Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Abdullah Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mahonda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Awali ya yote nami napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na wataalam wote wa Wizara ya Fedha kwa kutupatia na kufanya kazi kubwa sana ili kuikamilisha hii bajeti ambayo tunaijadili kipindi hiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile muda siyo rafiki napenda kuingia moja kwa moja katika mchango wangu. Napenda kuzungumzia mambo mawili; la kwanza ni uchumi kwa ujumla wake na la pili suala la ubunifu na ajira, kwa sababu sehemu nyingi wenzangu ambao wamenitangulia wamezigusia na kwa kweli sina haja ya kuyarudia.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na janga kubwa la Uviko 19 lililokabidili dunia nzima Tanzania imebahatika; na siyo bahati, kwa mkakati na kwa mpango mzuri tumejaaliwa uchumi wetu kukua kwa asilimia 4.8.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia nchi ambazo zinatuzunguka Kusini mwa Jangwa la Sahara nchi zote kwa wastani chumi zao zimepungua, zimekuwa hasi, zimepungua kwa asilimia 1.9. Na kwa ulimwengu kwa ujumla wake chumi zimepungua kwa asilimia 3.3.

Mheshimiwa Naibu Spika, hakika kabisa, na iko bayana kabisa, kuna jambo ambalo sisi tumeweza kulifanya vizuri katika Janga hili la UVIKO-19 na ikatuwezesha uchumi wetu kukua kulinganisha na chumi nyingine zote za ulimwenguni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nimechukua fursa ya kutazama makampuni yetu makubwa yameendeleaje katika kipindi hiki. Nimechagua kampuni zifuatazo; TBL, TCC, Vodacom, Tigo na Puma Energy, kwa makusudi kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiziangalia hizo kampuni, ndizo kampuni ambazo zinatupa kodi kwa wingi; TBL, TCC, Vodacom na Tigo pamoja na Puma. Kuangalia taswira ya kibiashara inakwendaje. Ukiangalia kampuni zote hizo tano, hasa hizo nne za mwanzo, zote mapato yao yamepungua kwa kipindi cha miaka miwili mpaka mitatu sasa na kipindi cha mwaka uliopita mapato (revenue) yamepungua.

Mheshimiwa Naibu Spika, Vodacom quarter ya mwisho imepata hasara. Sasa ukiangalia huu uchumi umekuwa katika sekta gani, wakati ukiangalia makampuni haya makubwa mengi yameathirika. Sekta zilizotuwesha uchumi wetu sisi kukua ni ujenzi, madini, mawasiliano, uchukuzi, kilimo na viwanda. Ujenzi asilimia 13, madini asilimia tisa; hayo ndiyo maeneo ambayo yamekuza uchumi wetu. Eneo la hospitality; mahoteli, migahawa na utalii, yamepungua kwa asilimia karibu 14. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukiipitia ripoti ya BoT ya Desemba, 2020, inaonesha bayana kwamba eneo kubwa la ukuzi wa uchumi ni ujenzi, asilimia 42.6 na kilimo, asilimia 24.6. Theluthi mbili ya uchumi wetu umeshikwa katika hayo maeneo mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nimetoa haya kama muhtasari. Ili kuitathmini bajeti lazima tuelewe uchumi wetu uko wapi na unakwendaje na bajeti yetu iendane na hali halisi ya huu uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia 42.6 katika ujenzi imekuwa kwa sababu ya ile miradi ya kimkakati. Fedha nyingi zimepelekwa kwenye SGR, fedha nyingi zimepelekwa kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere, fedha nyingi zitapelekwa kwenye bomba la mafuta la kutoka Uganda. Kwa takribani miaka mitano mpaka kumi sekta hiyo itaendelea kukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pato kubwa, asilimia 24.6, katika kilimo ndiyo imetoka hapo. Lakini ukiiangalia bajeti inachangia chini ya asilimia moja. Chini ya asilimia moja inakwenda sehemu ambayo inatupa robo ya pato letu la nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu kwa Waziri wa Fedha ni kwamba bajeti zijazo lazima tuongeze uwekezaji katika sekta hii ili izidi kustawi na izidi kutupa tija. Kama chini ya asilimia moja inatupa robo basi tukiweka asilimia kumi, kama Maputo Protocol, hakika uchumi wetu na bajeti yetu na mapato yetu yatakuwa makubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni kuhusu ubunifu na ajira nilisema ninataka kugusia. Tatizo la ajira Tanzania ni kubwa. Asilimia 70 ya Watanzania wana umri chini ya miaka 35. Tulisikilize vizuri; asilimia 70 wana umri wa chini ya miaka 35. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, humu ndani sisi Wabunge kwa demography hiyo hatuwawakilishi wananchi wetu, sisi ni wazee wote kwa takwimu na kwa mfano wa hiyo demography. Maana yake wachache sana hapa wako chini ya miaka 35, lakini asilimia 70 ndio hao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hiyo inaonekana dhahiri kwamba ajira itakuwa changamoto na itakuwa agenda yetu kubwa sana. Tunafanyaje kukabili tatizo la ajira? Maeneo ni haya mawili; la kwanza, kwa Tanzania ni kilimo, la pili ni ubunifu ambao upo kwenye teknolojia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo sasa ndiyo ninataka nipagusie zaidi. Mwaka 2005 wanafunzi wa Nairobi University, Kitivo cha Computer Science walibuni solution ambayo hii leo ni mobile money; mwaka 2005. Ukiangalia uchumi, siyo tu wa Tanzania, wa Afrika Mashariki yote, umetokana kwa sehemu kubwa na mchango huo. Ukiangalia sasa hivi katika mawasiliano mobile money inachangia fedha nyingi sana katika kodi zetu, Afrika Mashariki yote na Tanzania yenyewe. Hilo limetokana na ubunifu wa wanafunzi vijana. Na haikuwa bahati mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipindi hichi TCRA ilikuwa inaongozwa na Profesa Mkoma na BoT Gavana alikuwa Prof. Ndulu. Hawa maprofesa wawili walikuwa na imani ya kukuza vipaji na ubunifu kabla ya kuongeza mfumo wa kupata fedha Kiserikali. Waliuacha huu ukastawi halafu ndiyo wakawekea mfumo wa regulation. Haikuwa bahati mbaya, imefanywa kwa makusudi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha katika sekta hiyo ni kwamba lazima turuhusu ubunifu ustawi na tuulee. Tusifanye kama yule bata anayezaa yai la dhahabu kila siku tukamkaba yule mpaka lile yai asilizae. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hiyo – kama angalizo – kwa Tanzania ukilinganisha na wenzetu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ndiyo sekta ambayo ina kodi kubwa. Ukilinganisha na Uganda, kodi yake ni ndogo, ukilinganisha na Kenya, kodi yake ni ndogo, Tanzania kodi yake ni kubwa. Na kwa safari hii tunaelewa kwa nini imebidi kuiongeza, lakini hilo ni angalizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya ubunifu lazima ilelewe istawi ndiyo tuweze kupata tija. Sasa eneo kubwa ambalo sisi tunategemea kuwapa ajira vijana wetu ni maeneo mawili kwa bahati mbaya bajeti hii haiyapi support ya hali ya juu; kilimo na sekta ya ubunifu. Sekta zote hizo zipo kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kama tutaiwekea kipaumbele na tutafanya mazingira ya ustawi ili ikue itupe tija zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hakika kwa hayo machache, ninapenda kuunga mkono hoja na ahsante sana.