Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kiembesamaki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MOHAMED MAULID ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi kunipa ruhusa ya kuweza kuchangia siku ya leo Ijumaa, siku tukufu, asubuhi hii.
Kwanza ningependa kutoa shukrani au pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Waziri Mdogo au Naibu Waziri Mheshimiwa Masauni pamoja na timu nzima ambayo imejikita kutengeneza bajeti hii. Kwa kweli, ni bajeti ambayo tunaweza kusema haijawahi kutokea, tunawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi mchango wangu nianze kwenye TARURA. Napenda sana kuwashukuru viongozi wetu, pongezi kwa Serikali ambayo imehusisha vilio vya Wabunge moja kwa moja kuhusu fedha za TARURA, hii imetupa faraja kubwa sana. Ningependa kuwatoa hofu wananchi waelewe kwamba fedha ambayo imetengwa kwa ajili ya TARURA ambayo inatoka kwenye mafuta inakwenda kutuhusisha sisi kama Wabunge moja kwa moja na kutupa ujiko kule majimboni kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningewashauri sana Wabunge wenzangu tusiingilie sana katika kuwaambia wananchi kwamba fedha hii itasumbua katika matumizi au kuongeza gharama, si kweli, fluctuations katika pesa za mafuta ni jambo la kawaida kila siku na halileti athari yoyote kwenye matumizi. Kwa hiyo, tujikite zaidi kuwaelimisha wananchi kama Serikali ilivyotusaidia sisi kutuchangia, ili na sisi twende kifua mbele majimboni na sisi tuisaidie kuwaelimisha wananchi kwamba hili jambo litatusaidia sote kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilikuwa nataka kuzungumzia suala la ajira 8,000 ambazo Serikali…, samahani ni ajira milioni nane ambazo zimeainishwa kwenye ilani yetu ya uchaguzi. Kwa kupeleka fedha hizi TARURA zile ajira milioni nane ambazo zimezungumzwa katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi sasa nina hakika zitatekelezeka sawasawa. Ndani ya kipindi kifupi tutaweza kuona viwanda vyetu vipo tayari, malighafi kule vijijini kwa ajili ya viwanda hivi zitakuwa tayari, lakini hata barabara na viungo kati ya viwanda na upatikanaji wa malighafi zitakuwa tayari. Hongera sana Mama Samia kwa maono ya mbali kwa maslahi ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilikuwa nataka kulizungumza kuhusu fedha shilingi milioni 500 kwenye majimbo yetu. Fedha hizi kwa kweli, zitakwenda kusaidia tena zitakwenda kusaidia sana katika majimbo haya kwa sababu sisi kama Wabunge sasa zitatupa nguvu na zitaweza kutusaidia hata katika chaguzi zinazokuja mbele za mwaka 2025. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya sana Majimbo yetu yote ya Uchaguzi matatizo yake yanafanana na kilio kikubwa cha wananchi ni barabara kama yalivyo majimbo mengine yeyote Tanzania Bara na sisi tuna changamoto hii kule Zanzibar. Ningependa kuwahakikisha kwamba Halmashauri zetu na Manispaa hazina uwezo wa kutengeneza barabara hizi haitapendeka kama tutakuwa huku barabara zake zinaonekana vizuri kwetu kule hakupitiki, lakini Mbunge ni yule yule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama alivyo Mbunge mwingine yeyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili tunamwomba sana Mheshimiwa Mwigulu, Rais wetu ni msikivu sana na yeye ni mwelewa na viongozi wetu Mawaziri na hata hao Manaibu Waziri, nao ni wahanga vile vile wa jambo hili, ingawa midomo yao wameipiga zipu, lakini ukweli wote tunaathirika kwa pamoja lazima tuseme ukweli. Ikimpendeza Mheshimiwa Waziri suala hili nasi tuweze kusaidiwa ili twende kifua mbele. Huko majimboni kwetu wananchi wanafuatilia sana vikao hivi, tena wanavifuatilia kwa nguvu zote, wanatuuliza maswali mengi kuhusu fedha hizi ambazo kwakweli hatuna majibu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanaamini na wao vile vile majimbo yao yatanufaika, lakini kwa kweli upande wetu ni mgumu kidogo. Nomba Serikali yetu sikivu chini ya uongozi wa Mama Samia, Waziri Mkuu, Waziri Mwigulu, Manaibu Mawaziri ambao kama nilivyosema baadhi yao ni wahanga wa tatizo hili, watufikirie sisi Wabunge wa Majimbo ya Zanzibar na sisi tuyahudumie majimbo haya ili yaweze kupitika muda wote hasa wakati wa kipindi cha mvua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ningependa kuzungumza…
T A A R I F A
MHE. SALUM MOHAMMED SHAAFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Karibu kwa taarifa Mheshimiwa.
MHE. SALUM MOHAMMED SHAAFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nimpe taarifa mzungumzaji juu ya jambo alilolizungumza, huko Majimboni kwao Zanzibar wananchi wanawauliza maswali na akasema hawana majibu juu ya hii fedha ya shilingi milioni 500 ya kila Jimbo. Naomba nimpe taarifa mzungumzaji majibu ya Majimbo ya Tanzania Bara na Majimbo ya Zanzibar majibu yake ni mamoja, sote ni Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na hakuna Mbunge wa Zanzibar wala wa Bara. Ahsante.
MWENYEKITI: Unapokea taarifa Mheshimiwa Mohammed Ali?
MHE. MOHAMMED MAULID ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema nimeipokea taarifa hiyo kwa mikono na miguu pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumzie kidogo kuhusu suala la ndugu zetu wa Bodaboda. Kwa kweli kwa nia njema kabisa Serikali imefanya kuwasaidia vijana hawa ili waweze kujikwamua kimaisha. Hii ndio nia njema kabisa ya Serikali ya Mama Samia. Tatizo moja tu ambalo ningependa kutoa tahadhari, kwanza kuna Mbunge mmoja amenifilisi kuhusu hizi bodaboda ambazo hazina makosa ya jinai. Vituo vyetu vya polisi sasa hivi havifagiliki havipitiki, kipindi cha mvua vichafu kwa sababu ya bodaboda hizi. Sasa ikiwezekana kama sheria inaruhusu maana yake siwezi kushindana na sheria…
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa. Sasa naomba nimwite Mheshimiwa Seif Khamis Gulamali.
MHE. MOHAMMED MAULID ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)