Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hotuba hii nzuri na kihistoria. Nianze kwa kumpongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa namna ambavyo ameanza vizuri; kwanza kuendeleza miradi mikubwa ile ambayo awamu iliyotangulia ilikuwa imeanza nayo. Nampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza pia Mheshimiwa Waziri na Watendaji wote wa kwa bajeti nzuri waliyotuletea, iliyochukua mawazo ya Waheshimiwa Wabunge. Niliwahi kusimama hapa nikauliza, ni kwa asilimia ngapi michango ya Wabunge inachukuliwa kufanya matengenezo kwenye mipango ya Serikali? Sasa naomba nipongeze sana kwamba wamechukua kwa asilimia kubwa mawazo yetu. Kwa msingi huo, nianze kwa kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Siyo tu kwamba naunga mkono hoja, ni wa sababu nimeona kwenye bajeti hii Jimbo letu la Hai tumetengewa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye sekta ya viwanda tumetengewa shilingi bilioni 1.6 kwa ajili ya kufufua kiwanda cha Machine Tools. Siyo hivyo tu, tumepelekewa fedha kwenye elimu na barabara. Wananchi wa Jimbo la Hai wameniambia niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuunga mkono, narudia tena kumpongeza Mheshimiwa Rais. Niseme, akina mama popote mlipo Tanzania, huu ni wakati wenu wa kuiga mfano mzuri na kila mmoja ambaye anafanya shughuli yake afanye kwa ujasiri kwamba akina mama wanaweza. Siyo kwa sababu mimi ni kinara wa kutetea haki za akina mama na watoto, siyo hivyo tu ni kwa sababu ya kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme jambo, kwa msingi huo huo tu, tunaye baba yetu ambaye ndiye anamshauri Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan kufanya haya. Naye nampongeza sana. Kwa heshima hiyo, namwomba Waziri; sasa hivi tunajua kwenye mikopo ile ya Halmashauri asilimia zile 10, akina mama wanapata, walemavu wanapata na vijana. Kwa msingi huo huo kwa sababu kuna baba anayemshauri vizuri mama, hebu akina baba na wenyewe waingizwe kwenye kundi hilo wapate mikopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nishauri kuhusu bajeti hii. tumeambiwa hapa tunapanga kuongeza pato la Taifa mpaka kufikia kwenye asilimia sita na ushee. Mimi naona hii ni ndogo kwa sababu kama tutafuata maelekezo ya Mheshimiwa Rais kuwekeza kwenye kilimo, tunaweza kuvuka lengo hili. Hakuna namna yoyote tunaweza kuepuka kuinua uchumi wetu tukaacha kilimo nyuma, haiwezekani. Tunaambiwa asilimia 25 ya pato la Taifa linatokana na kilimo, lakini ukienda kuangalia ni wangapi wanashughulika na biashara hii? Utakuta ni eneo dogo sana. Naomba tuamue kwa dhati bajeti hii, fedha ambazo zimetengwa kwenye eneo la kilimo zije kwa asilimia 100 zote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo zuri tumeliona hapa. Wananchi wa Hai wamekuwa wakinipigia simu, vipi kuhusu tozo iliyowekwa kwenye umwagiliaji? Ile asilimia tano? Niseme, naiunga mkono Serikali tozo hii iwepo kwa sababu imehamishwa kule kwenye ushirika, imeletwa kwenye umwagiliaji. Kazi yake ni nini? Ni kuhakikisha wanajenga miundombinu, lakini fedha hii asilimia tano itafanya matengenezo. Jambo ambalo sasa hivi Serikali inajenga ile mifereji na zile skimu, lakini fedha za matengenezo haipo. Kwa hiyo, hii tozo iliyowekwa hapa itaenda kufanya kazi hiyo. Naomba ibaki hivyo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri nimezungumza vizuri na Naibu Waziri, Mheshimiwa Bashe akanihakikishia ile Mamlaka ya Umwagiliaji inaenda kuanzishwa, itafanya kazi hii. Kwa hiyo, naomba sana kwenye eneo la kilimo tuwekeze nguvu ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wetu wengi wapo huko kwenye majimbo yetu. Hawa tukiwawezesha kwa hatua ya kwanza; kwanza kufanya utafiti. Tuweke fedha nyingi kwenye utafiti, naona zimewekwa, zije kama zilivyo. Wakipewa fursa ya kufanya utafiti, tukahakikisha tunayo mbegu yetu, tuna watalaam wa kutosha kwenye kilimo, tuna maji ya kutosha, eneo linalobaki ni kuhakikisha tuna viwanda vya kuongeza thamani ya mazao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna namna tunaweza kuinua uchumi huu kama hatuongezi uzalishaji. Hili linawezekana. Mheshimiwa Mama Samia Suluhu leo akisimama akitamka kwamba jamani Waheshimiwa Wakuu wa Wilaya, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa mlioko huo, kila Mkuu wa Wilaya kwenye wilaya yake tunampa malengo ya