Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Soud Mohammed Jumah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Donge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuweza kunipa fursa hii kuweza kuchangia katika bajeti hii ya Serikali ya mwaka 2021/ 2022.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu Allah Subhana Wataalah kwa kuweza kutujaalia uzima na kuweza kuendelea na bajeti katika kipindi hiki cha lala salama. Hali kadhalika ningeomba vile vile kumpongeza sana sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wake wa Wizara ya Fedha wakiongozwa na Komandoo Katibu Mkuu Tutuba kwa kazi nzuri ya ukweli ambayo wameweza kuifanya. Kwa kweli, bajeti bajeti hii kama ambavyo wenzangu wamezungumza imezingatia hoja za Wajumbe wa Bunge hili Tukufu na ndiyo maana imekuja kuwa ni bajeti kielelezo, bajeti ya mfano, bajeti ya mkakati ambayo inakwenda kutuvusha katika uchumi ule wa kiwango cha chini tunakwenda katika daraja la juu sasa uchumi wa kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeanza tu kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Alhamis tarehe 10 wakati anawasilisha bajeti speech yake hapa siku ile ile kama nchi tano zilikuwa zikiwasilisha bajeti zao zile za nchi za Afrika Mashariki. Sambamba na hilo pia Zanzibar, siku ileile Alhamisi tarehe 10 iliwasilisha bajeti yake, Bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Sasa Mheshimiwa Waziri nikuombe hapa kabla sijaenda kwenye michango ya moja kwa moja kwamba ukimaliza bajeti hii tukimaliza Bunge hili, ningekuomba sana ukae na Waziri wa Fedha wa Tanzania Visiwani (Zanzibar) pamoja na Waziri anayeshughulikia masuala ya Muungano kule Zanzibar, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, muweze kukaa kuangalia vipaumbele vya bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambavyo vina mnasaba wa kuangalia ushirikiano ambao unahitajika kwa upande wa Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nazungumza hili kwa sababu mara nyingi bajeti ya Zanzibar kuna maeneo ambayo kwa kweli kama haikupata msukumo wa Waziri wa Fedha pamoja na Sekta za Muungano huku Tanzania Bara basi bajeti ile inakuwa ina kasoro na mambo mengi yanakuwa hayawezi kutekelezeka vyema. Kwa hiyo, naomba tu Mheshimiwa Waziri hili ukali-note ukimaliza usisubiri upate mualiko, mtafute mwenzako Waziri wa Fedha muweze kukaa kitako pamoja muangalie vipaumbele ambavyo vinahitaji ushirikiano muweze kuvitekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala muhimu ambalo pia ningependa kuligusia. Wakati Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano Hayati Magufui Mungu amrehemu anazindua Bunge la 12, alisisitiza sana ushirikiano wake kwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na hili kwa kweli mimi siiti ile ni hotuba ya kulizindua Bunge, naiita ni hotuba ya kutuusia kwa sababu kama alijua kwamba anaondoka basi niwausie au niwaase vipi Watanzania wakati naondoka waishi vipi hasa katika masuala ya Muungano. Hali kadhalika wakati anamuapisha Waziri Mkuu kule Chamwino pia alimkaribisha Mheshimiwa Rais wa Zanzibar kuweza kueleza machache na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar alitumia muda mwingi kuweza kuomba ushirikiano na kuungwa mkono na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, ningependa tuzidishe kuziunga mkono zile sekta na taasisi za Zanzibar katika masuala ambayo yanahitaji ushirikiano wa Kimuungano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kuna Sekta ya Kilimo na Mifugo. Sekta hii siyo ya Muungano lakini kuna changamoto kama wenzetu wa Mambo ya Ndani hawakuisaidia, basi wananchi wataendelea kupoteza nguvu zao bure na tija ya kilimo na mifugo haitaweza kupatikana Zanzibar.