Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Dunstan Luka Kitandula

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mkinga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili na mimi niweze kuchangia kwenye mjadala wa bajeti uliopo mbele yetu. Namshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa pumzi na uhai, naomba aendelee kutulinda ili tuweze kuendelea kulitumikia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, msemaji aliyemaliza kusema amezungumzia jambo la nchi yetu kuanzisha refinery ya kusafisha dhahabu hili ni jambo sana, nataka kuipongeza Serikali kwa hatua kubwa hii ambayo inaenda kuongeza thamani ya dhahabu yetu lakini tukipiga hatua zaidi kwa benki kuu kununua dhahabu ile maana yake tunaenda kuifanya sarafu yetu iwe na thamani zaidi, hongereni sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimpongeze Mheshimiwa Rais wakati wa uzinduzi kuna jambo aliliona, jambo ambalo limekuwa likipigiwa kelele kwa muda mrefu kuhusiana na kodi ya ongezeko la thamani kwenye sekta hiyo, ametoa maelekezo kwamba kodi ile isiwe kikwazo cha sisi kuweza kupata manufaa zaidi kutokana na sekta hii ya madini. Hapa ndipo ninapotaka kuanzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka miwili iliyopita tulifanya mabadiliko makubwa sana ya kuruhusu wachimbaji wadogo kuingia kwenye sekta hii, tuliondoa kodi zilizokuwa na kero na hali ile ikachangia wachimbaji wadogo wa Kitanzania kuingia kwa nguvu kubwa kwenye uchimbaji, hali ambayo imeifanya sekta ya madini kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wetu. Lakini ninapata hofu kwa measures za kikodi zinazopendekezwa na hofu kwamba tunaweze kufifisha jitihada hizi ambazo tumekwishazifanya na zimeleta manufaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mapendelezo yaliyopo hapa yanaenda kubadilisha kumtambua mchimbaji mdogo ni nini, Sheria ya Madini inamtambua mchimbaji mdogo katika kiwango fulani kikubwa mapendekezo yanayokuja hapa yanaenda kumtambua mchimbaji mdogo Katika level ndogo sana, hii inaweza kuleta kikwazo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo yanayokuja yanaenda kupandisha kodi kutoka asilimia saba mpaka kwenda asillimia10, sina uhakika kama tumefanya utafiti wa kutosha kwa nchi zinazotuzunguka wao kodi yao iko vipi, hofu yangu hapa ni kwamba tunaweza kuweka kodi hii tukajikuta tunarejesha tatizo la utoroshaji wa madini kwenda nje. Hivyo ile tamaa yetu ya kuona viwanda hivi tulivyovianzisha vina pata malighafi tukajikuta tunajipiga risasi wenyewe kwenye mguu wetu kwa madini haya kusafirishwa kwenda nje; naiomba Serikali iliangalie vizuri suala hili. Nayasema haya kwa sababu wakati tukiongeza hivi tukumbuke kuwa zipo taasisi nyingine na zenyewe zinaweka tozo kwenye sekta hii hii. Leo hii tunapozungumza watu wa mabonde, Bonde la Ziwa Victoria na kwingineko wanamtoza shilingi milioni sita kwa mwaka mchimbaji mdogo. Kwa hiyo tuangalie jambo hili lisije likawa kikwazo kwenye ukuaji wa sekta yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nijielekeze kwenye eneo la kilimo cha alizeti, naipongeza Serikali kwa jitihada hii. Sisi Mkoa wa Tanga tuliwekwa kwenye mazao saba ya kimkakati, kwa maana ya zao la mkonge, lakini Mkoa wa Tanga umebarikiwa, kwamba unapata mvua mara mbili kwa mwaka. Hivi kwa nini tusiitumie fursa hii ya upatikanaji wa mvua mara mbili kwa mwaka tukauingiza Mkoa wa Tanga kuwa miongoni mwa mikoa inayolima zao la alizeti? Kwa sababu kilimo cha mkonge kinachukua miaka mitatu kuanza kuzalisha, sasa katika kipindi cha hapa katikati ardhi ile inaweza kutumika kuzalisha mazao ya mafuta haya. Kwa hiyo naiomba Serikali iangalie eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nayasema haya kwa sababu huko nyuma mzee Kingunge marehemu alipokuja kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga alifanya uamuzi wa kuhakikisha mashamba yote ya mkonge yanatumika kulima kilimo cha mazao ya mahindi; na katika kipindi kile Mkoa wa Tanga uliongoza katika Taifa hili kwenye uzalishaji wa mahindi. Tukitumia mtazamo huu tunaweza kusaidia kukuza uzalishaji wa mazao ya mafuta katika nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni kuhusu mapendekezo ninayoyaona yanakuja hapa ya kikodi kwenye zao la mkonge. Nataka niipongeze Serikali kwamba ilifanya kazi kubwa sana ya kufufua zao hilo la mkonge, hamasa kubwa iliingia na mifumo ya kikodi iliyokuwa imewekwa ilikuwa inamuhakikishia mkulima kuwa na bei inayotabirika na bei nzuri. Mapendekezo haya yanayokuja yanakwenda kuua hamasa ya kulima zao la mkonge yanakwenda kumsababishia mkulima mdogo aweze kupata bei ndogo na hivyo ulimaji au ufufuaji wa zao hili unakwenda kuanguka.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali iangalie upya jambo hili eneo la produce cess na lile lingine hebu tuangalie vizuri. Yupo mtu tumempa jambo hilo atalizungumzia vizuri ndugu yangu Mnzava, lakini naomba sana Serikali mliangalie kwa umakini eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kwa kutanua wigo wa kodi. Ni jambo ambalo tumekuwa tukihangaika nalo kwa muda mrefu, nikupongeze Mheshimiwa Waziri umekuwa na ubunifu mkubwa sana, hongera sana. Lakini yapo maeneo mengine hebu tuyaangalie. Tunapofanya uagizaji wa mafuta kwa pamoja kwa sasa hivi kampuni zinazoagiza mafuta kutoka nje hazijasajiliwa hapa. Kwa hiyo kunakuwa na shida ya ushindani kati ya kampuni za wazawa zilizoko hapa na zile za kutoka nje. Za kutoka nje hazilipi cooperate tax na service levy. Hii inasababisha ushindani kati ya kampuni hizi za nje na hizi za ndani unakuwa si sahihi. Hebu tuangalie eneo hili tuweze kuona kama tunaweza kutumia mwanya huu kuweza kuongeza mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya nakushukuru sana, ahsante.