Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Msalala
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa hii nami kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Msalala kuchangia juu ya bajeti hii ya Wizara ya Mipango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita katika maeneo matatu kama muda utaniruhusu, na nianze moja kwa moja kwa kujikita katika suala zima eneo la madini. Lakini nianze kwa kumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika Taifa letu la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitachukua nafasi hii kukishukuru Chama changu cha Mapinduzi kwa ajili ya kuniamini mimi na kuwawakilisha wananchi wa Jimbo la Msalala lakini pia kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kuifanya. Tumeona Katibu Mkuu na Sekretarieti nzima ikizunguka kwa ajili ya kuinadi na kuisimamia Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii pia kuwapongeza Mawaziri na wafanyakazi wote wa Wizara ya Madini. Pia nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutupatia fedha kiasi cha shilingi 500,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa kilometa Moja barabara ya lami katika Kata ya Bulyanhulu. Kwa hiyo, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuona namna gani sasa wananchi wa Bulyanhulu wanasumbuliwa na vumbi na kutupatia kiasi cha shilingi 500,000,000 walau tuweke kilometa moja ya lami katika eneo lile ili tuweze kupunguza vumbi lile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya. Lakini pia niendelee kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kutupatia shule moja ya sekondari ambayo tunaenda kuijenga katika Kata ya Ikinda ambayo itapunguza adha ya ukosefu wa shule katika Kata ile ya Ikinda. Lakini niendelee kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais na Wizara kwa kutupatia kiasi cha shilingi 1,000,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali yetu ya wilaya. Hivyo hivyo, nimpongeze Mheshimiwa Rais tena kwa kutupatia kiasi cha shilingi 750,000,000 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la utawala katika Wilaya yangu ya Msalala. Nimpongeze pia kwa kutupatia kiasi cha shilingi 500,000,000 katika ujenzi wa kituo cha afya kinachoendelea katika Kata ya Isaka. Mambo mengi Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametutendea katika jimbo langu la Msalala. Hivyo, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Msalala ninamshukuru na tunamshukuru kwa dhati Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kututendea wema huu katika Jimbo langu la Msalala. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende sasa moja kwa moja kuchangia katika Sekta hii ya Madini. Sekta ya Madini kama mnavyofahamu imetembea katika misuko suko mikubwa sana mpaka hapa ilipofikia. Sekta ya Madini imekabiliwa na changamoto nyingi, nimshukuru Waziri wa Madini kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya kuhakikisha kwamba sekta hii ya Madini inasimama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kuchangia nimeona hapa kwenye bajeti hii kuna tozo ambayo inaenda kuanzishwa kwa wachimbaji wa madini wadogo wadogo na hii Mheshimiwa Waziri nikuambie ukweli, hii tunayoenda nayo kwa sasa ambayo inawataka wachimbaji wadogo wadogo wenye makusanyo yasiyozidi milioni mia moja kwenda kulipa tozo ambazo zimeorodheshwa hapa. Hii kiukweli tunaenda kuua Sekta hii ya Madini. Sekta ya Madini Mheshimiwa Waziri nikuambie ukweli, Sekta ya Madini kwa sasa tunaona kabisa kwamba Wizara zingine zote, Sekta ya Madini wameiona sasa kama ni Sekta ambayo ya kwenda kukusanya fedha. Sekta ya Madini tunakabiliwa na changamoto nyingi sana hasa za kikodi. Kuna kodi nyingi sana katika Sekta ya Madini na ili Sekta hii iende ikasimame ni lazima tuone namna gani tunaenda kuisaidia sekta hii katika kupunguza gharama na tozo mbalimbali zilizoko hapa.
