Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kwela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia kutoa mawazo yangu katika Bajeti Kuu ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii kufikisha salamu za wananchi wangu wa Jimbo la Kwela. Wamenituma nisimame ndani ya Bunge hili Tukufu nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Rais kwa mambo makubwa aliyotufanyia. Mwanzoni mwa Bunge hili nilikuja kulalamika, tulikuwa na maafa makubwa; madaraja karibia 18 yaliondoka katika Jimbo langu. Nashukuru Mheshimiwa Rais katika Awamu hii ya Sita ametutizama kwa jicho la huruma, ametuletea fedha takribani shilingi bilioni 3.6 za kwenda kurekebisha madaraja haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haitoshi katika barabara ya Kata 13 za Bonde la Ziwa Rukwa, Mheshimiwa Rais ametukumbuka katuletea shilingi bilioni 4.8. Kwa kweli wananchi wamesema tufikishie pongezi kupitia Bunge hili Tukufu ili Mheshimiwa Rais ajue Wana-Kwela wanathamini jinsi anavyowajali na anavyowakumbuka wakati wa matatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, isitoshe ametuletea shilingi bilioni moja kujenga ofisi ya Makao Makuu katika Mji Mdogo wa Laela na shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya miradi ya afya na elimu. Wananchi wa Jimbo la Kwela ndani ya kata zote 27 wanampongeza Mheshimiwa Rais, wanamwombea afya njema na siha, aendelee katika speed hii hii aliyoionesha ndani ya miezi hii mitatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, isitoshe, shilingi milioni 500 ambazo tumetangaziwa neema na Waziri, dada yangu Mheshimiwa Ummy Mwalimu, pia shilingi milioni 600 za barabara; na wananchi wa Jimbo la Kwela pia wanamshukuru Mheshimiwa Rais na timu yake ndani ya Serikali kwa namna ambavyo amekuja kwa kasi ya ajabu kuwaletea wananchi maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna shukurani ambazo nimetumwa na Waheshimiwa Madiwani wa Jimbo langu kwamba katufikishie salamu kwa kutukumbuka. Nasi tunaanza kulipwa kutoka kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina. Shukrani ya pekee wanaomba, angalau hii isiishie hapa, iwekewe sheria maalum ili kesho asije mtu mwingine akabadilisha kwamba hii ilikuwa batili. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, nakuletea hii habari ya Madiwani wangu, naomba uisikilize na mkaifanyie kazi, muifanyie reinforcement. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nitoe pongezi kwa Wizara hii ya Fedha. Nakupongeza ndugu yangu, First Class Economist, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, kwa kweli unaitendea haki hiyo First Class yako ya uchumi. Ndugu yangu kwenye Kamati yangu tulikuwa naye PAC, tulikuwa tunamwita Engineer wa Kamati ya PAC. Kweli kazi mnayoifanya kwenye Wizara hii ya Fedha mna- deserve sifa kubwa sana, mmetuletea bajeti ambayo ni realistic, ambayo inakuwa communicated. Tunai- communicate vizuri kwa wananchi na wameielewa. Naomba kwa spirit mliyokuja nayo mwendelee hivi hivi. Kweli Watanzania wanaanza kupata matumaini makubwa kutokana na bajeti hii ya kwanza katika Awamu hii ya Sita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kutoa pongezi zangu, nina mambo ya kuishauri Serikali. Naomba hapa tusikilizane vizuri kwa umakini mkubwa sana. Ni-declare interest kwamba, nisipoona mkulima wangu au wakulima ndani ya nchi hii wanatetewa, nakuwa mnyonge kwa sababu kwanza mimi binafsi ni mtoto wa mkulima. Nimekuja niongelee jambo moja kwa umakini mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, NFRA - Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula, ndiyo instrument pekee ya Serikali ambayo inaweza ikawa na touch au DNA na wakulima wetu kwa sababu hili ndilo soko la uhakika la wakulima kwa mazao yetu ya nafaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilikuwa napitia bajeti hapa. Tumewatengea bajeti ya shilingi bilioni 14. Mwaka wa fedha uliopita ilikuwa shilingi bilioni 15; kwa hiyo, kila mwaka tunapunguza kidogo. Miaka minne back hapo, tulikuwa tunawatengea shilingi bilioni 100. Sasa tunapoi-cripple hii NFRA maana yake tumeamua tuwazike wakulima wetu na hawa ndio wata-participate vizuri katika ku-implement bajeti hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tukafikirie, NFRA ina vyanzo vingi, achana na grant ya Serikali, wao pia walikuwa na room ya kwenda kukopa kwenye Commercial Bank. Mwaka 2019/2020, nina story naisikia kwamba mmewazuia Wizarani kwako Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, fieldmarshal, nasikia hamtoi vibali, wakakope. Wamekopa shilingi bilioni 35, lakini wamerudisha kwa uaminifu mkubwa, mpaka Commercial Bank nyingine wamethamini kwamba NFRA ni wateja wazuri. Hizi hela hawaendi kulipana posho, zinaenda kununua mazao hata kwa dada yangu, Mheshimiwa Jenista Mhagama. