Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Asya Mwadini Mohammed

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. ASYA MWADINI MOHAMMED: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuweza kunipa nafasi nami jioni hii ya leo niweze kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza kabisa nianze kunukuu hotuba ya Mheshimiwa Waziri aya ya 77 ukurasa wa 65 unaosema kuhusu Zanzibar. Kwa maneno aliyoweka ya kunukuu, napendekeza kutekeleza utaratibu wa kuruhusu mapato yanayotokana na kodi na tozo za Muungano kwenye mapato yanayotokana na viza ili yaweze kutumika pale yanapokusanywa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mapato yanayotokana na tozo na viza za Zanzibar yaonekane kwenye bajeti upande wa Zanzibar kuidhinishwa na kutumika kwa upande wa Zanzibar. Hii kwa Wazanzibari imekuwa ni jambo jema sana na inakwenda kuendelea kutatua zile kero mbalimbali zinazogusa Muungano wetu. Naiomba Serikali, maana maneno siyo vitendo, kwa hiyo, linapozungumzwa, tunaomba sana liende kwenye utekelezaji. Tuone kama bajeti inaanza kutumika Julai, basi utekelezaji huu na makusanyo kuanzia Julai yaanze kutekelezwa na yakaweze kutumika kwa upande wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuisaidia Serikali ili tuweze kupata mapato, najikita katika Sekta ya Uvuvi. Sekta hii inachangia pato la Taifa asilimia 1.8, lakini mapato yanayotokana na mauzo mbalimbali ya bidhaa za uvuvi ni 3%. Kwa masikitiko makubwa sana, hii sekta ni kubwa na pana, lakini pato ambalo limetajwa hapa la asilimia 1.8 ni dogo kulinganisha na rasilimali zinazotokana na bahari.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahari yetu Mungu ametujaalia neema kubwa sana kwa kweli, ina rasilimali nyingi sana za kutosha. Kama Serikali itajiwekeza zaidi, basi tuna uwezo wa kupata pato kubwa ndani ya Taifa letu na tutapunguza hata hizi kodi mbalimbali ambazo zinawagusa wananchi wanyonge wakipunguziwa mzigo huu, mapato yataongezeka kupitia sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukipitia bajeti ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano iliyokwisha, Wizara hii ya Uvuvi imekuwa ikipatiwa asilimia 21 tu ya bajeti katika utekelezaji wake. Hii inaonekana wazi kwamba Serikali bado haijaamua kujiwekeza vizuri katika Wizara hii, ikiwa miradi ya maendeleo inapewa asilimia 21 kwa miaka mitano, tusitegemee kama kuna mabadiliko wala kupata mapato katika Sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika rasilimali ambazo zipo ndani bahari, nakumbuka nilizungumza suala zima la uhifadhi wa matumbawe kama kivutio na nikatoa mfano wa baadhi ya wageni ambao huwa wanatembelea na tunapata mapato mengi kama Serikali. Nje na matumbawe, kuna kilimo cha mwani. Cha kushangaza ni kwamba Serikali yetu bado haijatupa jicho na wala haioni kama kuna umuhimu wa kuwekeza zaidi kwenye kilimo cha mwani. Ni kilimo ambacho kinalimwa kwa muda wa wiki sita tu na watu wanavuna. Kwanza kilimo chake ni cha muda mfupi lakini tumepewa bahari ambayo ndiyo sehemu sahihi tuna uwezo wa kupanda mwani wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile faida ambayo inapatikana katika kilimo cha mwani kwanza tutatengeneza ajira pana, maana watu watajiajiri kwenda baharini na tutakuwa na viwanda nje. Tunazungumza kila siku tunahitaji kuwa na Tanzania ya viwanda, lakini tutakuwa na viwanda ambavyo mwisho wa siku hatutakuwa na rasilimali kwenye hivyo viwanda ambavyo tunavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nje tu na ajira, mwani ni chakula. Tuna uwezo wa kutengeneza vitu mbalimbali ambavyo binadamu tunavitumia, ni vyakula vya kila siku. Vile vile, mwani