Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Anton Albert Mwantona

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rungwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nashukuru sana kwa kunipatia nafasi nami kuchangia katika Hotuba hii ya Bajeti ya mwaka 2021/2022 katika Bunge lako Tukufu. Pili, namshukuru Mwenyezi Mungu kutupatia afya ili nami niweze kuchangia katika hotuba hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongea kwa kifupi sana. Kwanza nianze kutoa shukrani zangu za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nilipokuwa nakwenda kwa mara ya kwanza kwenye kampeni, nimezunguka kwenye vijiji vyote 99 vya Rungwe, nimezunguka kwenye kata 29 zote za Rungwe, matatizo makubwa ya wananchi katika Jimbo langu ilikuwa ni barabara, maji, umeme na matatizo mengine madogo madogo. Matatizo makubwa ambayo wale wananchi walikuwa wakiniambia ukienda Bungeni ukatusemee ilikuwa ni hayo makubwa matatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwanza na barabara za vijijini. Tumerekebisha Mfuko wa TARURA, Serikali imerekebisha; tunakwenda kupata shilingi 100/= kwenye mafuta, kwa hiyo, tatizo la barabara nina uhakika linaenda kutatuliwa na hivyo kunirahisishia mimi maisha kama Mbunge wa Jimbo, kuwaambia na kuwanyooshea vidole kwamba Serikali yetu imefanya mambo haya, haya na haya. Pia nashukuru kwa kiasi kikubwa, kwa shilingi milioni 500 ambayo imepatikana kwa kila Jimbo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kampeni zangu nilizunguka nikakuta kuna kijiji ambacho hakina barabara ya kuunganisha. Nilipanda pikipiki mpaka kwenda kupiga kampeni kwenye Kijiji hicho; kinaitwa Kijiji cha Kikole. Ni kilometa 12 kutoka kwenye mji ambao unapitika unaitwa Masukuru mpaka Kikole mpakani na Kyela. Napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu hili kwamba hiyo fedha tumeielekeza huko na wananchi wa Kikole niwaambie, mama amesikia kilio chenu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba amesikia kilio chenu na Serikali ya Chama cha Mapinduzi imesikia kilio chenu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru sana Serikali, namshukuru sana Waziri wa Fedha, nashukuru sana Baraza la Mawaziri ambalo limefikiria kupeleka hii shilingi milioni 500 kwenda kuwasaidia wananchi katika maeneo ambayo yapo katika taabu kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa maji, pia tulikuwa na tatizo kubwa katika mji wetu mkuu pale Tukuyu katika Jimbo letu la Rungwe, lakini Serikali pia ilituletea shilingi milioni 500 mwezi uliopita na miradi mbalimbali inaendelea kutekelezwa katika Jimbo hilo. Wananchi wamefurahi sana na wanasema Mwantona tupelekee salamu kwamba wameiamini Serikali ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa umeme, sisi tuna vijiji 99. Vijiji ambavyo vilikuwa na umeme ilikuwa ni vijiji 66 na vijiji 33 vilikuwa havina umeme. Niwaambie wananchi wa Jimbo la Rungwe kwamba vijiji vyote 36 kwa mujibu wa bajeti hii, vinakwenda kupata umeme na wananchi wanaenda kufurahia matunda ya uhuru wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitashukuru Wizara ya Ardhi ambayo imekwenda kupunguza tozo au kiasi cha premium ambayo ilikuwa inalipwa katika upimaji wa viwanja vipya. Wametoa kutoka asilimia 2.5 hadi 0.5; lakini pia kwenye uhalalishaji wametoa kutoka 1% hadi 0.5%. Naona kabisa kwamba tunapokwenda, wananchi wengi watapima ardhi kwa sababu gharama imepungua, itakuwa ni ukombozi katika maisha yao kwa sababu ardhi ni mwanzo wa kujipatia mitaji na kufanya biashara zao ambazo zitawasaidia katika maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni shukrani pekee pia. Vile vile nashukuru kwa bajeti hii imekwenda kuangalia Property Tax. Nilimsikia mama kipindi fulani anasema kwamba tutumie akili zaidi kuliko kutumia nguvu katika ukusanyaji wa kodi za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba Waziri wa Fedha ametumia akili zaidi katika ukusanyaji wa Property Tax kuliko ilivyokuwa hapo awali. Kodi hii inakwenda kuongeza walipa kodi wengi zaidi (tax base) wanakwenda kuongezeka. Pia gharama za ukusanyaji wa kodi zinakwenda kupungua. Mara ya kwanza tulikuwa tunatumia Watendaji wa Kata, watu