Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Temeke
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi lakini pia nikupongeze kwa niaba ya Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa moyo wa dhati kabisa nimpongeza sana Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani kwa hotuba yake nzuri iliyosheheni ukweli na itakuwa busara sana Wizara ya Afya ikaichukuwa na kuyatumia yale yote ambayo yameainishwa mle. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Rais, Mheshimiwa John Pombe Magufuli ameahidi kutupatia vituo vya afya kwenye kila kata. Kwa hiyo, hili ni deni ambalo Serikali ya Awamu ya Tano tunaidai. Tulikuwa tunategemea katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri hapa ita-reflect moja kwa moja kwenye ahadi ambazo Mheshimiwa Rais amezitoa kwa Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ama amezitaja au hakuzitaja lakini nataka Wizara ijue kwamba sisi kama Watanzania tunategemea kuona vituo vya afya kwenye kila kata. Mimi nikuambie tu Temeke ambako nina kata 13 tuna kituo cha afya kimoja na Hospitali ya Temeke kwa hiyo nakudai vituo vya afya 12. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wakati wako nitakufuata uniambie tunavipataje ndani ya miaka hii mitano. Kama ni kupata viwili kila baada ya mwaka, kupata vitatu kila baada ya mwaka itakuwa ni jambo zuri. Kimsingi tunahitaji ahadi mlizozitoa zitekelezwe kwa sababu wananchi wanazisubiria. Laa kama mnaona yale mlioyaahidi hayawezi kutekelezeka basi isemwe ili tujue kwamba tunatafuta source zingine kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kwa sababu sisi kama Wabunge bado tuna nia thabiti ya kuwasaidia wananchi kuhakikisha kwamba huduma ya afya inapatikana katika maeneo yao ya karibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nilitaka kuishauri Wizara ya Afya, wakati inafanya allocation au namna ya kuzisaidia hizi hospitali izingatie sana mazingira ya kijiografia. Sisi katika Hospitali ya Temeke tunapata taabu sana pale kwa sababu muda wote hospitali inazidiwa na wagonjwa kwa sababu tu ya mazingira ya kijiografia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Temeke inapakana na Mikoa ya Kusini mwa Tanzania kwa maana ukitoka Temeke sasa ndiyo unaelekea Kusini. Kwa jiografia tu mbaya ya Mkoa wa Pwani, nasema jiografia mbaya kwa maana Mkoa wa Pwani umekatwa kati na Mkoa wa Dar es Salaam. Sasa mtu hawezi kutoka na mgonjwa labda Utete akampeleka Tumbi - Kibaha yaani avuke Temeke, haiwezekani maana yake atamshusha Temeke. Mtu hawezi kutoka na mgonjwa Kibiti akaipita Temeke aende Tumbi - Kibaha atamshusha Temeke halikadhalika na Mkuranga. Kwa hiyo, kumbe Hospitali ya Temeke haihudumii tu watu wa Temeke, inahudumia na watu wa mikoa ya jirani. Sasa tunapofanya zile allocation tuangalie mazingira haya ya kijiografia kwa sababu sisi tunakuwa tumezidiwa si kwa maana ya wakazi wa Temeke lakini kwa maana ya jirani zetu na unafahamu suala la huduma ya afya huwezi kumwambia mtu kwamba wewe hutokei Temeke nenda huko, kwa hiyo lazima wote tuwasaidie pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Wizara mlizipandisha daraja hizi hospitali za Temeke, Ilala na Mwananyamala, cha ajabu bado mmeuacha mzigo kwa halmashauri. Serikali irudi na itekeleze majukumu yake kwenye hizi hospitali kwa ni mzigo mkubwa sana kwa Halmashauri. Unaita Hospitali ya Mkoa halafu inahudumiwa na Halmashauri, vyanzo vyetu havitoshelezi kuzihudumia hizi hospitali. Ni lazima Serikali itekeleze wajibu wake kuhakikisha kwamba hizi hospitali zinakuwa na wafanyakazi, wataalam na vifaa tiba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana mpaka leo mwana mama anapokwenda kujifungua abebe na vifaa vidogo vodogo vya kwenda kumsaidia kujifungua hospitalini. Huu ni udhalilishaji mkubwa wa mama zetu. Kwa nini Serikali ishindwe hata kuweka vifaa vidogo vidogo kama groves, sindano, uzi, beseni, kweli? Miaka zaidi ya 50 kweli tunashindwa kupata sindano za mama kujifungulia?
Kwa hiyo, wako kina mama wengine wanadhalilika, wanajifungulia kwenye daladala kwa sababu tu hakwenda hospitali mapema alikuwa hajatimiza hivyo vifaa vya kwenda kujifungulia. Hebu tujaribu kuyatengeneza haya mazingira ya kujifugulia akina mama yawe mazuri na yenye staha kwa ajili ya kulinda heshima ya mwanamke. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.