Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon Abubakar Damian Asenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi ili na mimi nichangie bajeti yetu. Nami kama walivyosema Wabunge wenzangu mara kadhaa, napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake wote kwa kutuletea bajeti ya namna yake ambavyo kama Waheshimiwa Wabunge wameshasema mara kadhaa hapa mazuri ya bajeti hiyo nami nirudie yale ambayo wana Kilombero na wananchi wa Morogoro wanayashukuru na kuyapongeza. Mathalani suala la fedha za TARURA, milioni 500 kila Jimbo, Bima ya Afya kwa wote, mazingira mazuri ya biashara na kuwekeza katika kukuza thamani ya mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli ni bajeti ya namna yake na Mheshimiwa Waziri kaka yetu Mwigulu anathibitisha ubora wa watu ambao wanapenda timu ya yanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Pamoja na pongezi hizo nina mambo kama mawili ama matatu ya kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala zuri sana linalohusu posho kwa Waheshimiwa Madiwani tunalishukuru na tunalipongeza jambo hili. Lakini kama sisi tumesema Waheshimiwa Madiwani ni Wabunge wenzetu kule kwenye halmashauri, naishauri na kuiomba Serikali huko mbele tunakokwenda kuwe na utaratibu maalum wa vyombo vya usafiri kwa madiwani. Vyombo vya usafiri ambavyo vitawekewa utaratibu kama tulivyowekewa Wabunge mkopo wa magari tunaweza kufikiria pia Waheshimiwa Madiwani wakawekewa mkopo kama wa lazima hivi usiokuwa na riba kubwa wa kupata walau pikipiki nzuri za kisasa za kuwasaidia Waheshimiwa Madiwani kufanyakazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa kuwa Halmashauri imeondolewa mzigo wa posho sasa hivi mambo ya simu na nini kule kwenye halmashauri wanaweza wakayaangalia. Lakini pendekezo langu; Mheshimiwa Waziri ukweli ni kwamba kutokana na changamoto za baadhi ya majimbo Madiwani wakati mwingine wanateseka sana kwenye usafiri. Wasipopanda gari la Mbunge watadoea doea gari za halmashauri, lakini wakiwa na pikipiki zao zitawasaidia kufika kwenye vikao kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili mimi nina jambo mahsusi kwa Mheshimiwa Waziri, hasa la barabara yangu ya Ifakara Kidatu, na hapa nataka niseme kidogo, naona ukishika kalamu Mheshimiwa Waziri, mimi nafarijika sana. Sisi tunajenga barabara kilometa 66.9 ya lami, mwaka wa nne tunajenga. Yaani kila siku nikisimama hapa nasema mpaka nimeenda nimekaa chini kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ina changamoto nyingi, na hasa inauma kwa sababu unakuta wataalamu wa ujenzi wa barabara hii wanalalamika lakini wanakwambia Mbunge hii naongea mimi na wewe. Sasa barabara yetu Mheshimiwa Waziri imesainiwa na Wizara yako, na juzi tulikuwa na kikao na Wizara ya Fedha pale. Nataka kushukuru kwa dhati Katibu Mkuu wa Ujenzi na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha kaka Emmanuel Tutuba kwa kweli ni msikivu, na kikao cha juzi kimeanza kuleta matumaini kwamba kuna changamoto kwa kweli watazitatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kikao chetu cha mkoa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa Waheshimiwa Wabunge wote wa Mkoa wa Morogoro katika mambo ambayo tuliambiwa tunatakiwa kupata elimu ya kuyasemea mojawapo ni barabara hii; na kwenye kikao kile wataalamu wa ujenzi bila kutaka kuwataja hapa walisema changamoto; kuwa ni mvutano wa Mhandisi mjenzi na mshauri. Na