Mheshimiwa Waziri, leo hii tunakwenda kumwambia mchimbaji mdogo mdogo anapokwenda kuuza madini yake katika soko la dhahabu aende akakatwe tozo ya zuio la ajira. Leo hii tutambue Mheshimiwa Waziri, huyu mchimbaji mdogo mdogo kwanza hana maeneo ya kuchimba ambayo ni rasmi na utaratibu unaotumika kule ni kwamba mtu anayemiliki leseni ni tofauti kabisa na mchimbaji mdogo mdogo anayechimba katika leseni ile. Sasa, baada tu ya huyu mchimbaji mdogo mdogo kuchimba madini yake kunakuwa na migao mingi ambayo kimsingi inaenda kufanyika pale kabla hata ya kwenda sokoni kuuza dhahabu yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wachimbaji wadogo wadogo hawajaajiri watu, wanapochimba mathalani mchimbaji ametoa mifuko 100 kwenye shimo lake, hapo hapo anakatwa mifuko kwa ajili ya mmiliki wa leseni mifuko ishirini na zaidi. Hapo hapo anakatwa kwa ajili ya ulinzi, hapo hapo anakatwa kwa ajili ya wafanyakazi, hapo hapo wanamalizana. Maana yake ni kwamba mtu anapotoka na dhahabu yake mchimbaji mdogo mdogo huyu kwenda sokoni ameshamalizana na mambo mengine yote huku. Unaendaje kumkata tena fedha pale kwenye soko la dhahabu anapouza kwa ajili ya kulipa zuio la ajira? Mheshimiwa Waziri nikuombe hebu nendeni makapitie upya mapendekezo haya mliyoyaleta yanaenda kuua Sekta ya Madini. Sisi kama wachimbaji wadogo wadogo tuko radhi kuhakikisha ya kwamba tunalipa kodi. Lengo la kuanzishwa masoko haya ni kudhibiti utoroshwaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa kodi hizi zinazoendelea kuwekwa hapa inaenda kufungua tena milango ya kuhakikisha kwamba utoroshaji wa dhahabu unaendelea. Nikuombe Mheshimiwa Waziri, nenda kapitie upya. Hili suala haliwezekani, wachimbaji wadogo wadogo hawa wasiopitia mauzo ya chini ya milioni 100 hawawezi wakalipa mambo yote hapa, hapa yamewekwa kuna kodi inakatwa asilimia tatu ambayo kodi hii tayari ameshailipa kule mifuko. Imewekwa hapa anatakiwa akatwe kodi ya mapato ya ajira, huyu anamuajiri nani mchimbaji mdogo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikuombe chonde chonde twendeni tuhakikishe ya kwamba tunaenda kuondoa kodi hizi ili kumrahisishia mchimbaji mdogo mdogo. Lakini pia niiombe Wizara badala ya kujikita kuongeza kodi hizi tujikite katika kuhakikisha ya kwamba tunaenda kuwajengea uwezo wachimbaji wetu hawa wadogo wadogo. Leo wachimbaji wadogo wadogo wanahangaika na ukosefu wa mitaji, wanahangaika na ukosefu wa maeneo sahihi ya uchimbaji, tafiti hazitolewi kuwawezesha wachimbaji wadogo wadogo hawa ili waweze kuchimba maeneo sahihi, hazitolewi. Leo hii tunaenda kuongeza kodi tena. Mheshimiwa Waziri nikuombe, kuna maeneo mengi ya kwenda kukusanya kodi na siyo maeneo haya. Mheshimiwa Waziri, ukipiria ripoti ya CAG imeonesha kuna kampuni kubwa zipo ambazo kimsingi zinaweza zikachangia ongezeko la kodi na mapato katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Ripoti ya CAG imejieleza hapo. Imetueleza kuna kampuni za Kimataifa zinafanya kazi hapa na kampuni hizi kwa sasa ukiangalia uwezo wake ukisoma Ripoti ya CAG kuna kampuni zaidi