Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuweza kukushukuru kwa kupata nafasi ya kuweza kuchangia katika Wizara hii ya Afya. Awali ya yote nichukue nafasi hii kumpongeza Rais wangu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kasi kubwa anayoenda nayo ya kuhakikisha kwamba anatumbua majipu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niseme kwamba inashangaza kuona waliokuwa wakipiga kelele kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni dhaifu sasa wamegeuka wanasema kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi ni ya kibabe, wamegeuka wanasema kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi ina utawala wa kiimla. Nashindwa kuelewa ni kipi ambacho hawa wenzetu wanataka tuwasaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakumbuka kwamba siku zote wamekuwa wakipiga kelele na bahati nzuri Hansard za Bunge hili zipo wamekuwa wakisema kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeshindwa kabisa kukusanya mapato. Tumeshuhudia baada ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kasi yake ya kuendelea kutumbua majipu, TRA kwa mwezi Aprili wameweza kukusanya mapato ya shilingi trilioni 1.035. Hii yote ni matokeo ya kasi kubwa na uwezo mkubwa wa Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli lakini wenzetu hawa wamegeuka wanasema kwamba Serikali hii ni ya kibabe inatumbu majipu hovyo, hali hii inasikitisha. Kwa sisi kama wanasiasa vijana tunashindwa kujua nini hasa ambacho tutajifunza kutoka kwa hawa wenzetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba sasa nijielekeze kuzungumzia Wizara ya Afya. Kwa kuzingatia kwamba mwaka 2015 ilikuwa ni ukomo wa kuweza kufikia Malengo ya Milenia ambapo Lengo Kuu la Tano ilikuwa ni kuhakikisha kwamba tunapunguza vifo vya akina mama kufikia asilimia 75. Mpaka sasa hivi takwimu zinaonyesha kwamba vifo vya akina mama kila mwaka ni zaidi ya 15,000. Hali hii inatisha sana, inatisha kwa sababu akina mama wetu kule vijijini wanapata shida sana inapofika suala la huduma za kiafya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiacha kwa kina mama ukija kwenye vifo vya watoto, takwimu zinaonyesha kwamba ni zaidi ya watoto 40,000 kila mwaka wanafariki ndani ya saa 24. Takwimu hizi sisi kama Taifa hatupaswi kabisa kuweza kuzifumbia macho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile takwimu zinaonyesha kwamba akina mama 250,000 kila mwaka wanapata vilema vya uzazi, hali hii inasikitisha sana.
Mimi niombe Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, Serikali ambayo ni sikivu iweze kuwahurumia kina mama hawa mfano mama zangu wa kule Songwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niishukuru sana Serikali kwa sababu imeweza kutupatia mkoa. Mkoa wetu wa Songwe, ni mpya lakini kama unavyojua changamoto ni kubwa kwa hii mikoa mipya. Mkoa wa Songwe hatuna kabisa Hospitali ya Mkoa, hiki ni kilio chetu, mimi nikiwa kama mwakilishi wa akina mama wote wa Mkoa Songwe naomba utusaidie katika jambo hili. Nashukuru kwa sababu Waziri wa Wizara hii ni mwanamke mwenzetu, Wanawake wa Mkoa wa Songwe wanapata shida sana, tunaomba na sisi muweze kutufukiria muweze kutujengea Hospitali ya Mkoa ili basi akina mama wale waweze kupata tiba kiurahisi. (Makofi)
