Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Bagamoyo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nishukuru kwa kupata nafasi hii kwa jioni hii ya leo kutoa mchango wangu katika Bajeti hii ya Serikali ya mwaka 2021/2022. Kwanza napenda nitoe pongezi za dhati kabisa zinazotoka ndani ya moyo wangu kwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu, jemedari wetu, Amiri Jeshi Mkuu wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Kwa kipindi kifupi ambacho nipo ndani ya Bunge hili, mama huyu kiongozi wetu ametuheshimisha sana Wabunge kwa kutoa pesa, takribani kwa muda mfupi, shilingi bilioni moja na pointi kadhaa katika majimbo yetu. Tunampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, napenda nitoe pongezi zangu za dhati kabisa kwa Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa uwasilishaji wa bajeti yake ambayo haijapata kutokea. Miaka yote kabla sijawa Mbunge nilikuwa nasikiliza bajeti, lakini hii bajeti ambayo niko ndani ya Bunge ni bajeti ya aina yake. Nampongeza Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na ninaamini kuwepo katika timu fulani yenye rangi nzuri nzuri kumesababisha na mambo yake yawe mazuri ndani ya Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nitoe mchango wangu kwanza katika Sekta ya Uvuvi. Serikali mwaka huu katika mipango yake imeamua kujenga Bandari ya Mbegani ya Uvuvi. Naipongeza sana Serikali kwa jambo hili. Bandari hii ya Uvuvi itakapojengwa italeta manufaa makubwa siyo kwa Wanabagamoyo peke yake, ni kwa Watanzania wote kwa sababu Mbegani miaka mingi inafahamika ni Chuo kikubwa sana cha Uvuvi na wanafunzi wengi kwa miaka ya nyuma walikuwa wanasoma pale katika kile Chuo cha Mbegani. Sasa hivi, kile chuo kiko katika hali ngumu kidogo. Katika ujenzi huu wa bandari ya uvuvi ambayo inatakiwa kujengwa, itaifufua sekta ya uvuvi katika nchi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naipongeza Serikali kwa kununua meli nne za uvuvi. Hizi meli pamoja na hii bandari vikienda sambamba, basi katika sekta ya uvuvi, Serikali itakusanya mapato mengi ya kutosha. Wenzetu wako mbali katika suala la uvuvi. Kwa mfano, wenzetu Wakenya wana bandari yao pale inaitwa Liwatoni Fishing Port. Ile bandari imejengwa mpya kabisa; na mwaka huu mpaka Juni 2021, wamesema wanaingiza wanafunzi 1,000 pale kwa ajili ya kujifunza masuala ya uvuvi ili ile bandari iweze kufanya kazi kiaina yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo basi, naiomba Serikali katika bandari hii ambayo inatarajia kujenga pale Mbegani, kwanza waanze kutoa mafunzo kwa vijana ambao watakwenda kufanya uvuvi katika hiyo bandari. Halafu bandari itakapokwisha, kazi moja kwa moja inaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili nataka kuzungumzia katika sekta ya utalii. Siku moja nilichangia hapa katika mchango wangu kuhusu utalii wa ndani. Utalii wa ndani una pesa nyingi sana, lakini niliwashauri kitu kimoja, sasa hivi ifikie wakati tuanzishe utalii wa kutembea (mobile), kwa sababu Watanzania wengi sana hawana uwezo wa kwenda katika mbuga za wanyama. Tutashawishiwa sisi Wabunge twende Ngorongoro, twende Manyara na Mikumi lakini mtu wangu pale wa Bagamoyo au sehemu nyingine yoyote hawezi kuwa na kipato leo hii cha kwenda kutembea katika mbuga za wanyama za Mikumi, Ngorongoro au Manyara. Hapo itakuwa ni ngumu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naishauri Serikali, kwa sababu mabanda ya maliasili pale Saba Saba yanatembelewa na watu wengi sana katika kuona wanyama, waende kila mkoa wakafungue hizi zoo ndogo ndogo za kutalii watu. Wajenge mabanda, waweke simba, waweke swala, kila mnyama pale, watu wakienda wanalipa viingilio kwenda kuona wanyama. Wanafunzi, watu mbalimbali wakienda huko pesa itapatikana, tena kwa wingi sana, kuliko tukitegemea utalii wa ndani tuwashawishi watu waende Ngorongoro, Manyara na wapi. Watanzania walio wengi uwezo huo