee hawatunzwi vizuri katika nchi hii. Nakumbuka kipindi fulani Mheshimiwa, nani anakaa kule? Aliwahi kuchangia akasema itungwe sheria ya kulinda wazee, kama ambavyo wanawake wanatungiwa sheria, watoto wanatungiwa sheria, tunatungiwa sheria sisi wazazi kuwasomesha watoto na kuwatunza, ni kwa nini hakuna sheria ya kuwalazimisha watoto kutunza wazazi wao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichukue nafasi hii kumshukuru Rais wetu; alikutana na wazee akawaambia na amekuwa akiendesha kampeni, mimi nasikia tangazo kwenye redio, ambayo inasema wazee watunzwe ngazi ya jamii, ngazi ya familia, lakini kuna wakati mwingine Serikali inapaswa kuweka mkono wake pale ambapo wazee, watoto wao wanashindwa kuwatunza. Hebu tuyatazame makazi ya wazee, huwa natoa mfano mara nyingi, bahati nzuri Waziri wa Fedha anapita barabara hii ambayo tunapita kwenda Bukoba na hiyo ndio anapita kwenda kwake. Mheshimiwa Waziri aende pale Sukamahela, kuna kijiji cha wazee, lakini wazee wanashinda wamejianika juani pale wanaombaomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea ni nini na awamu ya kwanza ya Serikali ya nchi hii walitengeneza kijiji ambacho kilikuwa kina-accommodate wazee? Sasa hivi makazi ya wazee katika nchi hii hayapendezi, hawana vyakula, hawana magari, hawana matibabu. Kwa hiyo, naomba bajeti iwaguse wazee, hawa watu tuwatambue, mjue na ninyi ambao bado ni vijana mnakwenda kulekule, njia ni moja. Kwa hiyo, msije mkafikiri kwamba, ujana wenu hamtakuwa wazee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais ametuambia tuandae vizuri, tupange mapema namna ya kuzeeka kule mbele. Tukipanga vizuri hata ninyi ambao ni vijana mkiisaidia wazee kupanga humu ndani ya Bunge, tutahakikisha kwamba, na ninyi mkizeeka mtakuta mazingira ya kuzeeka ni mazuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho nataka kusema ni kwamba, baadhi ya wazee ni wazalishajimali, ni watu wazima, ni watu ambao bado wana nguvu. Kwa hiyo, wakitumika vizuri, wakasaidiwa wanaweza kusaidia na mchango wao unaweza kuendelea kuonekana. Nasema hivyo kwa sababu, wanawake, vijana, wana nafasi yao katika halmashauri. Wanawatengea pesa, lakini hakuna mahali popote katika bajeti hii walipotuonesha kwamba, wazee wanaweza kusaidiwa namna hii au wanaweza kukopesheka. Kwa hiyo, halmashauri, Serikali, imewaacha solemba, yaani imewaacha solemba huko, hawajulikani watapata wapi kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeenda katika kitabu cha TAMISEMI, wamesema wametambua wazee jumla ya 366,282; wanawake wakiwa 195,771 na wanaume wakiwa 170,481. Nikajiuliza je, hii Serikali inajua idadi ya wazee katika nchi yetu? Maana katika sera waliyounda wenyewe walisema wazee ni asilimia 10 ya population ya nchi. Kwa hiyo, kama tunajikadiria kufika milioni 60 ina maana wazee wako kama milioni sita. Je, wamewapangia nini? Waziri atwambie, sisi wazee ametupangia nini katika bajeti yake? Tunawakaribisha na wao waje huku tuliko sisi, je, wametupangia nini ndani ya bajeti hii? Hawajatugusa kabisa, gusa wazee. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema hivi kwa sensa ya mwaka 2022 ambayo inakuja mwaka kesho watusaidie sensa hii kutuonesha wazee ni wangapi? Wazee walio katika mfumo rasmi ni wangapi? Wazee wanaopata pension? Wakulima wale ambao wananyanyasika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wazee, humu wote ni wanasiasa wameenda kwenye kampeni nyumba hadi nyumba, wameona namna gani wazee wanavyoteseka nchini, wazee wanatupwa na watoto wao, Serikali imekaa kimya. Kwa hiyo, naomba Serikali katika jambo hili ihakikishe wazee wanapata huduma ya kutosha, wazee wanatambulika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha kusikitisha, hata wale wanaopata pension ambao wametumika katika nchi hii, miaka nendarudi wakifika wakati wa kustaafu hakuna anayewaangalia wanakaa miaka miwili, mitatu, minne, bila kulipwa mafao yao. Kwa hiyo, tunaona jinsi wazee katika nchi yetu wasivyoweza kuthaminiwa; ni kwamba, tuendelee kuwathamini na tuhakikishe wanapostaafu wapewe pension zao, lakini hata bajeti hii, kama sio mwaka huu basi mwaka kesho, Serikali ihakikishe kwamba wazee wanatunzwa, wanaangaliwa makazi yao, lakini pesa yao ionekane kabisa katika bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nije kwa watoto wa mitaani. Nigusie kidogo yote; swali ni moja au jibu ni moja kwamba watoto watunzwe kwenye familia. Nataka kuwaambia kwamba kuna familia ambazo zina matatizo kiasi cha watoto kulazimika kuingia mitaani. Kama ilivyo kwa wazee, inawezekana Serikali haijui kabisa hata watoto walioko mitaani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuionya Serikali hii kwamba kutojua na kutoshughulikia watoto wa mitaani tunalea mfumo wa ujambazi. Tunaulea sisi wenyewe, tusilalamike, kwa sababu hawa wanakaa mitaani, wanabaka, wanafanya ujambazi, lakini wanazaana. They multiply kwa hiyo, wanajenga kizazi cha aina fulani ambacho baadaye tusije kulalamika kule ujambazi umekua aah! Ujambazi haukui ni kwamba sisi na hasa Serikali imeshindwa au imewezesha mfumo wa kulea hicho kitu ukaendelea. Kwa hiyo, ni wajibu wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza kwamba sasa ifike mahali, Serikali ipange kiasi fulani kwa GDP, kama nchi nyingine wanavyofanya. Huwezi kufanikiwa kwa mwaka mmoja, lakini tuwe na malengo, tunaweza kutoa kiasi fulani by percentage katika GDP yetu, tunaweka kwa ajili ya watoto wetu na kwa ajili ya wazee. Nchi nyingine zimeweza kufanikiwa kufanya hivyo, ndiyo maana unakuta watoto wao wanalipwa na wazee wanalipwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sipendi sana na sisi Waafrika hatuko hivyo, kwamba wazee waende kulelewa katika nyumba za wazee, lakini ikilazimika kufanya hivyo, naomba Serikali isikwepe kufanya, ni wajibu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)