Mheshimiwa mwenyekiti, vilevile katika Wilaya ya Momba ambayo ni Wilaya mpya, cha kushangaza mpaka leo hii hatuna kabisa Hospitali ya Wilaya. Unaweza ukaona akina mama wa Wilaya ya Momba wanapata shida kiasi gani? Wilaya ile hakuna Hospitali ya Wilaya na sera katika Wizara ya Afya inasema kwamba ni kuhakikisha kwamba kila Halmashauri kunakuwa na Hospitali ya Wilaya. Halmashauri ile ya Momba mpaka leo hii hakuna kabisa Hospitali ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Kituo cha Afya pale Tunduma lakini ni kidogo, hakiwezi kutosheleza kuweza kuhudumia Wilaya nzima. Ni kituo ambacho kwa sasa hivi kinatumika kama Hospitali ya Wilaya ya Momba lakini kina changamoto nyingi. Naomba Waziri aweze kukiangalia Kituo kile cha Afya cha pale Tunduma. Kituo kile hakina madaktari wa kutosha, hakina x-ray za kutosha, ukiangalia hata sehemu ambako mama zetu wanaenda kujifungulia kwa kweli hali pale inasikitisha. Inafika mahali mama mjamzito anayeenda kujifungua katika kituo kile lakini hakuna sehemu ambayo mama huyo anaweza akaendelea kujisubirishia wakati anasubiri kwenda theater. Naomba sana Serikali iweze kukiangalia kile kituo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi navyoongea kuna vitanda vinne tu vya akina mama kujifungulia. Hicho ni kituo cha afya ambacho kinatumika kama hospitali ya wilaya lakini chagamoto zake ni kubwa mno. Mpaka sasa hivi kuna vitanda vitano tu ambavyo vinatumika kwa akina mama kupumzika baada ya kuwa wameshamaliza kujifungua. Kama unavyojua mama akishamaliza kujifungua inatakiwa akae chini ya uangalizi wa daktari si chini ya saa 24 lakini kwa sababu ya uhaba wa vitanda wanawake wale wanalazimika kutolewa ndani ya saa mbili, tatu kurudi nyumbani. Naomba sana suala hili liangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nichukue nafasi hii kuweza kukumbusha ahadi ya Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni. Alipita pale Momba na kwa bahati nzuri pale Momba tuna majengo yako pale Chipaka. Majengo yale yalikuwa ni ya wakandarasi yameachwa pale, ni makubwa mno yanafaa kabisa kuweza kutumika kama hospitali ya Wilaya. Jambo zuri ni kwamba Mheshimiwa Rais alituahidi kwamba majengo yale ataweza kuyakabidhi kwa Serikali ili yaweze kutumika kama Hospitali ya Wilaya. Nimesimama mahali hapa kwa niaba ya wanawake wote wa Mkoa wa Songwe kuweza kumkumbusha Mheshimiwa Rais akumbuke ahadi yake aweze kuwapatia akina mama wale majengo yale ili basi Wilaya ya Momba tuweze kuwa na Hospitali ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nizungumzie kidogo Idara ya Maendeleo ya Jamii. Idara hii ni muhimu sana kwa Taifa letu na ni mtambuka. Huwezi kwenda vijijini kwenda kutoa elimu ya ujasiriamali kwa akina mama kama hujatumia idara hii. Nionyeshe masikitiko yangu makubwa kwamba idara ile imesahaulika sana, wale Maafisa Maendeleo wamekaa pale kwenye Halmashauri hawana kazi, hawapelekewi pesa za OC ambazo zitawasaidia kushuka kule kijijini kuhakikisha kwamba wanatoa elimu ya ujasiriamali kwa akina mama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nawaomba Mawaziri wetu na nashukuru sana kwa sababu tuna Mawaziri ambao ni sikivu, dada yangu Ummy naomba sana wakati mwingine utakapokuwa ukitembelea hospitali unavyoenda unakutana na ma-DMO uchukue nafasi uweze kuonana pia na Maafisa Maendeleo ili waweze kukupa changamoto zao. Wamekaa pale Halmashauri hawana kazi, wanalia sana, kilio chao wanaomba ukisikie na mimi nina imani kabisa kwamba Serikali hii ni sikivu, itaweza kwenda kuwasikiliza na siku moja changamoto hizi zitafika mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine ni huduma ya afya katika Wilaya ya Mbozi. Wilaya ya Mbozi ndiyo makao makuu ya Mkoa wetu wa Songwe. Ukifika pale ile wodi ya kujifungulia kwanza ni ndogo mno, wanalala kitanda kimoja akina mama wawili, watatu, inafika mahali mpaka wengine wanajifungulia chini. Naomba Serikali na naomba Mheshimiwa Waziri aweze kutuangalia katika wodi ile ya akina mama pale Mbozi kwa kuiongeza ukubwa ili basi wa akina mama wale waweze kujifungua mahali ambako ni salama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naamini kwamba maombi haya yamezingatiwa na kilio cha akina mama wa Mkoa wa Songwe kitafika mwisho, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.