wakasema kwamba mhandisi mshauri akimaliza muda wake aende, kwa sababu barabara ina fadhiliwa na European Union mkandarasi mshauri ameshachukua bilioni tisa mpaka sasa tunajenga kilometa 66.9 ameshachukua bilioni tisa mpaka sasa hivi barabara inasuasua. Mheshimiwa Waziri jambo hili liko kwako mkataba wa barabara ile ya ujenzi ya Ifakara Kidatu umesainiwa na Wizara ya Fedha. Sasa nimejaribu kumuelewesha Mheshimiwa Katibu Mkuu na nimeona respond yake kwamba atafanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyozungumza na wewe European Union wameshaanza kusita kutoa fedha za mshauri, Serikali yako kwenye bajeti hii inatakiwa imlipe 1.4 Euro milioni karibu bilioni 4.6 za kumuongezea mkataba mkandarasi ambaye anamaliza mkataba wake Juni. Hii bilioni 4.6 wataalamu wale ambao wanatuambia Mheshimiwa Mbunge tuongee pembeni wanasema pesa hizi ni nyingi na huyu mshauri analipwa hela nyingi kuliko wakandarasi wote nchi hii kwanini? Kuna jambo gani nyuma ya pazia? Na hao wa ujenzi wanasema nusu ya fedha hizo aidha TANROAD inaweza kusimamia hiyo barabara au wakandarasi washauri wengine. Tuna miradi mikubwa hapa inataka akili nyingi kuliko kilometa 66 za barabara, kwa nini mkandarasi mshauri hapa alipwe fedha nyingi zaidi?

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa tuliambiwa hawa watu waligombana huko nje ya nchi kwenye mradi, ugomvi wao na mvutano wao kugombana wanauleta hapa, mpaka mambo mengine yanataka kwenda kwenye mahakama za kimataifa, mara huyu kamkataa huyu mara huyu kamkataa huyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamuomba Mheshimiwa Waziri, kama ambavyo Mheshimiwa Waziri Mkuu ameingilia jambo hili, Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi alienda na ametoa maelekezo kwamba ili barabara ile ikamilike ambayo iko chini ya Waziri wa Fedha inatakiwa Mhandisi mshauri, Juni hii analize aondoke ili TANROAD wapewe nguvu wasimamie barabara hii na wakandarasi washauri wanaoona wanafaa ili tuweze kusongambele. Kwa hiyo Mheshimiwa nakuomba chonde chonde, Mheshimiwa Waziri Mkuu amesha intervene na wewe uki-intervene hapo tutamaliza jambo hili vizuri na barabara yetu itaenda mbele. Ni aibu sana, kilometa 66.9 ambazo fedha zipo kwenye Wizara yako mfadhili kalipa lakini mpaka leo tunasuasua. Mfadhili ameshaonesha hataki kumlipa mkandarasi mshauri pesa tena kwa sababu amefika maximum ya malipo yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa sababu wataalamu wetu wa ujenzi wanatuambia mambo haya tuyaseme na sisi wanasiasa hasa vijana kama Mungu akipenda as a factor remain constant ceteris paribus we have nothing to lose because age is on our side, Mungu akipenda. Kwa hiyo kutetea nchi hii tutaendelea kusema ukweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona kwenye kilimo; mimi la kwangu nataka kuungana na Mbunge wa Hai, kuhusu ushirika. Ushirika ni matatizo, matatizo kweli kweli. Na kama kweli tunataka kukuza kilimo chetu, na mimi nina interest na kilimo cha miwa kule, ni vizuri Wizara ya Kilimo ikatoa elimu ya kutosha kwa watu wa ushirika; hasa zile Bodi ili ziweze kuendeleza mazao ya ushirika vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitakwambia hapa mfano wa jambo moja ambalo limefanywa na viongozi wangu wa ushirika kule, na migogoro hii Mheshimiwa Waziri anahangaika nayo kuitatua kila siku. Wanabandika taratibu za kutafuta zabuni zinafatua wanakuja