hutumika kama vipodozi. Akina mama wengi wa Kitanzania tunatumia cosmetics kutoka nje ya nchi wakati tuna rasilimali zetu nyingi. Ukianza na huu mwani, tuna uwezo wa kutengeneza sabuni na vitu vingi tukavitumia wenyewe. Kwa hiyo, kuna haja Serikali nayo kutupa jicho kwenye kilimo hiki cha mwani ili tuweze kuokoa Taifa letu na kupata mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kilimo hiki cha mwani tukizungumza kwa dunia, tuchukue mfano nchi ya Indonesia ndiyo imekuwa ya kwanza ikilima mwani na ndiyo nchi ambayo inafanya vizuri kwenye Sekta hii ya Mwani. Mheshimiwa Rais alisema kwamba tuwe tunajaribu kuwaiga watu wanaofanya vizuri, siyo dhambi. Kwa hiyo, nasi nadhani ni wakati wetu sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wa Indonesia walio wengi wametajirika kupitia kilimo cha mwani. Vile vile wana viwanda vingi vya kutengeneza dawa, vipodozi, wanatumia mwani kama chakula na bado maisha yao yamenyanyuka vizuri sana. Kwa hiyo, naishauri tu Serikali kwanza tuwekeze kwenye mwani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Serikali imeona labda imekuwa mzigo mzito au tunaona ni jambo ambalo haliwezekani, wawekezaji wako tayari na wanahitaji hii bahari. Wanaiangalia kwa jicho la huruma sana na wanaitamani kama leo waipate na waweze kuwekeza ili tuweze kutengeneza ajira pana kwa Taifa hili na ili tuweze kutengeneza pato la Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende katika Sekta ya Utalii. Sekta hii nayo imekuwa ni chachu ya uongezaji wa pato letu, tunaizungumza kila siku lakini ukiangalia sekta hii, utalii ambao umejikita zaidi ni utalii wa wanyamapori maana tumekuwa hatu-focus kwenye utalii mwingine, yaani tumeganda tu kwenye wanyamapori, sisi kila siku kazi yetu ni kutangaza, tuna Ngorongoro na sehemu nyingine. Sasa tunahitaji pia kupanua wigo zaidi. Vile vile, kama sisi hatuwezi wawekezaji wapo, wa ndani na wa nje wako tayari, wanahitaji hii nchi kwa ajili ya kuwekeza. Wao watatengeneza pesa lakini na sisi tutatengeneza mapato, ndiyo kinachotafutwa ili tuweze kuiokoa nchi yetu kwenye masuala mazima ambayo yanaleta maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata ukipitia ripoti ya CAG, naye alishauri kwamba utalii wa Tanzania, kuna haja sasa ya kwenda kuingiza katika utalii mwingine na kuanza kuutangaza. Tusing’ang’anie tu kwa wanyamapori. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri tena Serikali iweze kutengeneza mikakati iliyokuwa bora ili tuweze kusimamia Sekta hii vizuri sana. Halikadhalika unapopitia hii hotuba, Mheshimiwa Waziri alisema kwamba watapunguza ada ya leseni za biashara za utalii kutoka Dola 2,000 hadi Dola 500. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kupunguza tu ada kwenye leseni bado hatujasaidia kwenye hii Sekta, kwa sababu tuna changamoto nyingi ambazo zinaikabili Sekta hii. Ukiangalia miundombinu yetu ni mibovu sana. Sehemu ambazo zina vivutio hazifikiki. Kwa hiyo, naishauri Serikali waanze kwanza kuboresha sehemu zenye vivutio vya utalii, watengeneze barabara, viwanja vya ndege ili watalii wawe wana uwezo wa kufika vizuri na kuweza kuingiza pato ndani ya Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuwe kuna mazingira Rafiki; tupunguze sintofahamu kwa wawekezaji wetu, maana Uhamiaji anamganda mwekezaji; sijui Halmashauri anamganda mwekezaji na wengine wengi. Imekuwa harassment kubwa sana. Kwa hiyo, tupunguze hizo harassment kwa wawekezaji wetu ili nao waweze kuwekeza kwa kujiachia na kuweza kulisaidia Taifa hili kwa kuwapa ndugu zetu ajira na kulisaidia Taifa hili kwa kuweza kutuingizia mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Ahsante sana. (Makofi)