hawana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika suala la biashara. Biashara ndiyo inayoleta kodi na kodi ndiyo inatusaidia katika kuendesha nchi yetu. Hata hivyo, kuna changamoto sana katika biashara na hasa katika sheria hizi za TRA, za Utaifishaji. Sheria za Utaifishaji ni changamoto kubwa sana. Hizi sheria naona kwa upande mmoja au mwingine zinatakiwa sasa zifanyiwe mpango zirekebishwe. Kwa sababu leo hii kwa mfano mtu ana gari yake amenunua, amemkabidhi dereva Fuso au lory, amekwenda kubeba mzigo huko, bahati mbaya huo mzigo ni wa magendo. Inafika gari inakamatwa, inapelekwa katika sehemu labda TRA wanaikamata, wanataifisha mzigo, wanataifisha gari, pengine mwenyewe mwenye gari hahusiki. Hii inatia hasara sana kwa watu na watu wengi wanalalamika mno, kwamba kosa kafanya dereva lakini gari linataifishwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hebu hii sheria tuiangalie vizuri kwa kweli, inaumiza sana watu. Pale jimboni kwangu Bagamoyo kuna kijana mmoja ana Fuso zake mbili; madereva walikwenda wakapakia vitenge vya magendo, magari yakakamatwa, yakataifishwa. Kijana wa watu wamemrudisha nyuma. Alikuwa na Fuso mbili ambazo amezitafuta karibu miaka 20, ameanza tena sifuri. Yaani amechanganyika karibu anakuwa chizi. Jamani haya mambo mengine ya sheria tuyaangalie Mheshimiwa Waziri ili wafanyabiashara wetu waweze kufanya vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile hizi sheria za kutaifisha tunazozitunga humu ndani, wawekezaji wa nje wakizisikia hawatakuwa na imani ya nchi yetu. Wataona kwamba Tanzania ukienda kuwekeza, kama wenyewe kwa wenyewe wanataifishana, mimi mgeni nikiwekeza mali yangu itakuwa salama? Kwa hiyo, nafikiri kwamba tubadilike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho kabisa nataka kulizungumzia ni la sensa, sensa ni kitu muhimu sana. Kuna kitu ambacho nataka nimshauri Waziri, nchi zilizoendelea nyinginezo sasa hivi sensa yao, pamoja na kwamba, wanapanga kila baada ya miaka fulani wanafanya sensa, lakini wanafanya sensa ya ndani kwa kutumia watu wao. Na sisi Tanzania tuanze kufanya sensa ili tuwe na projection ya kujua maendeleo yetu yanakuaje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu, leo hii tunangojea kila baada ya miaka 10 au mingapi tufanye sensa, tunao watendaji wa vijiji, tunao watendaji wa kata, tuwatume kazi wapite vijijini kuangalia idadi ya watu wanaozaliwa ili Serikali iwe na projection vinginevyo tutakuwa na ule mpango wa zimamoto, hatujui idadi ya watu, watoto wanaoenda sekondari wanaongezeka, tunajenga madarasa ya zimamoto. Lazima tuwe na mipango thabiti katika hii sensa, tuwatumie viongozi wetu wa vitongoji watuletee taarifa wazipeleke katika kata taarifa za watoto waliozaliwa nchini, wa vitongoji wapeleke kwenye kata, watu wa kata nao wapeleke wilayani, watu wa wilayani wapeleke mkoani. Mkoani wapeleke Taifani tupate mtiririko wa idadi ya watu wanaozaliwa katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu, tukitegemea taarifa za hospitali tupu, wengine wanajifungulia majumbani hatupati taarifa zao kwa hiyo, inakuwa kidogo kuna ugumu fulani. Niiombe Serikali hili suala la sensa wasingojee mpaka kipindi, walianze mapema kuangalia projection ya nchi inakwendaje katika uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala ambalo la kilimo, nataka kuzungumzia, kilimo cha umwagiliaji. Hiki kilimo cha umwagiliaji tukikifuatilia na tukikitilia mkazo Taifa litatoka kabisa katika maisha tuliyonayo sasa hivi kwa sababu, umwagiliaji ndio wenye tija. Tukitegemea mvua hizi za kunyesha tu za msimu wakulima wetu wengi sana huwa hawazalishi pale ambapo idadi yao au idadi ya mazao wanayohitaji kufikia lengo, lakini kilimo cha umwagiliaji kitatusababishia tufike katika level nzuri kabisa ya uzalishaji katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hayo machache naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)