ya 504 ambazo zipo na kampuni hizo ni zaidi ya 116 mpaka 154 hazijafanyiwa ukaguzi. Hebu twendeni tukajikite katika kuhakikisha ya kwamba kampuni hizi zinazoanzisha shughuli hizi za utoroshaji wa mapato twende tukatafute fedha kule tuwaache wachimbaji wadogo wadogo waweze kunufaika na rasilimali za nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikuombe angalieni namna gani mnaenda kutupatia mitaji. Leo hii tunazungumzia habari ya mitaji kuna fedha zinatolewa asilimia 10, asilimia Nne zinaenda kwa vijana, asilimia Nne zinaenda kwa akina mama. Leo hii mchimbaji mdogo mdogo anayekopeshwa fedha hii anaenda kuchimba, bado hujajua kwamba ametumia gharama kiasi gani katika ku-invest, wewe unaenda kukaa katika soko kusubiri sasa umkate tozo ya ajira, umkate kodi mbalimbali bila kuangalia ametumia gharama kiasi gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe hebu twende tukapitie upya mapendekezo haya. Mimi siyaungi mkono mapendekezo haya Mheshimiwa Waziri na nitashika shilingi. Nendeni, ukija hapa Mheshimiwa Waziri njoo na majibu ya namna gani unaenda kutusaidia wachimbaji waodgo wadogo na mkaondoe tozo hizi. Haya masharti ni magumu mno.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunapozungumza Mheshimiwa Waziri mimi jimbo langu lina mgodi wa Bulyanhulu pale na Bulyanhulu kuna kampuni ambayo imeanzishwa Mheshimiwa Waziri iko pale. Wamezanzisha kampuni mbili kwa ajili, naweza kusema utoroshaji wa fedha. Kuna kampuni moja imeanzishwa ya TSL ambayo iko nje huko. Lengo la kampuni hii ni kupata purchasing activities ambazo zinaendelea. Lakini pia kuna kampuni nyingine TSL imeanzishwa Dar es Salaam hapa, leo hii mama ambaye analima nyanya Bulyanhulu hawezi akauza nyanya zake pale mgodini inatakiwa aende Dar es Salaam kwenye kampuni hiyo iliyoko kule na nyanya anapouza wale kazi yao ni ku- maximize profit tu kuongeza bei na kuhakikisha kwamba wanatorosha fedha katika maeneo yale. Nikuombe Mheshimiwa Waziri chonde chonde, sisi kama wachimbaji Mheshimiwa Waziri tuko tayari kulipa kodi lakini hatuko tayari kulipa kodi za namna hii. Nikuombe, sheria hii na mapendekezo haya yaende yakafutwe, yanaenda kuua Sekta ya Madini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Mheshimiwa Waziri amenielewa katika Sekta ya Madini. Sasa niende katika kuzungumzia suala zima la biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Tanzania ukiiangalia hapa tumezungukwa na nchi jirani. Mimi nilipata bahati ya kutembea kwenda Dubai nikaona namna gani wanafanya. Kuna maeneo mengi Mheshimiwa Waziri nikuombe, leo hii hapa unaona watu wa kutoka Uganda, Rwanda, kutoka maeneo mbalimbali wanaenda Dubai kwenda kununua magari wanayaleta yanapita hapa na yanaondoka. Hivi, kwanini kama Serikali Tusianzishe utaratibu wa kuwaruhusu watu hawa wanaoingiza magari wafungue yards kubwa hapa wasitozwe ushuru kwanza, watozwe tui le kodi ambayo kimsingi mteja akienda kununua gari lake ndiyo atozwe kodi. Maana yake ni kwamba tutawarahisishia watu wanaotoka Uganda, wanaotoka Burundi na maeneo mengine kuishia hapa nchini kwetu Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri nikuambie watu wakazi wa Isaka tuko tayari kutoa eneo tuwaite hawa watu ondoeni kodi za magari watu walete hapa magari yao waweke. Mteja akienda pale anaponunua gari lake basi aweze kutozwa kodi na wale wanaotoka nchi jirani wanapokuja kununua magari hapa wasitozwe kodi wapeleke huko, hii itasaidia kuongeza mapato katika nchi