wanatengua, mgogoro! Mgogoro! Mgogoro! Mgororo. Kama alivyosema Saashisha, kwamba Bodi hizi za ushirika lazima ziangaliwe vizuri. Kama zimebandika taratibu wanataka wazabuni wenye sifa hizi wamepatikana wasitengue zile barua zao, kwa sababu wanavyotengua barua wanampa leo huyu inaleta mgogoro mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, na nataka kutumia nafasi hii kuwasihi sana wakulima wangu wa miwa hasa wa Sanje ambao wananipigia simu kila wakati wanataka Mkutano Mkuu ili waamue jambo hili liishe; na naomba sana wavute Subira na Mungu atatusaidia tutamaliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo napenda kusisitiza kwamba namuomba Mheshimiwa Waziri wa Kilimo na Mheshimiwa Waziri wa Fedha kama kweli wanataka kupandisha thamani ya mazao yetu kama walivyoahidi katika bajeti basi wasimamie vizuri ushirika, na nimemuomba Mheshimiwa Waziri awaruhusu hawa wakulima wa miwa wafanye mkutano wao mkuu waamue juu ya jambo hili. Ninamshukuru Dkt. Ndiyege ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Ushirika, amelifanyia kazi jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokwenda sasa, kama kweli tunataka Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia iendelee kufanya vizuri sisi pamoja na wote wanaomshauri ni vizuri tukasisitiza kuhusu mambo ambayo Mheshimiwa Rais aliyafanya akiwa Makamu wa Rais na Hayati Dkt John Pombe Magufuli yakaendelezwa na yakasimamiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokwenda sasa, kama kweli tunataka Serikali ya Mheshimiwa Rais Samia iendelee kufanya vizuri sisi pamoja na wote wanaomshauri ni vizuri tukasisitiza kuhusu mambo ambayo Mheshimiwa Rais aliyafanya akiwa Makamu wa Rais na Hayati Dkt John Pombe Magufuli yakaendelezwa na yakasimamiwa, kwa sababu Watanzania wanaona na wanasikia. Ni hatari sana sasa hivi ukisikia kwamba kuna mkulima wa gunia moja analazimishwa kutozwa ushuru, maana yake Serikali iliyopita ilikuwa inasisitizwa ukiwa na chini ya tani moja vusha vusha.

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi nimekwenda kule Morogoro, nimekuta wakulima wanalalamika wanasema mbona sasa hivi tunatozwa na tulikuwa hatutozwi. Kwa hiyo, mtu yoyote anataka kukwamisha Serikali hii ni yule anayetaka kutengua mazuri ambayo Mheshimiwa Samia aliyafanya akiwa na hayati Dkt. Magufuli ambayo sasa hivi anayaendeleza na kurekebisha upungufu au kuuondoa, mathalani hiyo ya Machinga kuguswaguswa, mazao chini ya tani moja watu kuanza kutozwa ushuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kwamba, Serikali yetu kurudi katika mikopo, lazima tuombe Mungu kwamba mikopo hii ambayo nchi yetu itachukua, iwe ni mikopo mizuri, yenye masharti mazuri. Hayati Dkt. Magufuli alisikika mara kadhaa akisema, tahadhari za nchi ya Afrika kuhusu mikopo hii. Kwa hiyo, mambo haya yote yakisimamiwa vizuri itaonekana kwa kweli tunasonga mbele na tunaenda mbele pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, narudi kwenye miradi ya maji na Wizara ya Maji. Ni wazi kuwa kuna Wabunge tulikutana hapa kama 28, tukakutana na Waziri wa Maji ambaye anafanya kazi nzuri, tukazungumzia Miradi ya Miji 28 na kwamba miradi ile ni muhimu na kwa sababu ilikuwa ni mkopo kutoka Exim Bank ya India process zilikuwa zinaendelea. Sasa kaka yetu mara nyingi anafuatilia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABUBAKARI D. ASENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)