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli kwa kipindi kirefu na hata Rais wa Zanzibar wakati ananadi sera za Chama cha Mapinduzi aliahidi hili kwamba atajitahidi kuhakikisha kwamba kero za wizi wa mazao ya kilimo na mifugo inapungua. Kwa kweli, kwa tatizo kubwa la wizi wa mifugo na mazao ya kilimo Zanzibar na hata nafikiri Mheshimiwa Abdallah Mwinyi ni shahidi. Jimboni kwake kule kuna mwannachi wake mmoja alipoteza maisha kwa kulinda nazi. Amelinda nazi wakati mtu yuko juu kwenye mnazi anaangua basi yeye wakati analinda kuna mwizi mwingine akaja akampiga kisu na kumuua hapo hapo. Sasa kwa kweli ningeomba tu katika bajeti inayokuja Wizara ya Mambo ya Ndani ije ituambie mkakati ambao imeutumia katika kipindi hiki kuondoa tatizo la wizi wa mazao ya kilimo na mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu wameondokana kabisa na suala zima la ufugaji Zanzibar. Mtu alikuwa na mbuzi au ng’ombe wake watano, kule ufugaji wetu sio mkubwa sana lakini zizi zima limeenda kuchukuliwa wakachinjwa hapo hapo. Sasa nataka kuwauliza, hivi Jeshi la Polisi liko wapi? wakati watu wanajitahidi kulima wewe shamba lako zima unaenda asubuhi limeshavunwa lote, kama muhogo umeshavunwa wote. Kama viazi vimeshavunwa zote, kama nazi zimeshaanguliwa zote. Kwa hiyo, ina-disappoint au inakatisha tamaa wakulima kwa upande mmoja. Kwa hiyo, Wizara ya Mambo ya Ndani lazima tuje na mkakati tutalisaidiaje hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kwenda Misri, wenzetu kule ukitembea ndani ya dakika moja utakutana na Askari kwa sababu wanafahamu hali yao. Sasa na sisi Zanzibar Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani lazima uje na mkakati wa kulisaidia hili. Ni miongoni mwa kero ambazo Mheshimiwa Rais wa Zanzibar ameahidi kwenda kuzifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Donge, nafikiri kama ningekuwa Tanzania Bara tungeweka miongoni mwa Mikoa mitano ambayo inalisha nchi. Jimbo la Donge ni miongoni mwa Jimbo ambayo Mungu kayajaalia kuyapa rutuba ni miongoni mwa maeneo ambayo ni big fertile land lakini kwa kweli kumekithiri wizi kiasi kwamba hata ukilima basi huna uhakika wa kuvuna. Mazao yanavunwa usiku, yanavunwa machanga kiasi kwamba tija ya kilimo na mifugo haionekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nazungumzia hilo, ningependa vile vile kuzungumzia suala jingine la kuzishika mkono Sekta za Zanzibar. Zanzibar tuna miundombinu ya barabara ambazo ni main road hazizidi kilometa 700, Zanzibar nzima yaani hiyo. yaani ukitoka Mjini Zanzibar kwenda Nungwi, Mjini Zanzibar kwenda Makunduchi, Mjini Zanzibar kwenda Chwaka na ukitoka Wete kwenda Mkoani, Wete kwenda Makangale, Wete kwenda Micheweni ni kilometa zisizozidi 700. Lakini tumekuwa tukihangaika na barabara hizi kwa miaka sasa hivi, toka mapinduzi hatujaweza kumaliza kwa sababu hali ya Zanzibar kama hatukuishika mkono kuweza kuikamilisha vizuri ile miradi ya kimkakati ni ngumu. Kwa hiyo, ningeomba sana hii miradi ya wahisani ambayo inapitia katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tuiangalie sana Zanzibar kwa sababu kinyume chake ina-disappoint maendeleo ya Zanzibar kwa asilimia kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Kwanza aliisaidia Zanzibar kuipa eneo Makurunge kule. Lile eneo akasema chukueni fugeni ng’ombe ili Zanzibar iondokane na matatizo ya nyama ya ng’ombe na maziwa. Ile ni spirit ambayo sisi hivi sasa lazima tuiige. Kwa hiyo, naomba Mawaziri na uongozi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivi sasa tuige spirit ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Awamu ya Kwanza ya kupenda kuisaidia Zanzibar kuwa ni kama economic hub kwa East Africa. Tukiitengeneza Zanzibar ikawa ni economic hub itakwenda kuisaidia Tanzania Bara vilevile. Lakini matatizo ya Zanzibar vilevile yatakwenda kuhatarisha na kuongeza changamoto za Muungano vilevile. Kwa hiyo, ningependa tukalisaidia hili nalo kwa sababu lina umuhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Waziri wa Fedha amesaidia zile pesa za Majimbo zile Milioni Mia Tano ukisaidia Zanzibar hutapoteza kitu kwa sababu ndiyo ile spirit Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Kwanza ameifanya kwa kuipa Zanzibar ardhi ndani ya Tanzania Bara. Wewe ukipeleka zile fedha Milioni Mia Tano ni ile ile spirit ambayo ameifanya Mwalimu Nyerere kipindi hicho kwa kuipa Zanzibar ardhi huku.

Kwa hiyo, utakuwa hujafanya kosa kubwa Mheshimiwa, iga huo mfano ili na wewe uache legacy ambayo Zanzibar itakukumbuka miaka 50 inayokuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kumalizia kuhusu fedha za mifuko. Nimeshukuru sana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Naunga mkono hoja. Ahsante sana.