mbalimbali walikuwa wanaenda katika maeneo mbalimbali, gharama zilikuwa kubwa, lakini kwa kutumia utaratibu ambao umeshawekwa, gharama za ukusanyaji wa kodi zitapungua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu wazi kwamba kama kuna changamoto ambazo zipo, zishughulikiwe lakini utaratibu huu ni mzuri ambazo utasaidia sana kukuza mapato ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaomba nitoe ushauri kidogo kwa Serikali na nitaomba Waziri wa Fedha anisikilize especially kwenye halmashauri zetu. Halmashauri zetu ukiangalia kuanzia mwaka 2016/2017, 2017/2018, 2018/2019, 2019/2020 uwezo wa kujitegemea kwa halmashauri zetu uko chini 2016/2017 halmashauri ilikuwa na uwezo wa kujitegemea halmashauri zote kwa wastani ilikuwa ni asilimia 11, 2017/2018 uwezo wa halmashauri zetu kujitegemea nchini ulikuwa ni asilimia 13, 2018/2019 uwezo wa halmashauri zetu kujitegemea nchini kote ilikuwa ni asilimia 15 na mwaka huu kwa mujibu wa taarifa ya CAG uwezo wa halmashauri zetu kujitegemea umefikia asilimia 15 ina maanisha nini? inamaanisha kwamba mapato ya ndani ya halmashauri ukagawanya na matumizi mengineyo pamoja na mishahara ndiyo uwezo wa halmashauri kujitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme kwa dhati kabisa kama Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi ambayo ni sikivu waangalie kwa jinsi gani kubadilisha mindset kuziwezesha halmashauri zetu kuongeza uwezo wa kujitegemea. Si vizuri sana kuonekana kwamba Serikali Kuu inaongeza uwezo wa halmashauri kutokujitegemea ili tuweze kuwasaidia tumekuja Wabunge wote hapa tumeshangilia sana madiwani wetu kupewa posho zao tumeshangilia sana watendaji wa kata kupewa posho zao. Lakini nishauri kwa Serikali yangu tukufu kwamba tuwasaidie halmashauri zetu kuendeleza kukusanya mapato kuliko kuwapelekea pesa kwa ajili ya kuwalipa madiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naweza nikatoa mfano mmoja tu ambao unaweza ukasaidia kuongeza mapato ya halmashauri service levy ambayo ni mapato makubwa sana chanzo kikubwa halmashauri zetu haikusanyi sheria ya fedha Local Government Finance Act ya Mwaka 1982 ambayo imekuwa advanced 2002 inasema kabisa kwamba halmashauri itakusanya service levy kwa mtu yeyote ambaye ana leseni ya biashara yoyote lakini utafiti mdogo nilioufanya halmashauri nyingi hazikusanyi service levy mtu yeyote mwenye biashara ana leseni ya biashara anatakiwa alipe service levy lakini hawalipi na ndiyo maana unakuta mapato ya halmashauri yanakuwa chini na hivyo uwezo wa kujitegemea unazidi kushuka mwaka hadi mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba tufanye utafiti kwenye service levy tuzisaidie halmashauri zetu ziweze kukusanya service levy ili kuongeza mapato yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niliseme hilo kwa sababu siyo picha nzuri sana kwa Serikali kuonekana halmashauri nyingi sana zinategemea Serikali Kuu kuendesha shughuli zake siyo picha nzuri sana financial statement tunazidi kuzi-spoil za halmashauri. Kwa mfano nimeangalia haraka haraka hapa kwenye taarifa ya CAG kuna majiji yetu Matano. Jiji la kwanza ambalo liliongoza lilikuwa na uwezo mzuri wa kujitegemea lilikuwa ni Jiji la Dar es Salaam ambalo limeshavunjwa lilikuwa na asilimia 484 walikuwa na mapato ya bilioni 16 wakapokea mapato kutoka Serikali Kuu bilioni 3.6 ilikuwa ni milioni 484 ilikuwa ni asilimia 484 uwezo wake wa kujitegemea ulikuwa siyo mbaya ni mzuri lakini jiji la pili ilikuwa ni Dodoma walikuwa na asilimia 45 ya kujitegemea, jiji la tatu ilikuwa ni Arusha walikuwa na asilimia 32 ya kujitegemea. Jiji la nne ilikuwa ni Mbeya asilimia 20 ya kujitegemea Jiji la tano na la mwisho ilikuwa ni Tanga asilimia 6 ya kujitegemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tusione fahari sana sisi kama Serikali kuwawezesha kuwapelekea hela za ruzuku kwenye halmashauri vinginevyo tuwatafutie mapato mengine ambayo yatawasaidia wao kuwawezesha kwenye financial statement zao kwamba uwezo wao wa kujitegemea unazidi kupanda mwaka hadi mwaka.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Anton ahsante.

MHE. ANTON A. MWANTONA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)