kukusanya, kwamba kila msimu tunataka tani 300,000 za mahindi, hizi lazima zipatikane; za maharagwe kadhaa, baada ya kufanya utafiti, kila mmoja tunampa lengo lake. Watatuletea hizi tani. Wale ambao tunaona wanasuasua, basi zile kadi ambazo Mheshimiwa Waziri ulishauri, itumike moja. Wakipigwa wawili, watatu speed itaongezeka kuhakikisha wananchi wanafanya kazi ya kulima kuongeza uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kilimo hiki kitatusaidia mno. Pale Jimbo la Hai Mheshimiwa Waziri, mimi nakuhakikishia, nyie tuleteeni fedha. Fedha yenu itarudi. Tuleteeni fedha za kujenga skimu za kutosha zile tano za kimkakati, tuleteeni viwanda vya kuongeza thamani ya mazao sisi tulime, tuuze. Siyo tu kwa kuuza, kwa sababu pale Jimbo la Hai tumeweka mkakati, tuna soko hili naomba sana, sijaliona kwenye bajeti lakini uone namna ya kutafuta fedha popote lile soko la kwa Sadala lijengwe. Lile soko letu lina tofauti kidogo na masoko mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lile soko tume-design litauza yale mazao ya wananchi lakini kutakuwa na viwanda vidogo vidogo vya kuongeza thamani ya mazao haya. Kama ni nyanya, inaondoka pale ikiwa imepakiwa vizuri kwenda nje ya Nchi. Kwa hiyo, hapa tutatengeneza fedha. Lile soko ni la kwako kabisa, ni la kimkakati, ukilitumia vizuri litatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumze kuhusu kazi nzuri ambayo Serikali imefanya kwenye maslahi ya watumishi. Bajeti hii tunayoijadili hapa wanaokwenda kutekeleza ni watumishi. Nawashukuruni sana kwa kupokea mawazo yetu. Waheshimiwa Madiwani mmewajali, Maafisa Tarafa; na nakumbuka mimi ni Afisa Tarafa Mstaafu, kwa hiyo, nililisema kwenye Kamati na mmeliweka hapa. Endeleeni kuboresha maslahi ya watumishi kwa sababu hawa ndio ambao wanatufanyia kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine hapo kwa watumishi, kuna jambo ambalo halijakaa vizuri kuhusu promotion. Fedha zimeshatengwa hapa, mara nyingi sana humu ndani tunasimama tunasema shida ipo kwa Maafisa Utumishi. Naomba leo tuweke kumbukumbu sawa. Maafisa Utumishi wakimaliza kazi yao, kuna watu wanaitwa Approver wako pale Utumishi. Hawa lazima tutenge fedha za kutosha ili wawepo wa kutosha na speed ya kupandisha watu madaraja iongezeke na watumishi wetu waweze kufanya kazi kwa bidii na kwa speed ambayo inategemewa. Tukifanya hivyo, itatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona mikakati ambayo mmeweka ya kuongeza mapato ni nzuri sana. Awamu iliyopita kwenye tathmini tumeweza kukusanya kwa asilimia 86 mpaka kufikia Aprili, lakini mikakati tuliyoweka hasa pale bandarini, mmefanya jambo zuri sana la kutumia mifumo kukusanya. Ninaomba kuweka tahadhari kubwa ya kuangalia, hii mifumo tuhakikishe inafanya kazi masaa 24. Kwa sababu kosa linalotupata hapa ni kwamba wakati ambapo mifumo hii inasimama, ndiyo wakati tunapopigwa. Kwa hiyo, kama tumeamua kutumia hii mifumo, basi tuhakikishe mifumo hii inakuwa kamili kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sito tu pale bandarini, huku kwenye mahospitali yetu kuna makusanyo kwa kutumia mfumo wa GoT-HOMIS, ndiyo hali ipo hivyo hivyo, pale mfumo unapo-shake, tunaposema tunataka kwenda paperless, hawajajiandaa. Umeme unazimika, ndiyo fursa inatumika kutupiga. Kwa hiyo, naomba sana watu mitandao na mifumo wahakikishe tunakuwa na mifumo ambayo imesimama vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongezee hapa jambo. Niliwahi kusema humu ndani, hivi kuna shida gani kama tukiamua kuwa na mipango yetu ambayo itapangwa kwa kipindi cha miaka 50 na miaka 100? Nimejaribu kufanya tafiti, nimezungumza na maprofesa wa uchumi wananiambia jambo hili linawezekana. Ifike mahali Mheshimiwa Waziri, alika Maprofesa, alika wataalam wa uchumi, alika nchi nyingine duniani ambazo zimeweza kuwa na mipango hii. Hii itatusaidia sana kuwa na mipango ambayo itatekelezwa kwa kipindi cha muda mrefu lakini kuondoa utashi wa Kiongozi kufanya yale anayoyapenda yeye. Hii mipango itatusaidia kusukuma. Tunakuwa na mambo haya, tunasema hizi ni interest za Tanzania, ziwekwe hapa, tutatekeleza kwa kipindi cha miaka 50. Aje mweusi, aje mweupe atatekeleza, atalazimika kwa misingi ya sheria kuweza kutekeleza hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Hongereni sana kwa bajeti nzuri inayogusa maisha ya wananchi. (Makofi)