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana, nendeni mkatoe hicho kibali NFRA wakachukue hizo bilioni nyingi, warudishe kwa wakulima, wanunue mazao; na kwa sababu jukumu lao ni kutafuta masoko nje, wataenda kuuza huko, tutafanya recycling ya ile, itarudi tena kwenye mzunguko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sawa construction industry imefanya vizuri tume-invest mabilioni ya pesa; na ndiyo inafanya vizuri, ime-contribute asilimia 13 katika uchumi; kilimo 4.8; lakini investment kwenye kilimo ni short term investment ambayo impact yake tunaiona kwa haraka. Msiwanyime, waende kwenye Commercial Bank na ziko willing kutoa hiyo mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nawaomba kabisa, ndugu zangu naamini ninyi ni wasikivu, naombeni msikilize ili mkawakomboe wakulima. Kwa sababu mtapopeleka fedha ile tunaongeza purchasing power yao na ndio hao wataweza kuonja kwamba tuko kwenye uchumi wa kati, kwa sababu ya fedha zile tulizowapelekea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo moja ambalo limekuwa likisikitisha na hili naomba niongee nikutwishe mzigo dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama. Kutokana na ripoti ya CAG, inaonesha NFRA ilikopwa na Kitengo cha Maafa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, shilingi bilioni 167. Hizi zinanunua karibia tani 365,000. Sasa miaka 12 hamjarudisha hata senti moja, nendeni mkaweke utaratibu mzuri tukawalipe walau kwa installment 12 years, hawarudishiwi kitu chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutai-paralyse hii institution ya NFRA ambayo ni muhimu sana kwa wakulima wetu masikini wakiwemo wakulima wa Mkoa wa Rukwa, Ruvuma, Njombe na Iringa wanaitegemea sana NFRA. Nawaomba mwende kama Wizara, m-discuss jambo hili muone ni namna gani ambayo mtarudisha hizi fedha kwa wakulima. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULAMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu.
T A A R I F A
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULAMAVU: Namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa kukumbusha hilo deni ambalo anasema limejitokeza kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu. Naomba tu kumpa taarifa kwamba deni hilo ni yale mahindi ambayo yanakwenda huko huko kwenye Halmashauri za Waheshimiwa Wabunge ili kushughulikia matatizo mbalimbali wakati wa maafa na vitu vya namna hiyo, lakini hasa wakati wa maafa, ndiyo yale mahindi tunayowaletea huko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote, ulizaneni kwenye Halmashauri zenu; Halmashauri ambazo hazijalipa zirudishe hiyo fedha haraka sana ili iweze kufanya hiyo kazi ambayo Mheshimiwa Mbunge anaishauri.
Kwa hiyo, naomba nitoe hiyo taarifa, nadhani Mbunge atakubaliana nami Halmashauri waharakishe kurudisha hizo fedha. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Mbunge unapokea taarifa hiyo nzuri?
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Taarifa hiyo naipokea, lakini mzigo mzigo tunawakabidhi Wanyamwezi kwa maana Ofisi ya Waziri Mkuu watusaidie kulibeba hili. Huko Halmashauri ni wadogo, likiwa kwa mkubwa, Waziri Mkuu naamini litafanyiwa kazi kwa umakini mkubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme jambo moja. Nchi yetu kama Tanzania tuna advantage kubwa. Kwenye uzalishaji; productionwise na locationwise katika nchi zilizopo kwenye ukanda wa Maziwa Makuu, tuna faida kubwa. Sasa NFRA walishapewa mandate; katika dhima yao mojawapo ni kuhakikisha usalama wa chakula nchini kwa kununua, kuhifadhi na kuzungusha chakula. Kwa hiyo, wanaruhusiwa kufanya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba Waziri Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Naibu hapo, tusaidieni, kaiwezesheni hiyo ofisi ika-capitalize hayo masoko yaliyopo katika nchi za Maziwa Makuu ili tukawanusuru wakulima wetu. Kama tukiwa serious kweli kuiwezesha hii NFRA, nawahakikishieni nchi yetu tutaenda vizuri katika sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja. Ahsanteni sana. (Makofi)