yetu hii ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niende kwenye suala zima la kilimo. Tumeona mnajitahidi na nipongeze wakati tunajadili bajeti ya kilimo hapa watu wengi wamezungumzia walikuwa wanalia kilimo, kilimo, kilimo, lakini mimi nizungumze mambo mawili tu; katika kilimo hapa ni lazima tuone namna gani tunaenda kutengeneza masoko, issue sio mbegu, mbegu wananchi tunaweza tukanunua, lakini issue ni masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi leo ninapozungumza hapa kwenye Jimbo langu la Msalala wengi ni wakulima wa mpunga. Ukiangalia Kata ya Mwaruguru, Kata ya Jana, Kata ya Mwananse, Kata ya Kashishi, wote ni wakulima wa mpunga na tunavyozungumza hivi bado wana stock ya mwaka jana na bado wana stock ya mwaka huu na wameamua baadhi yao kutelekeza mpunga wao mashambani kwa sababu hawana sehemu ya kuupeleka na bei bado iko chini. Kwa hiyo, niwaombe namna gani Wizara inaweza kujikita katika kuhakikisha ya kwamba mnaenda kututafutia soko la kutusaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii Serikali imekuwa inakuja pale ambapo wananchi wanavuna ndio inaingia, lakini ni namna gani inamsaidia huyu kutafuta soko na kuhakikisha ya kwamba inamsaidia kwenye kumkopesha ili aweze kufanikiwa, hakuna. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri na niwaombe Wizara ya Kilimo hebu njooni sasa mfanye walau research katika Jimbo langu la Msalala ili muwasaidie wananchi hawa muone namna gani wanaweza wakauza mpunga wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni aibu leo gunia la mpunga mwananchi anauza kwa shilingi 36,000 lakini bado kuna matapeli wameibuka humo humo. Leo Serikali imepiga marufuku lumbesa, lakini viwanda vimeibuka sasa kuanza kutengeneza mifuko ambayo inabeba madebe kuanzia nane, wanaenda kumdhulumu mkulima. Niwaombe Wizara na wanaohusika njooni basi katika Jimbo langu la Msalala muone namna gani wakulima hawa tunaweza kuwasaidia ili waweze kuuza mazao yao kwa bei iliyokuwa nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kingine niseme tu kuna matapeli wamo katika Wizara ya Kilimo na maeneo mengine. Ili tuweze kufanikiwa katika sekta ya kilimo; moja ni tunaweza kutafuta masoko nje ya nchi. Leo hii watu wanatoka nje kuja kufanya biashara ya mazao, kuna watu wanakuja kuwatapeli, ku-destroy image ya nchi; Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo uko hapo unanisikia, leo hii kuna watu wamekuja hapa kufanya biashara ya ufuta, Mheshimiwa Naibu Waziri ananisikia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa wamekuja kutuamini hawa wakatoa fedha zao hapa na wametapeliwa, chukueni hatua kwa watu hawa. Kesi hii Mheshimiwa Waziri bado inasumbuliwa, watu hawa wamedhulumiwa zaidi ya dola laki nne watu wamedhulumiwa na wafanyakazi hao wapo kwenye ma-go down wanawaleta watu kutoka nje, wanawaleta kuwaonesha kwenye ma-go down ya ufuta yale na wanawaambia ufuta huu sisi ndio tunaweza kuuza, wanapewa advance, kufanya hivyo ni ku-destroy image ya nchi na masoko katika nchi yetu hii Mheshimiwa Waziri. Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo uko hapo, hebu ninaomba hili suala lichukulie hatua, limeenda TAKUKURU, limeenda wapi, lakini hakuna majibu watu wanalia kutafuta fedha zao. Huyo aliyechukua fedha hizo Mheshimiwa Waziri mchukulieni hatua arudishe fedha, anaharibu taswira ya nchi Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo ninaomba kuunga mkono hoja na ahsante sana. (Makofi)